Acts 11

Petro Aeleza Alivyotumwa Kwa Watu Mataifa

1Mitume na ndugu walioamini waliokuwa huko Uyahudi wakasikia kuwa watu Mataifa nao wamepokea neno la Mungu. 2Hivyo Petro alipopanda Yerusalemu, wale wa tohara waliokuwa wameamini wakamshutumu, 3wakisema, “Ulikwenda kwa watu wasiotahiriwa na kula pamoja nao.”

4Ndipo Petro akaanza kuwaeleza kuhusu mambo yote yalivyotokea hatua kwa hatua akisema, 5“Nilikuwa katika mji wa Yafa nikiomba, nami nikapitiwa na usingizi wa ghafula, nikaona maono. Kulikuwa na kitu kama nguo kubwa ikishuka kutoka mbinguni, ikishushwa kwa ncha zake nne, nayo ikanikaribia. 6Nilipoangalia ndani yake kwa karibu niliona wanyama wenye miguu minne, wanyama wa mwitu, watambaao na ndege wa angani. 7Ndipo nikasikia sauti ikiniambia ‘Petro, ondoka uchinje ule.’

8“Nikajibu, ‘La hasha Bwana! Kitu cho chote kilicho najisi hakijaingia kinywani mwangu.’

9“Sauti ikasema kutoka mbinguni mara ya pili, ‘Usikiite najisi kitu cho chote Mungu alichokitakasa.’ 10Jambo hili lilitokea mara tatu, ndipo kile kitu kikavutwa tena mbinguni.

11“Wakati ule ule watu watatu, waliokuwa wametumwa kutoka Kaisaria waliwasili katika nyumba niliyokuwa nikikaa. 12Roho Mtakatifu akaniambia niende nao bila kuwa na ubaguzi kati yao na sisi. Hawa ndugu sita pia walifuatana nami, nasi tukaingia nyumbani mwa huyo Kornelio. 13Akatuambia jinsi alivyoona malaika aliyekuwa amesimama katika nyumba yake na kusema, ‘Tuma watu waende Yafa wakamlete Simoni aitwaye Petro. 14Yeye atakupa ujumbe ambao kwa huo wewe na wa nyumbani mwako wote mtaokoka.’

15“Nami nilipoanza kusema, Roho Mtakatifu akashuka juu yao kama vile alivyotushukia sisi hapo mwanzo. 16Nami nikakumbuka neno la Bwana alivyosema, ‘Yohana alibatiza kwa maji, lakini ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu.’ 17Basi ikiwa Mungu aliwapa hawa watu kipawa kile kile alichotupa sisi tuliomwamini Bwana Yesu, mimi ni nani hata nifikirie kuwa ningeweza kumpinga Mungu?”

18Waliposikia haya hawakuwa na la kupinga zaidi. Nao wakamwadhimisha Mungu wakisema, “Basi, Mungu amewapa hata watu Mataifa toba iletayo uzima wa milele.”

Kanisa Huko Antiokia

19Basi wale waliotawanyika kwa ajili ya mateso yaliyotokana na kifo cha Stefano, wakasafiri hadi Foinike na Kipro na Antiokia. Nao hawakuhubiri lile Neno kwa mtu ye yote isipokuwa Wayahudi. 20Lakini baadhi yao walikuwapo watu wa Kipro na Kirene, ambao walipokuja Antiokia walinena na Wayunani pia wakimhubiri Bwana Yesu. 21Mkono wa Bwana ulikuwa pamoja nao, nayo idadi kubwa ya watu wakaamini na kumgeukia Bwana.

22Habari hizi zilipofika masikioni mwa kanisa huko Yerusalemu, wakamtuma Barnaba aende Antiokia. 23Alipofika na kuona madhihirisho ya neema ya Mungu, akafurahi na kuwatia moyo waendelee kuwa waaminifu kwa Bwana kwa mioyo yao yote. 24Barnaba alikuwa mtu mwema, aliyejaa Roho Mtakatifu, mwenye imani, nayo idadi kubwa ya watu wakaongezeka kwa Bwana.

25Kisha Barnaba akaenda Tarso kumtafuta Sauli, 26naye alipompata akamleta Antiokia. Hivyo kwa mwaka mzima Barnaba na Sauli wakakutana na kanisa na kufundisha idadi kubwa ya watu. Ilikuwa ni katika kanisa la Antiokia kwa mara ya kwanza wanafunzi waliitwa Wakristo.

27Wakati huo manabii walishuka toka Yerusalemu hadi Antiokia. 28Mmoja wao, jina lake Agabo, akasimama akatabiri kwa uweza wa Roho Mtakatifu kwamba njaa kubwa itaenea ulimwengu mzima. Njaa hiyo ilitokea wakati wa utawala wa Klaudio. 29Mitume wakaamua kwamba kila mtu, kulingana na uwezo wake alio nao, atoe msaada kwa ajili ya ndugu wanaoishi Uyahudi. 30Wakafanya hivyo, misaada yao ikapelekwa kwa wazee kwa mikono ya Barnaba na Sauli.

Copyright information for Neno