Deuteronomy 21

Upatanisho Kuhusu Mauaji

Kama mtu akikutwa ameuawa, naye amelala kwenye shamba katika nchi ambayo BWANA Mungu wenu anawapa kuimiliki, wala haijulikani ni nani aliyemwua, wazee wenu na waamuzi watatoka na kupima umbali kutoka maiti alipolala mpaka kwenye miji ya jirani. Kisha wazee wa ule mji uliokaribu zaidi na yule maiti watamchukua mtamba ambaye hajapata kufanyishwa kazi na ambaye hajafungwa nira, na kumpeleka kwenye bonde ambalo halijapata kulimwa au kupandwa mazao na ambapo kuna chemchemi itiririkayo. Huko kwenye hilo bonde watamvunja yule mtamba shingo. Makuhani, hao wana wa Lawi, watasogea mbele, kwa kuwa BWANA Mungu wenu, amewachagua kuhudumu na kutoa baraka katika jina la BWANA, na kuamua mashauri yote ya mabishano na mashambulio. Ndipo wazee wote wa mji ulio karibu zaidi na huyo maiti watanawa mikono yao juu ya huyo mtamba ambaye shingo yake imevunjwa huko kwenye bonde, nao watatangaza: “Mikono yetu haikumwaga damu hii, wala macho yetu hayakuona likifanyika. Ee BWANA, ukubali upatanisho kwa watu wako Israeli, ambao umewakomboa, wala usiwahesabie watu wako hatia ya damu ya mtu asiyekuwa na hatia.” Nayo damu iliyomwagika itakuwa imefanyiwa upatanisho. Hivyo mtakuwa mmejitakasa wenyewe kutoka hatia ya kumwaga damu isiyokuwa na hatia, kwa kuwa mmefanya lile lililo sawa mbele za macho ya BWANA.

Kuoa Mwanamke Mateka

10 Mkienda vitani kupigana na adui zenu naye BWANA Mungu wenu akawatia adui mikononi mwenu, nanyi mkachukua mateka, 11 kama ukiona miongoni mwa mateka mwanamke mzuri wa sura nawe wavutwa naye, waweza kumwoa akawa mke wako. 12 Mlete nyumbani mwako, anyoe nywele na kukata kucha zake, 13 avue nguo alizokuwa amevaa alipotekwa. Baada ya kuishi nyumbani mwako na kumwombolezea baba yake na mama yake kwa mwezi mzima, ndipo utakapoweza kumwendea na kuwa mume wake naye atakuwa mke wako. 14 Lakini kama hutaendelea kupendezwa naye, mwache aende po pote anapotaka. Kamwe huwezi kumuuza au kumtendea kama mtumwa, kwa sababu utakuwa umemvunjia heshima.

Haki Ya Mzaliwa Wa Kwanza

15 Kama mwanaume ana wake wawili, naye anampenda mmoja na mwingine hampendi na wote wawili wamemzalia wana wa kiume, lakini mwana mzaliwa wa kwanza ni wa yule mke asiyempenda, 16 wakati anapotoa wosia wa mali yake kwa wanawe, kamwe asitoe haki za mzaliwa wa kwanza kwa mwana wa mke ampendaye kwa upendeleo, badala ya mzaliwa hasa wa kwanza, ambaye ni mwana wa mke ambaye hampendi. 17 Ni lazima amkubali mwana wa mke asiyempenda kama mzaliwa wa kwanza kwa kumpa sehemu ya vile vyote alivyonavyo maradufu. Mwana huyo ni ishara ya kwanza ya nguvu za baba yake. Haki ya mzaliwa wa kwanza ni yake yeye.

Mwana Mwasi

18 Kama mtu ana mwana mkaidi na mwasi ambaye hamtii baba yake na mama yake, na hasikii wazazi wanapomrudi, 19 baba yake na mama yake watamleta kwa wazee kwenye lango la mji wake. 20 Watawaambia wazee, “Huyu mwanetu ni mkaidi na mwasi. Hatutii sisi, yeye ni mpotovu na mlevi.” 21 Kisha wanaume wote wa mjini mwake watampiga kwa mawe mpaka afe. Ndivyo imewapasa kuondoa maovu kati yenu. Israeli yote itasikia hili na kuogopa.

Sheria Mbalimbali

22 Kama mtu ana hatia ya kosa linalompasa kuuawa naye akauawa, mwili wake utaangikwa mtini, 23 kamwe msiuache mwili wake mtini usiku kucha. Hakikisheni mnauzika mwili wake siku ile ile, kwa sababu kila mtu anayeangikwa mtini yupo chini ya laana ya Mungu. Msiinajisi nchi ambayo BWANA Mungu wenu anawapa kama urithi wenu.

Copyright information for Neno