Daniel 5

Maandishi Ukutani

Mfalme Belshaza alifanya karamu kubwa kwa ajili ya maelfu ya wakuu wake na akanywa mvinyo pamoja nao. Wakati Belshaza alipokuwa akinywa mvinyo wake, aliamuru viletwe vile vikombe vya dhahabu na fedha ambavyo Nebukadneza baba yake alikuwa amevichukua kutoka hekaluni huko Yerusalemu, ili mfalme na wakuu wake, wake zake na masuria wake waweze kuvinywea. Kwa hiyo wakavileta vile vikombe vya dhahabu ambavyo vilikuwa vimechukuliwa kutoka katika Hekalu la Mungu huko Yerusalemu, naye mfalme na wakuu wake, wake zake na masuria wake wakavinywea. Walipokuwa wakinywa mvinyo, wakaisifu miungu ya dhahabu, ya fedha, ya shaba, ya chuma, ya miti na ya mawe.

Ghafula vidole vya kitanga cha mwanadamu vilitokea na kuandika juu ya ukuta, karibu na kinara cha taa ndani ya jumba la mfalme. Mfalme akatazama kitanga kilivyokuwa kikiandika. Uso wa mfalme ukageuka rangi naye aliogopa sana kiasi kwamba magoti yake yaligongana na miguu yake ikalegea.

Mfalme akawaita wasihiri, wanajimu na waganga waletwe, naye akawaambia hawa wenye hekima wa Babeli, “Ye yote asomaye maandishi haya na kuniambia maana yake, atavikwa nguo za zambarau na kuvikwa mkufu wa dhahabu shingoni mwake, naye atafanywa mtawala wa tatu kutoka juu katika ufalme.”

Ndipo watu wote wa mfalme wenye hekima wakaingia, lakini hawakuweza kusoma yale maandishi wala kumwambia mfalme maana yake. Basi Mfalme Belshaza akazidi kujawa na hofu na uso wake ukageuka rangi zaidi. Wakuu wake wakapigwa na bumbuazi.

10 Malkia
5.10 Au: Mama yake mfalme
aliposikia sauti za mfalme na wakuu wake alikuja akaingia katika ukumbi wa karamu. Akasema, “Ee mfalme, uishi milele. Usishtuke! Usibadilike rangi kiasi hicho!
11 Yuko mtu katika ufalme wako ambaye ana Roho ya Miungu Mitakatifu ndani yake. Wakati wa baba yako, mtu huyo alionekana kuwa na ufahamu, akili na hekima kama ile ya miungu. Mfalme Nebukadneza baba yako, yaani nasema mfalme baba yako, alimtuma kuwa mkuu wa waganga, wasihiri, wanajimu na waaguzi. 12 Mtu huyu Danieli, ambaye mfalme alimwita Belteshaza, alionekana kuwa na akili nyepesi, maarifa na ufahamu, pia uwezo wa kufasiri ndoto, kueleza mafumbo na kutatua matatizo magumu. Mwite Danieli, naye atakuambia maana ya haya maandishi.”

13 Hivyo Danieli akaletwa mbele ya mfalme, naye mfalme akamwuliza, “Je, wewe ndiwe Danieli, mmoja wa watu wa uhamisho walioletwa na mfalme baba yangu kutoka Uyahudi? 14 Nimesikia kwamba Roho ya Miungu iko ndani yako na kwamba una ufahamu, akili na hekima ya pekee. 15 Watu wenye hekima na wasihiri waliletwa mbele yangu ili kusoma maandishi haya na kuniambia maana yake, lakini hawakuweza kunifafanulia. 16 Basi nimesikia kwamba unaweza kutoa tafsiri na kutatua matatizo magumu. Ikiwa unaweza kusoma maandishi haya na kuniambia maana yake, utavikwa nguo za zambarau na mkufu wa dhahabu shingoni mwako, nawe utafanywa mtawala wa tatu kutoka juu katika ufalme.”

17 Ndipo Danieli akamjibu mfalme, “Waweza kubaki na zawadi zako mwenyewe na kumpa mtu mwingine ye yote zawadi zako. Hata hivyo, nitasoma maandishi kwa ajili ya mfalme na kumwambia maana yake.

18 “Ee mfalme, Mungu Aliye Juu Sana alimpa baba yako Nebukadneza utawala, ukuu, utukufu na fahari. 19 Kwa sababu ya nafasi ya juu aliyompa baba yako, kabila zote za watu, mataifa na watu wa kila lugha walimhofu na kumwogopa. Wale ambao mfalme alitaka kuwaua, aliwaua, wale aliotaka kuwaacha hai, aliwaacha hai, wale aliotaka kuwapandisha cheo, aliwapandisha, aliotaka kuwashusha, aliwashusha. 20 Lakini moyo wake ulipokuwa na majivuno na kuwa mgumu kwa kiburi, aliondolewa kutoka kwenye kiti chake cha utawala cha kifalme na kuvuliwa utukufu wake. 21 Akafukuzwa mbali na wanadamu na kupewa akili ya mnyama, akaishi pamoja na punda-mwitu, akala majani kama ng'ombe, nao mwili wake ukaloweshwa kwa umande wa mbingu, mpaka alipotambua kwamba Mungu Aliye Juu Sana ndiye mtawala juu ya falme za wanadamu na kwamba humtawaza juu yao ye yote amtakaye.

22 “Lakini wewe mwanawe, Ee Belshaza, hukujinyenyekeza, ingawa ulifahamu haya yote. 23 Badala yake, umejiinua dhidi ya Bwana wa mbingu. Uliletewa vikombe vya Hekalu lake, nawe na wakuu wako, wake zako na masuria wako mlivitumia kwa kunywea mvinyo. Ukaisifu miungu ya fedha, ya dhahabu, ya shaba, ya chuma, ya miti na ya mawe, miungu ambayo haiwezi kuona au kusikia wala kufahamu. Lakini hukumheshimu Mungu ambaye anaushikilia uhai wako na njia zako zote mkononi mwake. 24 Kwa hiyo ameutuma mkono ule ulioandika maneno.

25 “Haya ndiyo maneno yaliyoandikwa:
MENE, MENE, TEKELI NA PERESI


26 “Hii ndiyo maana ya maneno haya:
  • Mene: Mungu amezihesabu siku za utawala wako na kuukomesha.
27  Tekeli : Wewe umepimwa katika mizani na umeonekana umepungua. 28  Peresi : Ufalme wako umegawanywa na kupewa Wamedi na Waajemi.” 29 Ndipo kwa amri ya Belshaza, Danieli akavikwa nguo za zambarau na mkufu wa dhahabu shingoni, tena akatangazwa kuwa mtawala wa tatu kutoka juu katika ufalme.

30 Usiku ule ule Belshaza, mfalme wa Babeli akauawa, 31 naye Dario Mmedi akashika ufalme akiwa na miaka sitini na miwili.

Copyright information for Neno