Daniel 6

Danieli Katika Tundu La Simba

1Ilimpendeza Dario kuteua wakuu 120 kutawala katika ufalme wake wote, 2pamoja na wasimamizi watatu juu yao, ambao mmoja wao alikuwa Danieli. Wakuu walitoa hesabu kwa hao wasimamizi ili mfalme asipate hasara. 3Basi Danieli alijidhihirisha mwenyewe, miongoni mwa wasimamizi na wakuu kwa sifa zake za kipekee hata mfalme akapanga kumweka juu ya ufalme wote. 4Kwa hili, wakuu na wasimamizi wakajaribu kutafuta sababu za kumshitaki Danieli kuhusu usimamizi wake wa shughuli za serikali, lakini hawakuweza kufanikiwa. Hawakuweza kupata kosa kwake, kwa sababu alikuwa mwaminifu na wala hakupatikana na upotovu wala uzembe. 5Mwishoni watu hawa walisema, “Kamwe hatutapata msingi kwa ajili ya mashtaka dhidi ya mtu huyu Danieli isipokuwa kile kinachohusiana na sheria ya Mungu wake.”

6Basi wasimamizi na wakuu wakaingia kwa mfalme kama kikundi wakasema, “Ee Mfalme Dario, uishi milele! 7Wasimamizi wa kifalme, wasaidizi, wakuu, washauri na watawala wote wamekubaliana kwamba mfalme atoe sheria na kukazia amri kuwa ye yote atakayemwomba Mungu ye yote au mwanadamu katika muda huu wa siku thelathini zijazo, isipokuwa kwako wewe, Ee mfalme, atatupwa ndani ya tundu la simba. 8Sasa, Ee mfalme, toa amri na uiandike ili kwamba isiweze kubadilishwa, kwa kulingana na sheria za Wamedi na Waajemi, ambazo haziwezi kubatilishwa.” 9Hivyo Mfalme Dario akaiweka amri hiyo katika maandishi.

10Ikawa Danieli alipofahamu kuwa amri ile imetangazwa, alikwenda nyumbani kwenye chumba chake cha ghorofani ambako madirisha yalifunguka kuelekea Yerusalemu. Mara tatu kwa siku akapiga magoti na kuomba, akimshukuru Mungu wake, kama alivyokuwa akifanya mwanzoni. 11Ndipo watu hawa wakamwendea kama kikundi na kumkuta Danieli anaomba na kumsihi Mungu kwa ajili ya msaada. 12Basi wakaenda kwa mfalme na kusema naye kuhusu amri ya kifalme: “Je, hukutangaza amri kwamba kwa muda huu wa siku thelathini zijazo mtu ye yote ambaye atamwomba mungu au mwanadamu ye yote isipokuwa wewe, Ee mfalme, angetupwa ndani ya tundu la simba?”

Mfalme akajibu, “Amri ndivyo ilivyo, kulingana na sheria za Wamedi na Waajemi, ambazo haziwezi kutanguka.”

13Ndipo wakamwambia mfalme, “Danieli, ambaye ni mmoja wa watu wa uhamisho kutoka Yuda hakuheshimu, Ee mfalme, wala hajali amri uliyoiweka kwa maandishi. Angalia anaomba mara tatu kwa siku.” 14Wakati mfalme aliposikia hili, akahuzunishwa mno, akakusudia kumwokoa Danieli, naye akafanya kila jitihada ya kumwokoa hadi jua likatua.

15Ndipo wale watu wakamwendea mfalme kama kikundi na kumwambia, “Ee mfalme, kumbuka kwamba kulingana na sheria ya Wamedi na Waajemi hakuna amri wala sheria ambayo mfalme ameitoa inayoweza kubadilishwa.”

16Basi mfalme akatoa amri, nao wakamleta

Danieli wakamtupa ndani ya tundu la simba. Mfalme akamwambia Danieli, “Mungu wako unayemtumikia daima na akuokoe!”

17Jiwe likaletwa na kuwekwa kwenye mdomo wa tundu, naye mfalme akalitia muhuri kwa pete yake mwenyewe pamoja na kwa pete za wakuu wake, ili kwamba hali ya Danieli isiweze kubadilishwa. 18Kisha mfalme akarudi kwenye jumba lake la kifalme na usiku kucha hakula chakula wala kutumia viburudisho alivyoletewa. Wala hakuweza kulala.

19Mapema alfajiri mfalme akaondoka na kuharakisha kwenda kwenye tundu la simba. 20Wakati alipokaribia lile tundu, alimwita Danieli kwa sauti ya uchungu, “Danieli, mtumishi wa Mungu aliye hai, je, Mungu wako unayemtumikia daima, ameweza kukuokoa na simba hawa?”

21Danieli akajibu, “Ee mfalme, uishi milele! 22Mungu wangu alimtuma malaika wake, naye akafunga vinywa vya hawa simba. Hawajanidhuru, kwa sababu nilionekana sina hatia mbele zake. Wala kamwe sijafanya jambo lo lote baya mbele yako, Ee mfalme.”

23Mfalme akafurahi mno naye akatoa amri Danieli atolewe kwenye lile tundu. Danieli alipotolewa katika lile tundu, hakukutwa na jeraha lo lote, kwa sababu alikuwa amemtumaini Mungu wake.

24Kwa amri ya mfalme wale watu waliokuwa wamemshtaki Danieli kwa uongo waliletwa na kutupwa ndani ya lile tundu la simba, pamoja na wake zao na watoto wao. Nao kabla hawajafika chini kwenye sakafu ya lile tundu, simba wakawakamata na kusaga mifupa yao yote.

25Kisha Mfalme Dario akawaandikia kabila zote za watu, mataifa na watu wa kila lugha katika nchi yote:“Ninyi na mstawi sana!26“Natoa amri hii kwamba katika kila sehemu ya ufalme wangu lazima watu wamwogope na kumheshimu Mungu wa Danieli. “Kwa maana yeye ni Mungu aliye hai
naye hudumu milele,
ufalme wake hautaangamizwa,
nao utawala wake
kamwe hauna mwisho.
27Huponya na kuokoa:
hufanya ishara na maajabu
mbinguni na duniani.
Amemponya Danieli
kutoka katika nguvu za simba.”28Hivyo Danieli akastawi wakati wa utawala wa Dario na utawala wa Koreshi, Mwajemi.

Copyright information for Neno