Acts 10

Kornelio Amwita Petro

1Katika mji wa Kaisaria palikuwa na mtu jina lake Kornelio, ambaye alikuwa jemadari wa kile kilichojulikana kama kikosi cha Kiitalia. 2Yeye alikuwa mcha Mungu pamoja na wote wa nyumbani mwake. Aliwapa watu sadaka nyingi na kumwomba Mungu daima. 3Siku moja alasiri, yapata saa tisa, aliona maono waziwazi, malaika wa Mungu akimjia na kumwambia, “Kornelio!”

4Kornelio akamkazia macho kwa hofu akasema, “Kuna nini, Bwana?”

Malaika akamwambia, “Sala zako na sadaka zako kwa maskini zimefika juu na kuwa ukumbusho mbele za Mungu.
5Sasa tuma watu waende Yafa wakamwite mtu mmoja jina lake Simoni aitwaye Petro. 6Yeye anaishi na Simoni mtengenezaji ngozi ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.”

7Yule malaika aliyekuwa akizungumza naye alipoondoka, Kornelio akawaita watumishi wake wawili pamoja na askari mmoja mcha Mungu aliyekuwa miongoni mwa wale waliomtumikia. 8Akawaambia mambo yote yaliyotukia, kisha akawatuma waende Yafa.

Maono Ya Petro

9Siku ya pili yake, walipokuwa wameukaribia mji, wakati wa adhuhuri, Petro alipanda juu ghorofani kuomba. 10Alipokuwa akiomba akahisi njaa, akatamani kupata chakula. Lakini wakati walipokuwa wakiandaa akalala usingizi mzito sana. 11Akaona mbingu zimefunguka na kitu kama nguo kubwa kikishushwa kwa ncha zake nne. 12Ndani yake walikuwepo aina zote za wanyama wenye miguu minne, nao watambaao na ndege wa angani. 13Ndipo sauti ikamwambia “Petro, ondoka, uchinje na ule.”

14Petro akajibu, “La Bwana! Sijawahi kamwe kula kitu cho chote kilicho najisi.”

15Ile sauti ikasema naye tena mara ya pili, “Usikiite najisi kitu cho chote alichokitakasa Bwana.”

16Jambo hili likatukia mara tatu na ghafula ile nguo ikarudishwa mbinguni.

17Wakati Petro akiwa bado anajiuliza kuhusu maana ya maono haya, wale watu waliokuwa wametumwa na Kornelio wakaipata nyumba ya Simoni mtengenezaji wa ngozi wakawa wamesimama mbele ya lango. 18Wakabisha hodi na kuuliza kama Simoni aliyeitwa Petro alikuwa anaishi hapo.

19Wakati Petro akiwa anafikiria juu ya yale maono, Roho Mtakatifu akamwambia, “Simoni, wako watu watatu wanaokutafuta. 20Inuka na ushuke, usisite kwenda nao kwa kuwa mimi nimewatuma.”

21Petro akashuka na kuwaambia wale watu waliokuwa wametumwa kutoka kwa Kornelio, “Mimi ndiye mnayenitafuta. Mmekuja kwa sababu gani?”

22Wale watu wakamjibu, “Tumetumwa na kamanda Kornelio ambaye ni mtu mwema anayemcha Mungu na kusifiwa na Wayahudi wote. Yeye ameagizwa na malaika wa Mungu akukaribishe nyumbani kwake, ili asikilize maneno utakayomwambia.” 23Basi Petro akawakaribisha wakafuatana naye ndani akawapa pa kulala. Kesho yake akaondoka pamoja nao, akifuatana na baadhi ya ndugu kutoka Yafa.

Petro Nyumbani Mwa Kornelio

24Siku iliyofuata wakawasili Kaisaria. Kornelio alikuwa akiwangoja pamoja na jamaa yake na marafiki zake wa karibu. 25Petro alipokuwa akiingia ndani, Kornelio alikuja kumlaki, akaanguka miguuni pake kwa heshima. 26Lakini Petro akamwinua akamwambia, “Simama, mimi ni mwanadamu tu.”

27Petro alipokuwa akizungumza naye akaingia ndani na kukuta watu wengi wamekusanyika. 28Akawaambia, “Mnajua kabisa kwamba ni kinyume cha sheria yetu Myahudi kuchangamana na mtu Mataifa au kumtembelea. Lakini Mungu amenionyesha kwamba nisimwite mtu ye yote kuwa najisi au asiye safi. 29Ndiyo sababu ulipotuma niitwe nilikuja bila kupinga lo lote. Basi sasa naomba unieleze kwa nini umeniita?”

30Kornelio akajibu, “Siku nne zilizopita, nilikuwa nyumbani nikisali saa kama hii, saa tisa alasiri. Ghafula mtu mwenye nguo za kumetameta akasimama mbele yangu, 31akasema, ‘Kornelio, maombi yako yamesikiwa na sadaka zako zimekumbukwa mbele za Mungu. 32Basi tuma watu waende Yafa wakaulize mtu mmoja Simoni aitwaye Petro, yeye ni mgeni katika nyumba ya Simoni mtengenezaji ngozi, ambaye nyumba yake iko kando ya bahari.’ 33Nilituma watu kwako mara moja, nawe umefanya vyema kuja. Basi sasa sisi sote tuko hapa mbele za Mungu kuyasikiliza yote ambayo Bwana amekuamuru kutuambia.”

Hotuba Ya Petro

34Ndipo Petro akafumbua kinywa chake akasema, “Mungu hana upendeleo, 35Lakini katika kila taifa, kila mtu amchaye na kutenda yaliyo haki hukubaliwa naye. 36Ninyi mnajua ule ujumbe uliotumwa kwa Israeli, ukitangaza habari njema za amani kwa Yesu Kristo. Yeye ni Bwana wa wote. 37Mnajua yale yaliyotukia katika Uyahudi wote kuanzia Galilaya baada ya mahubiri ya Yohana Mbatizaji: 38Jinsi Mungu alivyomtia Yesu wa Nazareti mafuta katika Roho Mtakatifu na jinsi alivyokwenda huku na huko akitenda mema na kuponya wote waliokuwa wameonewa na nguvu za Shetani, kwa sababu Mungu alikuwa pamoja naye.

39“Sisi ni mashahidi wa mambo yote aliyoyafanya katika Uyahudi na Yerusalemu. Wakamwua kwa kumtundika msalabani. 40Lakini Mungu alimfufua kutoka kwa wafu siku ya tatu na akamwezesha kuonekana na watu. 41Hakuonekana kwa watu wote, lakini kwetu sisi tuliochaguliwa na Mungu kuwa mashahidi, ambao tulikula na kunywa naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu. 42Naye alituamuru kuhubiri kwa watu wote na kushuhudia kwamba yeye ndiye aliyetiwa mafuta na Mungu kuwa hakimu wa walio hai na wafu. 43Manabii wote walishuhudia juu yake kwamba kila mtu amwaminiye hupokea msamaha wa dhambi katika Jina lake.”

Watu Mataifa Wapokea Roho Mtakatifu

44Wakati Petro akiwa anasema maneno hayo, Roho Mtakatifu aliwashukia wote waliokuwa wakisikiliza ule ujumbe. 45Wale wa tohara walioamini waliokuwa wamekuja pamoja na Petro walishangaa kuona kuwa kipawa cha Roho Mtakatifu kimemwagwa juu ya watu Mataifa. 46Kwa kuwa waliwasikia wakinena kwa lugha mpya na kumwadhimisha Mungu.

Ndipo Petro akasema,
47“Je, kuna mtu ye yote anayeweza kuzuia watu hawa wasibatizwe kwa maji? Wamempokea Roho Mtakatifu kama sisi tulivyompokea.” 48Kwa hiyo akaamuru wabatizwe kwa jina la Yesu Kristo. Wakamsihi Petro akae nao kwa siku chache.

Copyright information for Neno