Daniel 7

Ndoto Ya Danieli Ya Wanyama Wanne

Katika mwaka wa kwanza wa kutawala kwake Belshaza mfalme wa Babeli, Danieli aliota ndoto, nayo maono yakapita katika akili yake alipokuwa amelala kitandani mwake. Akayaandika mambo aliyoyaona katika ndoto yake.

Danieli akasema: “Katika maono yangu usiku nilitazama, mbele yangu kulikuwepo na upepo kutoka pande nne za mbinguni zikivuruga bahari kuu. Wanyama wakubwa wanne, kila mmoja tofauti na mwenzake, wakajitokeza kutoka baharini.

“Mnyama wa kwanza alifanana na simba, naye alikuwa na mabawa kama ya tai. Nikatazama mpaka mabawa yake yalipong'olewa naye akainuliwa katika nchi akasimama kwa miguu miwili kama mwanadamu, naye akapewa moyo wa binadamu.

“Hapo mbele yangu kulikuwa na mnyama wa pili, ambaye alionekana kama dubu. Upande wake mmoja ulikuwa umeinuka, alikuwa na mbavu tatu katika kinywa chake kati ya meno yake. Akaambiwa, ‘Amka, ule nyama mpaka ushibe!’

“Baada ya huyo, nilitazama, mbele yangu kulikuwa na mnyama mwingine, aliyefanana na chui. Juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne kama yale ya ndege. Mnyama huyu alikuwa na vichwa vinne, naye akapewa mamlaka ya kutawala.

“Baada ya huyo, katika maono yangu usiku nilitazama, mbele yangu kulikuwa na mnyama wa nne, mwenye kutisha na kuogofya tena mwenye nguvu nyingi. Alikuwa na meno makubwa ya chuma, akapondaponda na kuangamiza wahanga wake na kukanyaga chini ya nyayo zake cho chote kilichosalia. Alikuwa tofauti na wanyama wote waliotangulia, naye alikuwa na pembe kumi.

“Wakati nilipokuwa ninafikiri kuhusu pembe hizo, mbele yangu kulikuwa na pembe nyingine, ambayo ni ndogo, ikajitokeza miongoni mwa zile kumi, pembe tatu za mwanzoni ziling'olewa ili kuipa nafasi hiyo ndogo. Pembe hii ilikuwa na macho kama ya mwanadamu na mdomo ulionena kwa majivuno.

“Nilipokuwa ninaendelea kutazama, “viti vya enzi vikawekwa,
naye Mzee wa Siku akaketi.
Mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji,
nywele za kichwa chake
zilikuwa nyeupe kama sufu.
Kiti chake cha enzi kilikuwa kinawaka kwa miali ya moto,
nayo magurudumu yake yote
yalikuwa yanawaka moto.
10 Mto wa moto ulikuwa unatiririka,
ukipita mbele yake.
Maelfu elfu wakamhudumia,
kumi elfu mara kumi elfu
wakasimama mbele zake.
Mahakama ikakaa ili kuhukumu
na vitabu vikafunguliwa.11 “Kisha nikaendelea kutazama kwa sababu ya yale maneno ya majivuno yaliyosemwa na ile pembe. Nikaendelea kuangalia mpaka yule mnyama alipochinjwa na mwili wake ukaharibiwa na kutupwa katika ule moto unaowaka. 12 (Wanyama wengine walikuwa wamevuliwa mamlaka yao, lakini waliruhusiwa kuishi kwa muda fulani.)

13 “Katika maono yangu ya usiku nilitazama, mbele yangu nikamwona anayefanana na mwanadamu, akija pamoja na mawingu ya mbinguni. Akamkaribia huyo Mzee wa Siku na akaongozwa mbele zake. 14 Akapewa mamlaka, utukufu na ufalme wenye nguvu, watu, kabila zote za mataifa na watu wa kila lugha wakamwabudu. Utawala wake ni utawala wa milele ambao hautapita, nao ufalme wake ni ule ambao kamwe hautaangamizwa.

Tafsiri Ya Ndoto

15 “Mimi, Danieli, nilipata mahangaiko rohoni, nayo maono yale yaliyopita ndani ya akili zangu yalinisumbua. 16 Nikamkaribia mmoja wa wale waliosimama pale na kumwuliza maana halisi ya haya yote.

“Basi akaniambia na kunipa tafsiri ya vitu hivi:
17 ‘Hao wanyama wakubwa wanne ni falme nne zitakazoinuka duniani. 18 Lakini watakatifu wa Yeye Aliye Juu Sana watapokea ufalme na kuumiliki milele, naam, milele na milele.’

19 “Kisha nilitaka kufahamu maana ya kweli ya mnyama yule wa nne, ambaye alikuwa tofauti na wale wengine wote tena wa kutisha mwenye meno ya chuma na makucha ya shaba, mnyama ambaye alipondaponda na kuangamiza wahanga wake na kukanyaga cho chote kilichosalia. 20 Pia mimi nilitaka kujua kuhusu zile pembe kumi juu ya kichwa chake na pia kuhusu ile pembe nyingine iliyojitokeza, ambayo mbele yake zile tatu za mwanzoni zilianguka, ile pembe ambayo ilionekana kuvutia macho zaidi kuliko zile nyingine na ambayo ilikuwa na macho na kinywa kilichonena kwa majivuno. 21 Nilipoendelea kutazama, pembe hii ilikuwa inapigana vita dhidi ya watakatifu na kuwashinda, 22 mpaka huyo Mzee wa Siku alipokuja na kutamka hukumu kwa kuwapa ushindi watakatifu wa Yeye Aliye Juu Sana, na wakati ukawadia walipomiliki ufalme.

23 “Alinipa maelezo haya: ‘Mnyama wa nne ni ufalme wa nne ambao utatokea duniani. Utakuwa tofauti na falme nyingine zote nao utaharibu dunia nzima, ukiikanyaga chini na kuipondaponda. 24 Zile pembe kumi ni wafalme kumi watakaotokana na ufalme huu. Baada yao mfalme mwingine atainuka, ambaye atakuwa tofauti na wale waliotangulia, naye atawaangusha wafalme watatu. 25 Atanena maneno kinyume cha Yeye Aliye Juu Sana na kuwaonea watakatifu wake, huku akijaribu kubadili sikukuu zao takatifu pamoja na sheria. Watakatifu watatiwa chini ya mamlaka yake kwa wakati, nyakati mbili, na nusu wakati
7.25 Wakati, nyakati mbili, na nusu wakati maana yake mwaka mmoja, miaka miwili, na nusu mwaka, yaani miaka mitatu na nusu
.

26 “ ‘Lakini ndipo mahakama itakapokaa kuhukumu, nayo mamlaka yake yataondolewa na kuangamizwa kabisa milele. 27 Ndipo ufalme, mamlaka na ukuu wa falme chini ya mbingu yote utakabidhiwa kwa watakatifu, watu wa Yeye Aliye Juu Sana. Ufalme wake utakuwa ufalme wa milele, nao watawala wote watamwabudu na kumtii yeye.’

28 “Huu ndio mwisho wa jambo lile. Mimi Danieli nilitaabika sana katika mawazo yangu, nao uso wangu ukabadilika, lakini nililiweka jambo hilo kuwa siri moyoni mwangu.”

Copyright information for Neno