Colossians 3

Kanuni Za Kuishi Maisha Matakatifu

1Basi, kwa kuwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. 2Yafikirini mambo yaliyo juu, wala si ya duniani. 3Kwa maana ninyi mlikufa, nao uhai wenu sasa umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. 4Wakati Kristo atakapotokea yeye aliye uzima wenu ndipo nanyi mtakapotokea pamoja naye katika utukufu.

5Kwa hiyo, ueni kabisa cho chote kilicho ndani yenu cha asili ya kidunia: Yaani, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na kutamani, ambayo ndiyo ibada ya sanamu. 6Kwa sababu ya mambo haya, ghadhabu ya Mungu inakuja. 7Ninyi pia zamani mlienenda katika mambo haya mlipoishi maisha hayo. 8Lakini sasa yawekeni mbali nanyi mambo kama haya yote, yaani: Hasira, ghadhabu, uovu, masingizio na lugha chafu kutoka midomoni mwenu. 9Msiambiane uongo kwa maana mmevua kabisa utu wenu wa kale pamoja na matendo yake, 10nanyi mmevaa utu mpya unaofanywa upya katika ufahamu sawasawa na mfano wa Muumba wake. 11Hapa hakuna Myunani wala Myahudi, aliyetahiriwa wala asiyetahiriwa, asiyestaarabika wala aliyestaarabika, mtumwa wala mtu huru, bali Kristo ni yote na ndani ya wote.

12Kwa hiyo, kwa kuwa ninyi mmekuwa wateule wa Mungu, watakatifu, wapendwao sana, jivikeni moyo wa huruma, utu wema, unyenyekevu, upole na uvumilivu. 13Vumilianeni na kusameheana. Mtu akiwa na lalamiko lo lote dhidi ya mwenzake, sameheaneni kama vile Bwana alivyowasamehe ninyi. 14Zaidi ya maadili haya yote jivikeni upendo, ambao ndio unaofunga kila kitu pamoja katika umoja mkamilifu.

15Amani ya Kristo na itawale mioyoni mwenu, kwa kuwa ninyi kama viungo vya mwili mmoja mmeitiwa amani. Tena iweni watu wa shukrani. 16Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu, mkifundishana na kuonyana katika hekima yote, mkimwimbia Mungu zaburi, nyimbo na tenzi za rohoni huku mkiwa na shukrani mioyoni mwenu. 17Lo lote mfanyalo, ikiwa ni kwa neno au kwa tendo, fanyeni yote katika Jina la Bwana Yesu, mkimshukuru Mungu Baba katika yeye.

Kanuni Katika Madaraka Ya Nyumbani

18Ninyi wake, watiini waume zenu, kama inavyostahili katika Bwana.

19Ninyi waume, wapendeni wake zenu, wala msiwe na uchungu dhidi yao.

20Enyi watoto, watiini wazazi wenu katika mambo yote, kwa maana hivi ndivyo inavyompendeza Bwana.

21Ninyi akina baba msiwachokoze watoto wenu, wasije wakakata tamaa.

22Ninyi watumwa, watiini mabwana zenu wa hapa duniani katika mambo yote. Fanyeni hivyo si wakiwepo tu, bali mkimwogopa Mungu, wala si kwa kutafuta upendeleo wao wakati wanapowaona. 23Lo lote mfanyalo, fanyeni kwa moyo kama watu wanaomtumikia Bwana na si wanadamu. 24Kwa kuwa mnajua kwamba mtapokea urithi wenu kutoka kwa Bwana kuwa thawabu yenu. Ni Bwana Yesu Kristo mnayemtumikia. 25Ye yote atendaye mabaya atalipwa kwa ajili ya mabaya yake, wala hakuna upendeleo.

Copyright information for Neno