Amos 9

Israeli Kuangamizwa

1Nilimwona Bwana akiwa amesimama kando ya madhabahu, naye akasema: “Piga juu ya nguzo
ili vizingiti vitikisike.
Viangushe juu ya vichwa vya watu wote,
na wale watakaosalia nitawaua kwa upanga.
Hakuna awaye yote atakayekimbia,
hakuna atakayetoroka.
2Wajapojichimbia chini mpaka kwenye vina vya kuzimu,
kutoka huko mkono wangu utawatoa.
Wajapopanda juu hadi kwenye mbingu,
kutoka huko nitawashusha.
3Wajapojificha juu ya kilele cha Karmeli,
huko nitawawinda na kuwakamata.
Wajapojificha kutoka kwenye uso wangu
katika vilindi vya bahari,
huko nako nitaamuru joka kuwauma.
4Wajapopelekwa uhamishoni na adui zao,
huko nako nitaamuru upanga uwaue.
Nitawakazia macho yangu kwa mabaya
wala si kwa mazuri.”
5Bwana, BWANA Mwenye Nguvu Zote,
yeye agusaye dunia nayo ikayeyuka,
na wote wakaao ndani mwake wakaomboleza:
nayo nchi yote huinuka kama Nile,
kisha hushuka kama mto wa Misri;
6yeye ambaye hujenga jumba lake la kifalme katika mbingu
na kuisimika misingi yake juu ya dunia,
yeye aitaye maji ya bahari
na kuyamwaga juu ya uso wa nchi:
BWANA ndilo jina lake.
7“Je, Waisraeli,
ninyi si sawa kwangu kama Wakushi?”
asema BWANA.

“Je, sikuleta Israeli kutoka Misri,
Wafilisti toka Kaftori
9:7 Yaani Kirete

na Washami kutoka Kiri?
8“Hakika macho ya BWANA Mwenyezi
yako juu ya ufalme wenye dhambi.
Nami nitauangamiza
kutoka kwenye uso wa dunia:
hata hivyo sitaiangamiza kabisa
nyumba ya Yakobo,”
asema BWANA.

9“Kwa kuwa nitatoa amri,
na nitaipepeta nyumba ya Israeli
miongoni mwa mataifa yote
kama vile nafaka ipepetwavyo katika ungo,
na hakuna hata punje moja nzuri
itakayoanguka chini.
10Watenda dhambi wote miongoni mwa watu wangu
watauawa kwa upanga,
wale wote wasemao,
‘Maafa hayatatupata wala kutukuta.’


Kurejezwa Kwa Israeli

11Katika siku ile nitaisimamisha
hema ya Daudi iliyoanguka.
Nitakarabati mahali palipobomoka
na kujenga upya magofu yake,
na kujenga kama ilivyokuwa awali,
12ili wapate kumiliki mabaki ya Edomu
na mataifa yote yale yanayobeba Jina langu,”
asema BWANA ambaye atafanya mambo haya.

13

“Siku zinakuja,” asema BWANA, “wakati mvunaji atakapotanguliwa na mkulima
na mpanzi atakapotanguliwa
na yeye akamuaye zabibu.
Divai mpya itadondoka kutoka milimani
na kutiririka kutoka vilima vyote.
14Nitawarejesha tena watu wangu Israeli waliohamishwa;
wataijenga tena miji iliyoachwa magofu,
nao wataishi ndani mwake.
Watapanda mizabibu na kunywa divai yake,
watalima bustani na kula matunda yake.
15Nitaipanda Israeli katika nchi yao wenyewe,
hawatang'olewa tena
kutoka katika nchi ambayo nimewapa,”

asema BWANA Mungu wenu.


Copyright information for Neno