Acts 23

1Paulo akawakazia macho wale wajumbe wa baraza, akasema, “Ndugu zangu, nimetimiza wajibu wangu kwa Mungu kwa dhamiri safi kabisa hadi leo.” 2Kwa ajili ya jambo hili Kuhani Mkuu Anania akaamuru wale waliokuwa karibu na Paulo wampige kofi kinywani. 3Ndipo Paulo akamwambia, “Mungu atakupiga wewe, ewe ukuta uliopakwa chokaa! Wewe umeketi hapo ili kunihukumu kwa mujibu wa sheria, lakini wewe mwenyewe unakiuka sheria kwa kuamuru kwamba nipigwe kinyume cha sheria!”

4Wale watu waliokuwa wamesimama karibu na Paulo wakamwambia, “Je, wewe wathubutu kumtukana Kuhani Mkuu wa Mungu?”

5Paulo akajibu, “Ndugu zangu, sikujua kwamba yeye alikuwa Kuhani Mkuu. Kwa maana imeandikwa, ‘Usimnenee mabaya kiongozi wa watu wako.’ ”

6Paulo alipotambua ya kuwa baadhi yao walikuwa Masadukayo na wengine ni Mafarisayo, akapaza sauti kwenye baraza, “Ndugu zangu, mimi ni Farisayo, mwana Farisayo. Hapa nimeshtakiwa kuhusu tumaini langu katika ufufuo wa wafu.” 7Aliposema haya, farakano likaanza kati ya Mafarisayo na Masadukayo na baraza lote likagawanyika. 8(Kwa maana Masadukayo wanasema kwamba hakuna ufufuo, wala hakuna malaika au roho, lakini Mafarisayo wanaamini haya yote.)

9Kukawa na ghasia kubwa, nao baadhi ya walimu wa sheria ambao ni Mafarisayo, wakasimama wakapinga kwa nguvu wakisema, “Hatuoni kosa lo lote la mtu huyu! Huenda ikawa roho au malaika amezungumza naye” 10Ugomvi ukawa mkubwa kiasi kwamba yule jemadari akahofu kuwa wangemrarua Paulo vipande vipande, akaamuru vikosi vya askari vishuke na kumwondoa Paulo katikati yao kwa nguvu na kumleta ndani ya ngome ya jeshi.

11Usiku uliofuata, Bwana akasimama karibu naye akamwambia, “Jipe moyo! Kama vile ulivyonishuhudia hapa Yerusalemu, hivyo imekupasa kunishuhudia huko Rumi pia.”

Hila Za Kumwua Paulo

12Kulipopambazuka Wayahudi wakafanya shauri pamoja na kujifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala kunywa mpaka wamemwua Paulo. 13Waliofanya mpango huo walikuwa zaidi ya watu arobaini. 14Wakawaendea viongozi wa makuhani na wazee na kusema, “Tumejifunga pamoja kwa kiapo kwamba hatutakula wala kunywa mpaka tumemwua Paulo. 15Hivyo basi, wewe pamoja na baraza, inawapasa mumjulishe jemadari ili amtelemshe Paulo kwenu, mjifanye kama mnataka kufanya uchunguzi wa kina zaidi wa shauri lake. Nasi tuko tayari kumwua kabla hajafika hapa.”

16Lakini mtoto wa dada yake Paulo aliposikia juu ya shauri hilo baya, alikwenda kule kwenye ngome ya askari na kumweleza Paulo.

17Ndipo Paulo akamwita mmoja wa wakuu wa maaskari akamwambia, “Mpeleke huyu kijana kwa jemadari, analo jambo la kumweleza.” 18Hivyo yule mkuu wa maaskari akampeleka yule kijana kwa jemadari akamwambia, “Paulo, yule mfungwa aliniita na kuniomba nimlete huyu kijana kwako, kwa sababu ana neno la kukueleza.”

19Yule jemadari akamshika yule kijana mkono, akampeleka kando na kumwuliza, “Unataka kuniambia nini?”

20Yule kijana akasema, “Wayahudi wamekubaliana wakuombe umpeleke Paulo kwenye baraza lao kesho kwa kisingizio kwamba wanataka kufanya uchunguzi wa kina wa shauri lake. 21Lakini usishawishiwe nao kwa maana zaidi ya watu arobaini wanamvizia. Wamejifunga kwa kiapo kwamba hawatakula wala kunywa mpaka wamemwua Paulo. Sasa wako tayari, wanangoja idhini yako kwa ajili ya ombi lao.”

22Yule jemadari akamruhusu yule kijana aende na akamwonya, akisema, “Usimwambie mtu ye yote kwamba umenieleza habari hizi.”

Paulo Ahamishiwa Kaisaria

23Kisha yule jemadari akawaita wakuu wake wawili wa maaskari akawaambia, “Jiandaeni kuondoka saa tatu usiku huu kuelekea Kaisaria pamoja na askari 200, wapanda farasi sabini na watu 200 wenye mikuki. 24Pia tayarisheni na farasi watakaotumiwa na Paulo, mumpeleke salama mpaka kwa mtawala Feliksi.”

25Kisha akaandika barua kwa Feliksi kama ifuatavyo:

26Klaudio Lisia,

Kwa Mtawala, Mtukufu Feliksi:

Salamu.27Mtu huyu alikamatwa na Wayahudi wakakaribia kumwua, lakini nikaja na vikosi vyangu vya maaskari nikamwokoa, kwa kuwa nilipata habari kwamba yeye ni raia wa Rumi. 28Nilitaka kujua kwa nini walikuwa wanamshutumu, hivyo nikamleta mbele ya baraza lao. 29Ndipo nikaona kuwa alikuwa anashutumiwa kwa mambo yanayohusu sheria yao, lakini hakuwa ameshtakiwa kwa jambo lo lote linalostahili kifo au kifungo. 30Nilipoarifiwa kuwa kulikuwa na shauri baya dhidi ya mtu huyu, nilimtuma kwako mara, nikiwaagiza washtaki wake pia waeleze mbele yako mashtaka yao dhidi yake.31Hivyo maaskari, kwa kufuata maelekezo waliyopewa, wakamchukua Paulo wakati wa usiku na kumleta mpaka Antipatri. 32Kesho yake wakawaacha wale wapanda farasi waendelee na safari wakiwa na Paulo, wakati wao walirudi kwenye ngome ya maaskari. 33Walipofika Kaisaria kumpa mtawala ile barua, walimkabidhi pia Paulo kwake. 34Mtawala alipokwisha kuisoma ile barua alimwuliza Paulo kwamba alikuwa mtu wa jimbo gani. Alipojua kuwa anatoka Kilikia, 35alisema, “Nitasikiliza shauri lako washtaki wako watakapofika hapa.” Kisha akaamuru Paulo awekwe chini ya ulinzi kwenye jumba la kifalme la Herode.

Copyright information for Neno