Daniel 11

1Nami katika mwaka wa kwanza wa kutawala kwake Dario, Mmedi, nilisimama kumsaidia na kumlinda.)

Wafalme Wa Kusini Na Wa Kaskazini

2“Sasa basi, ninakuambia kweli: Wafalme watatu zaidi watatokea Uajemi, kisha atatokea mfalme wa nne, ambaye atakuwa tajiri sana kuliko wengine wote. Wakati atakapokuwa amekwisha kujipatia nguvu kwa utajiri wake, atamchochea kila mmoja dhidi ya ufalme wa Uyunani. 3Ndipo mfalme mwenye nguvu atatokea, ambaye atatawala kwa nguvu nyingi na kufanya anavyopenda. 4Baada ya kujitokeza, milki yake itavunjwa na kugawanyika katika pande nne za mbinguni. Hautakwenda kwa wazao wake, wala hautakuwa na nguvu alizoonyesha, kwa sababu milki yake itang'olewa na kupewa wengine.

5“Mfalme wa Kusini atakuwa na nguvu, lakini mmoja wa majemadari wake atakuwa na nguvu zaidi kuliko mfalme, naye atatawala ufalme wake mwenyewe kwa nguvu nyingi. 6Baada ya miaka kadha wa kadha, wataungana. Binti wa mfalme wa Kusini ataolewa kwa mfalme wa Kaskazini ili kuimarisha mapatano, lakini huyo binti nguvu zake za ushawishi hazitadumu, vivyo hivyo na baba yake. Katika siku hizo atafukuzwa, pamoja na hao wasindikizaji wake wa kifalme, watoto wake na ye yote aliyemuunga mkono.

7“Mmoja kutoka jamaa ya huyo binti atainuka na kuchukua nafasi yake. Huyo mtu atashambulia majeshi ya mfalme wa Kaskazini na kuingia katika ngome yake, atapigana dhidi yao naye atashinda. 8Naye ataitwaa miungu yao, vinyago vyao vya chuma na vitu vyao vya thamani vya fedha na dhahabu na kuvichukua hadi Misri kama nyara za vita. Kwa miaka kadha wa kadha atamwacha mfalme wa Kaskazini bila kumsumbua. 9Kisha mfalme wa Kaskazini atashambulia kwa vita mfalme wa Kusini lakini atarudi nyuma hadi kwenye nchi yake mwenyewe. 10Hata hivyo, wana wa mfalme wa Kaskazini watajiandaa kwa vita na kukusanya jeshi kubwa, ambalo litafagia nchi kama mafuriko yasiyozuilika na kuendelea na vita hadi kwenye ngome ya mfalme wa Kusini.

11“Kisha mfalme wa Kusini atatoka kwa ghadhabu na kupigana dhidi ya mfalme wa Kaskazini, ambaye ataunda jeshi kubwa, lakini litashindwa. 12Wakati jeshi litakapokuwa limechukuliwa, mfalme wa Kusini atajawa na majivuno na atachinja maelfu mengi, hata hivyo hatabaki na ushindi. 13Kwa maana mfalme wa Kaskazini atakusanya jeshi jingine, kubwa kuliko lile la kwanza, na baada ya miaka kadha wa kadha, atasonga mbele na jeshi kubwa mno lililoandaliwa vizuri.

14“Katika nyakati hizo wengi watainuka dhidi ya mfalme wa Kusini. Watu wenye ghasia miongoni mwa watu wako mwenyewe wataasi ili kutimiza maono, lakini bila mafanikio. 15Ndipo mfalme wa Kaskazini atakuja na kuuzunguka mji kwa majeshi na kuuteka mji uliozungushiwa boma. Majeshi ya Kusini yatakosa nguvu ya kuyazuia, naam, hata vikosi vyao vya askari vilivyo bora kuliko vingine, havitakuwa na nguvu ya kuwakabili. 16Huyo avamiaye nchi kwa vita atafanya apendavyo, hakuna ye yote atakayeweza kusimama mbele yake. Atajiimarisha mwenyewe katika Nchi ya Kupendeza na atakuwa na uwezo wa kuiangamiza. 17Naye atafanya mipango kuja na nguvu za ufalme wake wote na kufanya mapatano ya amani na mfalme wa Kusini. Naye atamtoa binti yake aolewe naye ili kufanya mipango ya kuuangusha ufalme ndani kwa ndani, lakini mipango haitafanikiwa wala kumsaidia. 18Ndipo atabadili mwelekeo wake kuelekea nchi za pwani na ataziteka nyingi, lakini jemadari kutoka mahali pengine atakomesha ufidhuli wake na kurudisha ufidhuli wake juu yake. 19Baada ya hili atazigeukia ngome za nchi yake mwenyewe lakini atajikwaa na kuanguka, wala hataonekana tena.

20“Atakayetawala baada yake atamtuma mtoza ushuru ili kudumisha fahari ya kifalme. Hata hivyo, kwa miaka michache ataangamizwa, lakini si katika hasira wala katika vita.

21“Atakayetawala baada yake atakuwa mtu wa kudharauliwa ambaye hajapewa heshima ya kifalme. Atauvamia ufalme wakati watu wake wanapojiona wako salama, naye atautwaa kwa hila. 22Ndipo jeshi kubwa litafagiliwa mbele yake, jeshi pamoja na mkuu wa agano wataangamizwa. 23Baada ya kufanya mapatano naye, atatenda kwa udanganyifu, pamoja na watu wachache tu ataingia madarakani. 24Wakati majimbo yaliyo tajiri sana yanapojiona salama, atayavamia naye atafanikisha kile ambacho baba zake wala babu zake hawakufanya. Atagawa nyara, mateka na utajiri miongoni mwa wafuasi wake. Atafanya hila ya kupindua miji yenye maboma, lakini kwa muda mfupi tu.

25“Pamoja na jeshi kubwa atachochea nguvu zake na ushujaa wake dhidi ya mfalme wa Kusini. Mfalme wa Kusini atafanya vita na jeshi lenye nguvu sana, lakini hataweza kusimama kwa sababu ya mashauri yaliyofanywa kwa hila dhidi yake. 26Wale wanaokula kutoka kwenye ruzuku za mfalme watajaribu kumwangamiza, jeshi lake litafagiliwa mbali, nao wengi watakufa vitani. 27Wafalme hawa wawili, mioyo yao ikiwa imekusudia mabaya wataketi kwenye meza moja na kudanganyana wao kwa wao, lakini pasipo faida, kwa sababu bado mwisho utakuja katika wakati ulioamuriwa. 28Mfalme wa Kaskazini atarudi katika nchi yake na utajiri mwingi, lakini atakuwa ameukaza moyo wake kinyume na Agano takatifu. Atachukua hatua dhidi ya hilo agano na kisha atarudi katika nchi yake.

29“Katika wakati ulioamuriwa atavamia tena Kusini, lakini wakati huu matokeo yake yatakuwa tofauti na yale ya wakati wa kwanza. 30Meli za nchi ya Kitimu zitampinga, naye atavunjika moyo. Ndipo atageuka nyuma na kutoa wazi hasira yake dhidi ya Agano takatifu. Atarudi na kuonyesha fadhili kwa wale waliachao Agano takatifu.

31“Majeshi yake yenye silaha yatainuka ili kunajisi ngome ya Hekalu na kuondolea mbali sadaka ya kuteketezwa ya kila siku. Ndipo watalisimamisha chukizo la uharibifu lisababishalo ukiwa. 32Kwa udanganyifu atapotosha wale walionajisi Agano, lakini watu wanaomjua Mungu wao watampinga kwa uthabiti.

33“Wale wenye hekima watawafundisha wengi, ingawa kwa kitambo watauawa kwa upanga au kuchomwa moto, au kukamatwa na kufanywa mateka. 34Watakapoanguka, watapokea msaada kidogo, nao wengi ambao si waaminifu wataungana nao. 35Baadhi ya wenye hekima watajikwaa, ili kwamba waweze kusafishwa, kutakaswa na kufanywa wasio na waa mpaka wakati wa mwisho, kwa maana bado litakuja kwa wakati ulioamuriwa.

Mfalme Ajikwezaye Mwenyewe

36“Mfalme atafanya apendavyo. Atajikweza na kujitukuza mwenyewe kujihesabu mwenye nguvu zaidi juu ya kila mungu naye atasema vitu ambavyo havijasikiwa dhidi ya Mungu wa miungu. Atafanikiwa hadi wakati wa ghadhabu utimie, kwa maana kile kilichokusudiwa lazima kitokee. 37Hataonyesha heshima kwa miungu ya baba zake au kwa yule aliyetamaniwa na wanawake, wala hatajali mungu ye yote, bali atajikweza mwenyewe juu yao wote. 38Badala ya kuwajali hao miungu, ataheshimu mungu wa ngome, mungu ambaye hakujulikana na baba zake, atamheshimu kwa dhahabu na fedha, kwa vito vya thamani na zawadi za thamani kubwa. 39Atashambulia ngome zenye nguvu mno kwa msaada wa mungu wa kigeni naye atawaheshimu sana wale watakaomkubali yeye. Atawafanya watawala juu ya watu wengi na atagawa nchi kwa kulipia.

40“Katika wakati wa mwisho mfalme wa Kusini atapigana naye vita, naye mfalme wa Kaskazini atamshambulia kwa magari ya vita na askari wapanda farasi na idadi kubwa ya meli. Atavamia nchi nyingi na kukumba nchi hizo kama mafuriko. 41Pia ataivamia Nchi ya Kupendeza. Nchi nyingi zitapinduliwa, bali Edomu, Moabu na viongozi wa Amoni wataokolewa kutoka katika mkono wake. 42Atapanua mamlaka yake juu ya nchi nyingi, Misri haitaepuka. 43Atamiliki hazina za dhahabu, fedha na utajiri wote wa Misri, pamoja na Walibya na Wakushi kwa kujisalimisha. 44Lakini taarifa kutoka mashariki na kaskazini zitamshtua, naye ataondoka kwa ghadhabu nyingi ili kuangamiza na kuharibu kabisa wengi. 45Atasimika mahema yake ya kifalme kati ya bahari na mlima mtakatifu wa kupendeza. Hata hivyo, atafikia mwisho wake, wala hakuna ye yote atakayemsaidia.

Copyright information for Neno