Acts 24

Mbele Ya Feliksi Huko Kaisaria

Baada ya siku tano, Kuhani Mkuu Anania akashuka akiwa amefuatana na baadhi ya wazee pamoja na mwanasheria mmoja aitwaye Tertulo, nao wakaleta mashtaka yao dhidi ya Paulo mbele ya mtawala. Paulo alipoitwa aingie ndani, Tertulo akaanza kutoa mashtaka akisema, “Mtukufu Feliksi, kwa muda mrefu tumefurahia amani na matengenezo mengi mazuri yamefanywa kwa ajili ya watu hawa kwa sababu ya upeo wako wa kuona mambo ya mbele. Wakati wote na kila mahali, kwa namna yo yote, mtukufu sana Feliksi, tumeyapokea mambo haya yote kwa shukrani nyingi. Lakini nisije nikakuchosha zaidi, ningekuomba kwa hisani yako utusikilize kwa kifupi.

“Tumemwona mtu huyu kuwa ni msumbufu, anayechochea ghasia miongoni mwa Wayahudi duniani pote. Yeye ndiye kiongozi wa dhehebu la Wanazarayo, na hata amejaribu kulinajisi Hekalu, hivyo tukamkamata tukataka kumhukumu kufuatana na sheria zetu. Lakini jemadari Lisia, alitujia na nguvu nyingi akamwondoa mikononi mwetu, akiwaamuru washtaki wake waje mbele yako: ili kwa kumchunguza wewe mwenyewe unaweza kujua kutoka kwake mambo yote yale tunayomshtaki kwayo.”

Pia wale Wayahudi wakaunga mkono wakithibitisha kuwa mashtaka yote haya ni kweli.

Paulo Ajitetea Mbele Ya Feliksi

10 Mtawala Feliksi alipompungia Paulo mkono ili ajitetee, yeye akajibu, “Najua kwamba wewe umekuwa hakimu katika taifa hili kwa miaka mingi, hivyo natoa utetezi wangu kwa furaha. 11 Unaweza kuhakikisha kwa urahisi kuwa hazijapita zaidi ya siku kumi na mbili tangu nilipopanda kwenda Yerusalemu kuabudu. 12 Hawa wanaonishtaki hawakunikuta nikibishana na mtu ye yote Hekaluni au kuchochea umati wa watu katika sinagogi au mahali pengine po pote mjini. 13 Wala hawawezi kabisa kukuthibitishia mashtaka haya wanayonishtaki kwayo. 14 Lakini, ninakubali kwamba mimi namwabudu Mungu wa baba zetu, mfuasi wa Njia, ile ambayo wao wanaiita dhehebu. Ninaamini kila kitu kinachokubaliana na Sheria na kile kilichoandikwa katika Manabii, 15 nami ninalo tumaini kwa Mungu, ambalo hata wao wenyewe wanalikubali kwamba kutakuwa na ufufuo wa wafu, kwa wote wenye haki na wasio na haki. 16 Kwa hiyo ninajitahidi siku zote kuwa na dhamiri safi mbele za Mungu na mbele za wanadamu.

17 “Basi, baada ya kutokuwapo kwa miaka mingi nilikuja Yerusalemu ili kuwaletea watu wangu msaada kwa ajili ya maskini na kutoa dhabihu. 18 Nilikuwa nimeshatakaswa kwa taratibu za kiibada waliponikuta Hekaluni nikifanya mambo haya. Hapakuwa na umati wa watu, pamoja nami wala aliyehusika kwenye fujo yo yote. 19 Lakini kulikuwa na baadhi ya Wayahudi kutoka Asia, ambao wangelazimika wawepo hapa mbele yako ili watoe mashtaka kama wanalo jambo lo lote dhidi yangu. 20 Au, watu hawa walioko hapa waseme ni uhalifu gani walioniona nao waliponisimamisha mbele ya baraza, 21 isipokuwa ni kuhusu jambo hili moja nililopiga kelele mbele yao kwamba, ‘Mimi nashtakiwa mbele yako leo kwa sababu ya ufufuo wa wafu.’ ”

22 Basi Feliksi ambaye alikuwa anafahamu vizuri habari za Njia ile, akaahirisha shauri lile kwa maelezo yake akisema, “Wakati jemadari Lisia atakapotelemka huku, nitaamua shauri lako.” 23 Ndipo akaamuru mkuu wa maaskari amweke chini ya ulinzi lakini ampe uhuru na kuwaruhusu rafiki zake wamhudumie.

24 Baada ya siku kadhaa Feliksi alipokuja pamoja na Drusila mkewe, ambaye alikuwa Myahudi, alituma aitiwe Paulo na kumsikiliza alipokuwa akinena juu ya imani katika Yesu Kristo. 25 Naye Paulo alipokuwa akinena juu ya haki, kuwa na kiasi na juu ya hukumu ijayo, Feliksi aliingiwa na hofu na kusema, “Hiyo yatosha sasa! Waweza kuondoka. Nitakapokuwa na wasaa nitakuita.” 26 Wakati huo huo Feliksi alitazamia kwamba Paulo angempatia rushwa. Hivyo akawa anamwita mara kwa mara na kuzungumza naye.

27 Baada ya miaka miwili kupita, Porkio Festo akaingia kwenye utawala mahali pa Feliksi, lakini kwa kuwa Feliksi alitaka kuwapendeza Wayahudi, akamwacha Paulo gerezani.

Copyright information for Neno