Daniel 4

Ndoto Ya Nebukadneza Ya Mti

Mfalme Nebukadneza,Kwa kabila za watu, mataifa na watu wa kila lugha, wanaoishi katika ulimwengu wote:Amani na mafanikio yawe kwenu!Ni furaha yangu kuwaambia kuhusu ishara ya miujiza na maajabu ambayo Mungu Aliye Juu Sana amenifanyia.

Tazama jinsi ishara zake zilivyo kuu,
jinsi maajabu yake
yalivyo na nguvu!
Ufalme wake ni ufalme wa milele;
enzi yake hudumu
kutoka kizazi hadi kizazi.Mimi, Nebukadneza, nilikuwa nyumbani katika jumba langu la kifalme, nikiwa ninaishi kwa raha na hali yakufanikiwa. Niliota ndoto iliyoniogopesha. Nilipokuwa nimelala kitandani mwangu, njozi na maono yaliyopita akilini mwangu vilinitisha. Hivyo nikaagiza kwamba watu wote wenye hekima wa Babeli waletwe mbele yangu kunifasiria ndoto yangu. Walipokuja waganga, wasihiri, wanajimu na waaguzi, niliwaambia ndoto yangu, lakini hawakuweza kunifasiria. Mwishoni, Danieli alikuja mbele yangu nikamweleza hiyo ndoto. (Danieli anaitwa Belteshaza, kwa jina la mungu wangu, nayo roho ya miungu mitakatifu inakaa ndani yake.)

Nilisema, “Belteshaza, mkuu wa waganga, ninajua kuwa Roho ya Miungu Mitakatifu iko ndani yako, wala hakuna siri iliyo ngumu kwako. Hii ndiyo ndoto yangu, nifasirie. 10 Haya ndiyo maono niliyoona nilipokuwa nimelala kitandani mwangu: Nilitazama, na mbele yangu ulisimama mti katikati ya nchi. Ulikuwa mrefu sana. 11 Mti ule ulikua ukawa mkubwa na wenye nguvu, nayo ncha yake ikagusa anga, ulionekana mpaka miisho ya dunia. 12 Majani yake yalikuwa ya kupendeza, matunda yake yalikuwa mengi, juu yake kulikuwa na chakula kwa ajili ya wote. Chini ya kivuli chake wanyama wa kondeni walipata hifadhi na ndege wa angani waliishi katika matawi yake. Kila kiumbe kililishwa kutokana na mti huo.

13 “Katika maono niliyoyaona nikiwa nimelala kitandani mwangu, nilitazama, mbele yangu alikuwepo mlinzi, aliye mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni. 14 Akaita kwa sauti kubwa: ‘Kateni mti huu, yafyekeni matawi yake, yaondoeni majani na kuyatawanya matunda yake. Wanyama na wakimbie kutoka chini yake na ndege wakimbie kutoka katika matawi yake. 15 Lakini acheni kisiki chake na mizizi, kikiwa kimefungwa kwa chuma na shaba, kibaki ardhini, kwenye majani ya kondeni.

“ ‘Mwacheni aloweshwe na umande wa mbinguni, naye aachwe aishi pamoja na wanyama miongoni mwa mimea ya dunia.
16 Akili yake na ibadilishwe kutoka ile ya mwanadamu na apewe akili ya mnyama, mpaka nyakati saba zipite juu yake.

17 “ ‘Uamuzi huu umetangazwa na walinzi, hukumu hii imetangazwa na watakatifu, ili walio hai wajue kuwa Aliye Juu Sana ndiye anayetawala juu ya falme zote za wanadamu, naye humpa ye yote amtakaye na kumtawaza juu yake hata yeye aliye mnyonge sana miongoni mwa wanadamu.’

18 “Hii ndiyo niliyopata mimi, Mfalme Nebukadneza. Sasa Belteshaza, niambie maana yake, kwa maana hakuna hata mmoja wa wenye hekima katika ufalme wangu anayeweza kunifasiria. Bali wewe waweza, kwa sababu Roho ya Miungu Mitakatifu imo ndani yako.”

Danieli Anafasiri Ndoto

19 Ndipo Danieli (aliyeitwa pia Belteshaza) alipofadhaika sana kwa kitambo, nayo mawazo yake yakamtia hofu. Basi mfalme akasema, “Belteshaza, usiruhusu ndoto wala maana yake kukutia hofu.”

Belteshaza akamjibu, “Bwana wangu, laiti ndoto hii ingehusu adui zako na maana yake iwahusu watesi wako!
20 Mti uliouona, uliokua ukawa mkubwa na wenye nguvu, nayo ncha yake ikigusa anga na kuonekana duniani kote, 21 ukiwa na majani yakupendeza na matunda mengi, ukitoa chakula kwa wote, ukiwapa hifadhi wanyama wa kondeni na kuwa mahali pa viota katika matawi yake kwa ajili ya ndege wa angani, 22 Ee mfalme, wewe ndiwe ule mti! Umekuwa mkubwa na mwenye nguvu, ukuu wako umekua mpaka kufika juu angani, nayo mamlaka yako yameenea mpaka miisho ya dunia.

23 “Ee mfalme, wewe ulimwona mlinzi, aliye mtakatifu, akishuka kutoka mbinguni na kusema, ‘Ukateni mti na kuuangamiza, lakini kiacheni kisiki kikiwa kimefungwa kwa chuma na kwa shaba, kwenye majani ya kondeni, wakati mizizi yake inabaki ardhini. Mwacheni aloweshwe na umande wa mbinguni, mwacheni aishi kama wanyama-pori mpaka nyakati saba zipite juu yake.’

24 “Ee mfalme, hii ndiyo tafsiri, hii ni amri ya Aliye Juu Sana aliyoitoa dhidi ya bwana wangu mfalme: 25 Wewe utafukuzwa mbali na wanadamu, nawe utaishi pamoja na wanyama pori, utakula manyasi kama ng'ombe na kuloana kwa umande wa mbinguni. Nyakati saba zitapita juu yako, mpaka utakapokubali kuwa Yeye Aliye Juu Sana ndiye anayetawala juu ya falme za wanadamu, naye humtawaza ye yote amtakaye. 26 Amri ya kuacha kisiki pamoja na mizizi yake inamaanisha kwamba ufalme wako utarejezwa kwako utakapokubali kwamba Mbingu ndizo zitawalazo. 27 Kwa hiyo, Ee mfalme, uwe radhi kupokea shauri langu: Acha dhambi zako kwa kutenda yaliyo haki, ukaache uovu wako uwe na huruma kwa walioonewa. Hivyo itawezekana baada ya hayo mafanikio yako yakaendelea.”

Ndoto Inatimia

28 Haya yote yalimpata Mfalme Nebukadneza. 29 Miezi kumi na miwili baadaye, mfalme alipokuwa akitembea juu ya paa la jumba la kifalme la Babeli, 30 alisema, “Je, huu si Babeli mji mkuu nilioujenga kama makao ya kifalme, kwa uwezo wangu mkubwa na kwa ajili ya utukufu wa enzi yangu?”

31 Maneno hayo yalikuwa bado katika midomo yake wakati sauti ilipokuja kutoka mbinguni, ikisema, “Mfalme Nebukadneza, hiki ndicho kilichoamriwa kwa ajili yako: Mamlaka yako ya kifalme yameondolewa kutoka kwako. 32 Utafukuzwa mbali na wanadamu ukaishi pamoja na wanyama pori, utakula manyasi kama ng'ombe. Nyakati saba zitapita juu yako, mpaka utakapokubali kuwa Yeye Aliye Juu Sana ndiye anayetawala juu ya falme za wanadamu, naye humtawaza ye yote amtakaye.”

33 Papo hapo yale yaliyokuwa yamesemwa kuhusu Nebukadneza yakatimia. Alifukuzwa mbali na wanadamu, akala majani kama ng'ombe. Mwili wake uliloweshwa kwa umande wa mbinguni mpaka nywele zake zikakua kama manyoya ya tai na kucha zake kama makucha ya ndege.34 Mwisho wa huo wakati, mimi Nebukadneza, niliinua macho yangu kuelekea mbinguni, nazo fahamu zangu zikanirudia. Ndipo nikamsifu Yeye Aliye Juu Sana, nikamheshimu na kumhimidi yeye aishiye milele.

Utawala wake ni utawala wa milele;
ufalme wake hudumu
kutoka kizazi na kizazi.
35 Mataifa yote ya dunia
yanahesabiwa kuwa si kitu.
Hufanya kama atakavyo
kwa majeshi ya mbinguni
na kwa mataifa ya dunia.
Hakuna anayeweza kuuzuia mkono wake
au kumwambia,
“Umefanya nini wewe?”36 Wakati huo huo fahamu zangu ziliponirudia, heshima yangu na fahari yangu nikarudishiwa kwa ajili ya utukufu wa ufalme wangu. Washauri wangu na wakuu wangu walikuja kunitafuta, nami nikarudishwa kwenye kiti changu cha ufalme hata nikawa mkuu kuliko mwanzoni. 37 Basi mimi, Nebukadneza, humhimidi, humtukuza na kumsifu Mfalme wa mbinguni, kwa sababu kila kitu afanyacho ni haki na njia zake zote ni adili. Nao waendao kwa kiburi anaweza kuwashusha.

Copyright information for Neno