Amos 2

1Hili ndilo asemalo BWANA: “Kwa dhambi tatu za Moabu,
hata kwa dhambi nne,
sitazuia ghadhabu yangu.
Kwa sababu alichoma mifupa ya mfalme wa Edomu,
ikawa kama chokaa.
2Nitatuma moto juu ya Moabu
ambao utateketeza ngome ya Keriothi.
Moabu ataanguka kwa ghasia kubwa
katikati ya vilio vya vita na mlio wa tarumbeta.
3Nitamwangamiza mtawala wake
na kuwaua maafisa wake wote pamoja naye,”
asema BWANA.4Hili ndilo asemalo BWANA: “Kwa dhambi tatu za Yuda,
hata kwa dhambi nne,
sitaizuia ghadhabu yangu.
Kwa sababu wameikataa sheria ya BWANA
na hawakuzishika amri zake,
kwa sababu wamepotoshwa na miungu ya uongo,
miungu ambayo babu zao waliifuata.
5Nitatuma moto juu ya Yuda
ambao utateketeza ngome za Yerusalemu.”


Hukumu Juu Ya Israeli

6Hili ndilo asemalo BWANA: “Kwa dhambi tatu za Israeli,
hata kwa dhambi nne,
sitaizuia ghadhabu yangu.
Wanawauza wenye haki kwa fedha,
na maskini kwa jozi ya viatu.
7Wanakanyaga juu ya vichwa vya maskini
kama vile juu ya mavumbi ya nchi
na kukataa haki kwa walioonewa.
Baba na mwanawe hushiriki msichana mmoja,
kwa hivyo hulinajisi Jina langu takatifu.
8Watu hulala kando ya kila madhabahu
juu ya nguo zilizowekwa rehani.
Katika nyumba ya mungu wao hunywa mvinyo
ulionunuliwa kwa fedha walizotozwa watu.
9“Nilimwangamiza Mwamori mbele yao,
ingawa alikuwa mrefu kama mierezi
na mwenye nguvu kama mialoni.
Niliyaangamiza matunda yake juu
na mizizi yake chini.
10“Nilikupandisha toka Misri,
na nikawaongoza miaka arobaini jangwani
niwape nchi ya Waamori.
11Pia niliinua manabii kutoka miongoni mwa wana wenu
na Wanadhiri kutoka miongoni
mwa vijana wenu wa kiume.
Je, hii si kweli, Enyi watu wa Israeli?”
asema BWANA.

12“Lakini mliwafanya Wanadhiri kunywa mvinyo
na kuwaamuru manabii wasitoe unabii.
13“Sasa basi, nitawaponda
kama gari lipondavyo
wakati limejazwa nafaka.
14Mkimbiaji hodari hatanusurika,
wenye nguvu wataishiwa nguvu zao
na shujaa hataweza kuokoa maisha yake.
15Mpiga upinde atakimbia,
askari wapiga mbio hawataweza kutoroka,
na mpanda farasi hataokoa maisha yake.
16Hata askari walio mashujaa sana
siku hiyo watakimbia uchi,”
asema BWANA.Copyright information for Neno