Deuteronomy 13

Kuabudu Miungu Mingine

Kama nabii, au yule anayetabiri kwa njia ya ndoto, akijitokeza miongoni mwenu na akawatangazia ishara ya miujiza na ajabu, ikiwa ishara au ajabu ya aliyozungumza ikatokea, naye akasema, “Na tufuate miungu mingine” (miungu ambayo hamjaifahamu) “na tuiabudu,” kamwe msiyasikilize maneno ya nabii wala mwota ndoto huyo. BWANA Mungu wenu anawajaribu kuangalia kama mnampenda kwa moyo wenu wote na kwa roho yenu yote. Ni BWANA Mungu wenu ambaye mnapaswa kumfuata tena ni yeye mnapaswa kumheshimu. Shikeni maagizo yake na kumtii, mtumikieni na kushikamana naye. Huyo nabii au mwota ndoto lazima auawe, kwa sababu amehubiri uasi dhidi ya BWANA Mungu wenu, ambaye aliwatoa kutoka nchi ya Misri na kuwakomboa kutoka nchi ya utumwa; amejaribu kuwageuza kutoka njia ambayo BWANA Mungu wenu aliwaagiza mfuate. Ni lazima mwondoe uovu miongoni mwenu.

Kama ndugu yako hasa, au mwanao au binti yako, au mke umpendaye, au rafiki yako wa karibu sana akikushawishi kwa siri, akisema, “Na twende tukaabudu miungu mingine” (miungu ambayo ninyi wala baba zenu hamkuifahamu, miungu ya watu wanaowazunguka, ikiwa karibu au mbali, kutoka mwisho mmoja wa nchi mpaka mwingine), usikubali wala usimsikilize. Usimhurumie! Usimwache wala usimkinge. Hakika ni lazima auawe. Ni lazima mkono wako uwe wa kwanza katika kumwua kisha mikono ya watu wengine wote. 10 Mpigeni kwa mawe mpaka afe, kwa sababu alijaribu kuwageuza mtoke kwa BWANA Mungu wenu ambaye aliwatoa Misri, kutoka nchi ya utumwa. 11 Kisha Israeli wote watasikia na kuogopa, wala hakuna mmoja miongoni mwenu atakayefanya uovu tena.

12 Kama mkisikia ikisemwa kwamba moja ya miji ambayo BWANA Mungu wenu anawapa mkae ndani yake 13 kuna wanaume waovu wameinuka miongoni mwenu na wamewapotosha watu wa mji, wakisema, “Twendeni tukaabudu miungu mingine” (miungu ambayo hamkuifahamu), 14 ndipo itakubidi kuuliza, kupima na kuchunguza kwa makini. Kama ni kweli, tena ikihakikishwa kwamba jambo hili lichukizalo limefanyika miongoni mwenu, 15 kwa hakika ni lazima muwaue kwa upanga wale wote wanoishi katika mji ule. Uharibuni kabisa, pamoja na watu wake na mifugo yake. 16 Kusanyeni nyara zote za mji katika uwanja wa wazi na kuuchoma mji kabisa pamoja na nyara zake zote kama sadaka ya kuteketezwa kwa BWANA Mungu wenu. Utabaki kuwa magofu milele na hautajengwa tena. 17 Hakuna kimoja kati ya vitu vilivyolaaniwa kitakachokutwa mikononi mwenu, ili BWANA ageuze hasira yake kali. Atawahurumia na kuwa na rehema kwenu pia kuongeza idadi yenu, kama alivyowaahidi baba zenu, 18 kwa sababu mnamtii BWANA Mungu wenu, mkizishika amri zake zote zile ninazowapa leo na kufanya lile lililo jema machoni pake.

Copyright information for Neno