Amos 5

Maombolezo Na Wito Wa Toba

1Sikia neno hili, Ee nyumba ya Israeli, ombolezo hili ninalifanya kuwahusu ninyi: 2“Bikira Israeli ameanguka,
kamwe hatainuka tena,
ameachwa pweke katika nchi yake,
hakuna ye yote wa kumwinua.”3Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “Wakati mmoja wa miji yako utakapopeleka watu elfu moja vitani,
mia moja tu watarudi;
wakati mji utakapopeleka mia moja,
kumi tu ndio watarudi hai.”4Hili ndilo BWANA asemalo kwa nyumba ya Israeli: “Nitafuteni mpate kuishi,
5Msitafute Betheli,
msiende Gilgali,
msisafiri kwenda Beer-Sheba.
Kwa maana kwa hakika Gilgali itakwenda uhamishoni,
na Betheli itakuwa si kitu
5:5 Yaani aveni kwa Kiebrania, kumaanisha Beth-Aveni, jina lingine la Betheli kwa dhihaka
.”
6Mtafuteni BWANA mpate kuishi,
au atafagia nyumba ya Yosefu kama moto;
utawateketeza,
nayo Betheli haitakuwa
na ye yote wa kuuzima.
7Ninyi ambao mnageuza haki kuwa uchungu
na kuiangusha haki chini
8(yeye ambaye alifanya Kilimia na Orioni,
ambaye hugeuza giza kuwa mapambazuko
na mchana kuwa usiku,
ambaye huyaita maji ya bahari
na kuyamwaga juu ya uso wa nchi:
BWANA ndilo jina lake;
9yeye hufanya maangamizo kwenye ngome
na kufanya mji uliozungushiwa ngome kuwa ukiwa),
10mnamchukia yule akemeaye mahakamani,
na kumdharau yule ambaye husema kweli.
11Mnamgandamiza maskini
na kumlazimisha awape nafaka.
Kwa hiyo, ingawa mmejenga majumba ya mawe ya fahari,
hamtaishi ndani yake;
ingawa mmepanda mashamba mazuri ya mizabibu,
hamtakunywa divai yake.
12Kwa kuwa ninajua hesabu ya makosa yenu
na ukubwa wa dhambi zenu.
Mmewaonea wenye haki na kupokea rushwa
na kuzuia haki ya maskini mahakamani.
13Kwa hiyo mtu mwenye busara hunyamaza kimya
nyakati kama hizo,
kwa kuwa nyakati ni mbaya.
14Tafuteni mema, wala si mabaya,
ili mpate kuishi.
Ndipo BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote
atakuwa pamoja nanyi,
kama msemavyo yupo nanyi.
15Yachukieni maovu, yapendeni mema;
dumisheni haki mahakamani.
Yamkini BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote
atawahurumia mabaki ya Yosefu.16Kwa hiyo hili ndilo Bwana, BWANA Mungu Mwenye Nguvu Zote, asemalo: “Kutakuwepo maombolezo katika barabara zote
na vilio vya uchungu
mahali pa njia kuu.
Wakulima wataitwa kuja kulia
na waombolezaji waje kuomboleza.
17Kutakuwepo kuomboleza katika mashamba yote ya mizabibu,
kwa kuwa nitapita katikati yenu,”
asema BWANA.Siku Ya BWANA

18Ole wenu ninyi mnaoitamani
siku ya BWANA!
Kwa nini mnaitamani siku ya BWANA?
Siku hiyo itakuwa giza, si nuru.
19Itakuwa kama vile mtu aliyemkimbia simba
kumbe akakutana na dubu,
kama vile mtu aliyeingia nyumbani mwake
na kuupumzisha mkono wake kwenye ukuta
kumbe akaumwa na nyoka.
20Je, siku ya BWANA haitakuwa giza, na si nuru:
giza nene, bila mwonzi wa mwanga?
21“Ninachukia, ninazidharau sikukuu zenu za dini;
siwezi kuvumilia makusanyiko yenu.
22Hata ingawa mnaniletea sadaka zenu za kuteketezwa
na sadaka za nafaka,
sitazikubali.
Ingawa mnaniletea sadaka nzuri za amani,
sitazitambua.
23Niondoleeni kelele za nyimbo zenu!
Sitasikiliza sauti za vinubi vyenu.
24Lakini acheni haki itiririke kama mto,
na uadilifu uwe kama kijito kisichokauka!
25“Je, mliniletea dhabihu na sadaka
mlipokuwa jangwani miaka arobaini,
Ee nyumba ya Israeli?
26Mmeyainua madhabahu ya mfalme wenu:
Sikuthi mungu wenu mtawala,
Kiuni mungu wenu wa nyota;
ambao mliwatengeneza wenyewe.
27Kwa sababu hiyo nitawapelekeni
uhamishoni mbali kupita Dameski,”
asema BWANA, ambaye jina lake
ni Mungu Mwenye Nguvu Zote.
Copyright information for Neno