Acts 5

Anania Na Safira

1Lakini mtu mmoja jina lake Anania pamoja na mkewe Safira waliuza kiwanja. 2Mkewe akijua kikamilifu, Anania alificha sehemu ya fedha alizopata, akaleta kiasi kilichobaki na kukiweka miguuni pa mitume.

3Petro akamwuliza, “Anania, mbona Shetani ameujaza moyo wako ili kumwambia uongo Roho Mtakatifu, ukaficha sehemu ya fedha ulizopata kutokana na kiwanja? 4Je, kabla hujauza hicho kiwanja si kilikuwa mali yako? Hata baada ya kukiuza, fedha ulizopata si zilikuwa kwenye uwezo wako? Kwa nini basi umewaza hila hii moyoni mwako kufanya jambo kama hili? Wewe hukumwambia uongo mwanadamu bali Mungu.”

5Anania aliposikia maneno haya akaanguka chini na kufa. Hofu kuu ikawapata wote waliosikia jambo lililokuwa limetukia. 6Vijana wakaja, wakaufunga mwili wake sanda, wakamchukua nje kumzika.

7Saa tatu baadaye mkewe Anania akaingia, naye hana habari ya mambo yaliyotukia. 8Petro akamwuliza, “Niambie, je, mliuza kiwanja kwa thamani hii?” Akajibu, “Ndiyo, tuliuza kwa thamani hiyo.”

9Ndipo Petro akamwambia, “Imekuwaje mkakubaliana kumjaribu Roho Mtakatifu wa Bwana? Tazama! Nyayo za vijana waliomzika mumeo ziko mlangoni, wewe nawe watakuchukua nje.”

10Saa ile ile akaanguka chini miguuni mwake na kufa, wale vijana wakaingia, wakamkuta amekufa, wakamchukua wakamzika kando ya mumewe. 11Hofu kuu ikalipata kanisa lote pamoja na watu wote waliosikia juu ya matukio haya.

Mitume Waponya Wengi

12Mitume wakafanya ishara nyingi na miujiza miongoni mwa watu. Nao wale wote walioamini walikuwa wakikusanyika katika ukumbi wa Solomoni kwa nia moja. 13Hakuna mtu mwingine aliyethubutu kuambatana nao ijapokuwa waliheshimiwa sana na watu. 14Lakini wengi walioamini idadi kubwa ya wanaume na wanawake wakaongezeka kwa Bwana. 15Hata wakawa wanawaleta wagonjwa na kuwalaza kwenye magodoro na kwenye vitanda barabarani ili yamkini Petro akipita kivuli chake kiwaguse baadhi yao. 16Pia watu wakakusanyika kutoka katika miji iliyokuwa karibu na Yerusalemu, wakileta wagonjwa na watu walioteswa na pepo wachafu, hao wote wakaponywa.

Mitume Washtakiwa

17Kisha Kuhani Mkuu na wenzake wote waliokuwa pamoja naye (ambao ni wa kundi la Masadukayo), wakiwa wamejawa na wivu, 18wakawakamata mitume na kuwatia gerezani. 19Lakini wakati wa usiku malaika wa Bwana akaja akafungua milango ya gereza akawatoa nje akawaambia, 20“Nendeni, mkasimame Hekaluni mkawaambie watu maneno yote ya uzima huu mpya.”

21Waliposikia haya wakaenda Hekaluni alfajiri wakaendelea kufundisha watu.

Kuhani Mkuu na wale waliokuwa pamoja nao walipowasili, alikusanya baraza na wazee wote wa Israeli wakatuma wale mitume waletwe kutoka gerezani.
22Lakini wale walinzi wa Hekalu walipokwenda gerezani hawakuwakuta wale mitume mle. Kwa hiyo wakarudi na kutoa habari. 23Wakasema, “Tumekuta milango ya gereza imefungwa sawasawa na maaskari wa gereza wamesimama nje ya mlango, lakini tulipofungua milango hakuwepo mtu ye yote ndani.” 24Basi mkuu wa walinzi wa Hekalu, viongozi na makuhani waliposikia haya, wakafadhaika na kushangaa sana kwa ajili yao kwamba jambo hili litakuwaje.

25Ndipo mtu mmoja akaja akawaambia, “Tazameni watu wale mliowatia gerezani wako Hekaluni wakiwafundisha watu.” 26Ndipo yule mkuu wa walinzi wa Hekalu wakaenda pamoja na maaskari wakawaleta wale mitume, lakini bila ghasia kwa sababu waliogopa kupigwa mawe na watu.

27Wakiisha kuwaleta hao mitume wakawaamuru kusimama mbele ya baraza. Kuhani Mkuu akawahoji. 28“Tuliwaonya kwa nguvu msifundishe kwa jina hili, lakini ninyi mmeijaza Yerusalemu yote mafundisho yenu na tena mmekusudia kuleta damu ya mtu huyu juu yetu.”

29Petro na wale mitume wengine wakajibu, “Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. 30Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu kutoka kwa wafu, ambaye ninyi mlimwua kwa kumtundika kwenye msalaba. 31Mungu alimtukuza akamweka mkono wake wa kuume kuwa Kiongozi na Mwokozi ili awape Israeli toba na msamaha wa dhambi. 32Nasi tu mashahidi wa mambo haya, vivyo hivyo na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wale wanaomtii.”

33Wale wajumbe wa baraza la wazee waliposikia haya, walijawa na ghadhabu, wakataka kuwaua wale mitume. 34Lakini Farisayo mmoja, jina lake Gamalieli, aliyekuwa mwalimu wa sheria, aliyeheshimiwa na watu wote, akasimama mbele ya baraza akaamuru wale mitume watolewe nje kwa muda. 35Ndipo alipowaambia wajumbe wa baraza, “Enyi watu wa Israeli, fikirini kwa uangalifu yale mnayotaka kuwatendea watu hawa. 36Kwa maana wakati uliopita aliinuka mtu mmoja jina lake Theuda ambaye alijidai kuwa yeye ni mtu maarufu, akapata wafuasi wapatao 400 walioambatana naye. Lakini aliuawa na wafuasi wake wote wakatawanyika na kupotea. 37Baada yake alitokea Yuda Mgalilaya wakati ule wa kuandikwa orodha ya watu akaongoza kundi la watu kuasi. Yeye naye aliuawa, nao wafuasi wake wakatawanyika. 38Kwa hiyo, kwa habari ya jambo hili nawashauri, jiepusheni na watu hawa. Waacheni waende zao! Kwa maana kama kusudi lao na shughuli yao imetokana na mwanadamu haitafanikiwa. 39Lakini ikiwa imetoka kwa Mungu hamtaweza kuwazuia watu hawa, badala yake mtajikuta mnapigana dhidi ya Mungu”

40Wakapokea ushauri wa Gamalieli. Wakawaita mitume ndani, wakaamuru wachapwe mijeledi, kisha wakawaagiza wasinene tena kwa jina la Yesu, nao wakawaachia waende zao.

41Wale mitume walitoka nje ya baraza, wakiwa wamejaa furaha kwa sababu wamehesabiwa kustahili kupata aibu kwa ajili ya jina la Yesu. 42Kila siku, Hekaluni na nyumba kwa nyumba, hawakuacha kufundisha na kuhubiri habari njema kwamba Yesu ndiye Kristo
5:42 Yaani Masiya
.

Copyright information for Neno