Deuteronomy 23

Kutengwa Na Mkutano

Asiingie mtu ye yote aliyehasiwa kwa kupondwa makende au kwa kukatwa uume wake katika kusanyiko la BWANA.

Mtu ye yote ambaye amezaliwa kwenye ndoa isiyo halali au wazao wake wasiingie kwenye kusanyiko la BWANA, hata mpaka kizazi cha kumi.

Hapatakuwa na Mwamori au Mmoabi au ye yote wa wazao wao atakayeruhusiwa kuingia katika kusanyiko la BWANA, hata mpaka kizazi cha kumi. Kwa kuwa hawakuja kuwalaki wakiwa na mkate na maji mlipokuwa njiani mlipotoka Misri, tena walimwajiri Balaamu mwana wa Beori kutoka Pethori iliyoko Aramu-Naharaimu
23.4 Yaani Mesopotamia ya Kaskazini-Magharibi
ili kuwalaani ninyi.
Hata hivyo, BWANA Mungu wenu hakumsikiliza Balaamu bali aligeuza laana kuwa baraka kwenu kwa sababu BWANA Mungu wenu anawapenda. Msitafute mapatano ya urafiki nao maisha yenu yote.

Usimchukie Mwedomu, kwa kuwa yeye ni ndugu yako. Usimchukie Mmisri, kwa sababu uliishi kama mgeni katika nchi yake. Kizazi cha tatu cha watoto watakaozaliwa nao wanaweza kuingia katika kusanyiko la BWANA.

Unajisi Katika Kambi

Unapokuwa umepiga kambi dhidi ya adui zako, jitenge na kitu cho chote kisicho safi. 10 Ikiwa mtu amechafuka kwa sababu ya kutokwa na shahawa usiku, inampasa atoke nje ya kambi na kukaa huko. 11 Lakini jioni ikikaribia ataoga, na baada ya jua kuzama ataingia tena kambini.

12 Tengeni mahali nje ya kambi ambapo mnaweza kwenda kujisaidia. 13 Kama sehemu ya vifaa vyenu iweni na kitu cha kulimia, nanyi mnapojisaidia, chimba shimo na kisha funika kile kikutokacho. 14 Kwa kuwa BWANA Mungu wenu hutembea katika kambi yenu ili kuwalinda na kuwaweka adui zenu mikononi mwenu. Kambi yenu ni lazima iwe takatifu, ili asione kitu cho chote miongoni mwenu kilicho kichafu akageuka na kuwaacha.

Sheria Mbalimbali

15 Ikiwa mtumwa amekimbilia kwako, usimrudishe kwa bwana wake. 16 Mwache aishi miongoni mwenu mahali po pote anapopapenda na katika mji wo wote anaochagua. Usimwonee.

17 Asiwepo Mwisraeli mwanamke kahaba au mwanaume hanithi wa mahali pa kuabudia miungu. 18 Kamwe usilete mapato ya ukahaba ikiwa ni ya mwanamke au ni ya mwanaume katika nyumba ya BWANA Mungu wako kwa ajili ya nadhiri yo yote, kwa sababu BWANA Mungu wako anachukizwa na yote mawili.

19 Usimtoze ndugu yako riba, iwe ni fedha ama chakula ama kitu kingine cho chote ambacho waweza kupata riba juu yake. 20 Unaweza kumtoza mgeni riba, lakini siyo nduguyo Mwisraeli, ili kwamba BWANA Mungu wako akubariki katika kila kitu unachoweka mkono katika nchi unayoiingia kuimiliki.

21 Ukiweka nadhiri kwa BWANA Mungu wako, usichelewe kuitimiza, kwa kuwa BWANA Mungu wako atakudai, nawe utakuwa na hatia ya dhambi. 22 Lakini ukijizuia kuweka nadhiri, hutakuwa na hatia. 23 Cho chote kitakachotamkwa kwa midomo yako ni lazima uhakikishe umekifanya, kwa sababu uliweka nadhiri yako kwa hiari mbele za BWANA Mungu wako kwa kinywa chako mwenyewe.

24 Kama ukiingia katika shamba la mizabibu la jirani yako, unaweza kula zabibu kadiri utakavyo, lakini usiweke cho chote kwenye kikapu chako. 25 Kama ukiingia katika shamba la nafaka la jirani yako, unaweza kukwanyua kwa mikono yako, lakini usikate kwa mundu nafaka iliyosimama.

Copyright information for Neno