Deuteronomy 14

Vyakula Vilivyo Najisi Na Vilivyo Safi

1Ninyi ni watoto wa BWANA Mungu wenu. Msijichanje ama kujinyoa upara kwenye paji la uso kwa ajili ya aliyekufa, 2kwa maana ninyi ni taifa takatifu kwa BWANA Mungu wenu. BWANA amewachagua ninyi kuwa taifa la kipekee kutoka mataifa yote juu ya uso wa dunia, mwe tunu yake.

3Msile kitu cho chote ambacho ni machukizo. 4Hawa ndio wanyama mtakaokula: ng'ombe, kondoo, mbuzi, 5kulungu, paa, kongoni, paa mweupe, mbuzi-mwitu, pofu na kondoo wa mlimani. 6Mnaweza kumla mnyama ye yote mwenye kwato zilizogawanyika mara mbili, pia yule anayecheua. 7Hata hivyo, miongoni mwa wale wanaocheua au wale walio na kwato zilizogawanyika kamwe msile ngamia, sungura na pelele. Iwapo wanacheua, lakini hawana kwato zilizogawanyika; ni najisi kwenu kwa taratibu za kiibada. 8Nguruwe pia ni najisi; ingawa ana kwato zilizogawanyika, hacheui. Msile nyama yake wala kugusa mzoga wake.

9Katika viumbe hai vyote viishivyo kwenye maji, mnaweza kula ye yote aliye na mapezi pamoja na magamba. 10Lakini cho chote kisicho na mapezi na magamba msile; kwenu ni najisi.

11Mnaweza kula ndege ye yote aliye safi. 12Lakini wafuatao msiwale: tai, kipungu, kipungu mweusi, 13kengewa mwekundu, kengewa mweusi, mwewe wa aina yo yote, 14kunguru wa aina yo yote, 15mbuni, kirukanjia, dudumizi, kipanga wa aina yo yote 16bundi, muvurila, bundi mkubwa, 17mwari, nderi, ndezi, mnandi, 18membe, koikoi wa aina yo yote, hudihudi na popo.

19Wadudu wote warukao kwa makundi ni najisi kwenu, msiwale. 20Lakini viumbe vyote vyenye mabawa vilivyo safi mwaweza kula.

21Msile kitu cho chote mtakachokuta kimekufa. Mnaweza kumpa mgeni ye yote anayeishi katika mojawapo ya miji yenu, naye anaweza kula au mnaweza kumuuzia mtu wa nchi nyingine. Lakini ninyi ni watu watakatifu kwa BWANA Mungu wenu.

Msitokose mwana-mbuzi katika maziwa ya mama yake.

Zaka

22Hakikisheni mmetenga sehemu ya kumi ya mazao yote ya mashamba yenu kila mwaka. 23Mtakula zaka za nafaka yenu, divai mpya, mafuta na wazaliwa wa kwanza wa makundi yenu ya ng'ombe na ya kondoo na mbuzi mbele za BWANA Mungu wenu pale mahali atakapopachagua kama maskani kwa ajili ya Jina lake, ili kwamba mpate kujifunza kumheshimu BWANA Mungu wenu daima. 24Lakini ikiwa mahali pale ni mbali sana nanyi mmebarikiwa na BWANA Mungu wenu na hamwezi kubeba zaka yenu (kwa sababu mahali pale BWANA atakapopachagua kuliweka Jina lake ni mbali sana), 25basi badilisheni zaka yenu kuwa fedha, mkaichukue hiyo fedha mwende nayo mahali BWANA Mungu wenu atakapopachagua. 26Tumieni hiyo fedha kununua cho chote ukitakacho: ng'ombe, kondoo, divai au kinywaji cho chote chenye chachu au cho chote mnachotaka. Kisha ninyi na wa nyumbani mwenu mtaila mbele za BWANA Mungu wenu na kufurahi. 27Msiache kuwajali Walawi waishio katika miji yenu, kwa kuwa hao hawana shamba wala urithi wao wenyewe

28Mwishoni mwa kila mwaka wa tatu, leteni zaka zote za mazao ya miaka ile na uyahifadhi kwenye miji yenu, 29ili Walawi (ambao hawana mashamba wala urithi wao wenyewe) na wageni, yatima na wajane wanaoishi kwenye miji yenu wapate kuja kula na kushiba, ili BWANA Mungu wenu apate kuwabariki ninyi katika kazi zote za mikono yenu.

Copyright information for Neno