Acts 9

Kuongoka Kwa Sauli

1Wakati ule ule, Sauli alikuwa bado anazidisha vitisho vya kuua wanafunzi wa Bwana, akamwendea Kuhani Mkuu, 2naye akamwomba Kuhani Mkuu ampe barua ya kwenda kwenye masinagogi huko Dameski, ili akimkuta mtu ye yote wa Njia Ile, akiwa mwanaume au mwanamke, aweze kuwafunga na kuwaleta Yerusalemu. 3Basi akiwa katika safari yake, alipokaribia Dameski, ghafula nuru kutoka mbinguni ikamwangaza kotekote. 4Akaanguka chini, akasikia sauti ikimwambia, “Sauli, Sauli, mbona unanitesa?”

5Sauli akajibu, “U nani wewe, Bwana?”

Ile sauti ikajibu, “Mimi ni Yesu unayemtesa.”
6“Sasa inuka uingie mjini, nawe utaambiwa yakupasayo kutenda.”

7Watu wale waliokuwa wakisafiri pamoja na Sauli wakasimama bila kuwa na la kusema, kwa sababu walisikia sauti lakini hawakumwona aliyekuwa akizungumza. 8Sauli akainuka kutoka pale chini na alipojaribu kufungua macho yake hakuweza kuona kitu cho chote. Basi wakamshika mkono wakamwongoza mpaka Dameski. 9Naye kwa muda wa siku tatu alikuwa kipofu naye hakula wala kunywa cho chote.

10Huko Dameski alikuwepo mwanafunzi mmoja jina lake Anania. Bwana alimwita katika maono, “Anania!”

Akajibu, “Mimi hapa Bwana.”

11Bwana akamwambia, “Ondoka uende katika barabara iitwayo Nyofu ukaulize katika nyumba ya Yuda mtu kutoka Tarso, jina lake Sauli, kwa maana wakati huu anaomba, 12katika maono amemwona mtu aitwaye Anania akija na kuweka mikono juu yake ili apate kuona tena.”

13Anania akajibu, “Bwana, nimesikia kutoka kwa watu wengi habari nyingi kuhusu mtu huyu na madhara yote aliyowatendea watakatifu wako huko Yerusalemu. 14Naye amekuja hapa Dameski akiwa na mamlaka kutoka kwa viongozi wa makuhani ili awakamate wote wanaotaja jina lako.”

15Lakini Bwana akamwambia Anania, “Nenda! Mtu huyu ni chombo changu kiteule nilichokichagua, apate kulichukua Jina langu kwa watu Mataifa na wafalme wao na mbele ya watu wa Israeli. 16Nami nitamwonyesha jinsi impasavyo kuteseka kwa ajili ya Jina langu.”

17Kisha Anania akaenda kwenye ile nyumba, akaingia ndani. Akaweka mikono yake juu ya Sauli akasema, “Ndugu Sauli, Bwana Yesu aliyekutokea njiani amenituma kwako ili upate kuona tena na ujazwe Roho Mtakatifu.” 18Ghafula vitu kama magamba vikaanguka chini, kutoka machoni mwa Sauli, akapata kuona tena. Akasimama, akabatizwa. 19Baada ya kula chakula, akapata nguvu tena. Sauli akakaa siku kadhaa pamoja na wanafunzi huko Dameski.

Sauli Ahubiri Dameski

20Papo hapo akaanza kuhubiri kwenye masinagogi kwamba “Yesu Kristo ni Mwana wa Mungu” 21Watu wote waliomsikia Sauli walishangaa na kuuliza, “Huyu si yule mtu aliyesababisha maangamizi makuu miongoni mwa watu waliolitaja jina hili? Naye si amekuja hapa kwa kusudi la kuwakamata na kuwapeleka wakiwa wamefungwa mbele ya viongozi wa makuhani?” 22Sauli akazidi kuwa uhodari na kuwashangaza Wayahudi walioishi Dameski kwa kuthibitisha kuwa Yesu ndiye Kristo
9:22 Yaani Masiya
.

23Baada ya siku nyingi kupita, Wayahudi wakafanya shauri kumwua Sauli. 24Lakini shauri lao likajulikana kwa Sauli. Wayahudi wakawa wanalinda malango yote ya mji, mchana na usiku ili wapate kumwua. 25Lakini wafuasi wake wakamchukua usiku wakamshusha akiwa ndani ya kapu kupitia mahali penye nafasi ukutani.

Sauli Huko Yerusalemu

26Sauli alipofika Yerusalemu akajaribu kujiunga na wanafunzi lakini wote walimwogopa, kwa maana hawakuamini kwamba kweli naye alikuwa mwanafunzi. 27Lakini Barnaba akamchukua, akampeleka kwa wale mitume. Akawaeleza jinsi Sauli akiwa njiani alivyomwona Bwana, jinsi Bwana alivyosema naye na jinsi alivyohubiri kwa ujasiri kwa jina la Yesu huko Dameski. 28Kwa hiyo Sauli akakaa nao akishirikiana nao na akihubiri waziwazi kwa jina la Yesu kila mahali huko Yerusalemu. 29Alinena na kuhojiana na Wayahudi wenye asili ya Kiyunani lakini wao walijaribu kumwua. 30Wale ndugu walipopata habari wakampeleka hadi Kaisaria, wakamsafirisha kwenda Tarso.

31Ndipo kanisa katika Uyahudi wote, Galilaya na Samaria likafurahia wakati wa amani. Likatiwa nguvu na likaendelea kudumu katika kumcha Bwana na kwa faraja ya Roho Mtakatifu, idadi yake ikazidi kuongezeka.

Kuponywa Kwa Ainea

32Petro alipokuwa akisafiri sehemu mbalimbali, alikwenda kuwatembelea watakatifu walioishi huko Lida. 33Huko alimkuta mtu mmoja aitwaye Ainea, ambaye alikuwa amepooza na kwa muda wa miaka minane alikuwa hajaondoka kitandani. 34Petro akamwambia, “Ainea, Yesu Kristo anakuponya, inuka utandike kitanda chako.” Mara Ainea akainuka. 35Watu wote wa Lida na Sharoni walipomwona Ainea akitembea wakamgeukia Bwana.

Petro Amfufua Dorkasi

36Huko Yafa palikuwa na mwanafunzi jina lake Tabitha (ambalo kwa Kiyunani ni Dorkasi
9:36 Tabitha kwa Kiaramu na Dorkasi kwa Kiaramu yote yamaanisha Paa
). Huyu alikuwa mkarimu sana, akitenda mema na kuwasaidia maskini.
37Wakati huo akaugua, akafa na wakiisha kuuosha mwili wake wakauweka katika chumba cha ghorofani. 38Kwa kuwa Yafa hapakuwa mbali sana na Lida, wanafunzi waliposikia kwamba Petro yuko huko waliwatuma watu wawili kwake ili kumwomba, “Tafadhali njoo huku pasipo kukawia.”

39Kwa hiyo Petro akainuka akaenda nao, naye alipowasili, wakampeleka hadi kwenye chumba cha ghorofani alipokuwa amelazwa. Wajane wengi walisimama karibu naye wakilia na kuonyesha majoho na nguo nyingine ambazo Dorkasi alikuwa amewashonea alipokuwa pamoja nao.

40Petro akawatoa wote nje ya kile chumba, kisha akapiga magoti akaomba, akaugeukia ule mwili akasema, “Tabitha, inuka.” Akafumbua macho yake na alipomwona Petro, akaketi. 41Petro akamshika mkono akamwinua, ndipo akawaita wale watakatifu na wajane akamkabidhi kwao akiwa hai. 42Habari hizi zikajulikana sehemu zote za Yafa na watu wengi wakamwamini Bwana. 43Petro akakaa Yafa kwa siku nyingi akiishi na Simoni mtengenezaji ngozi.

Copyright information for Neno