Deuteronomy 26

Malimbuko Na Zaka

Mtakapokuwa mmeingia nchi ile ambayo BWANA Mungu wenu anawapa kama urithi na mtakapokuwa mmeimiliki na kukaa ndani yake, chukueni baadhi ya mavuno ya kwanza ya yale yote mtakayozalisha kutoka udongo wa nchi ambayo BWANA Mungu wenu anawapa na mweke kwenye kapu. Kisha uende mahali ambapo BWANA Mungu wako atapachagua kuwa makao kwa ajili ya Jina lake na umwambie kuhani atakayekuwapo kwa wakati huo, “Ninatangaza leo kwa BWANA Mungu wako kwamba nimekuja katika nchi ambayo BWANA aliwaapia baba zetu kwamba atatupa.” Kuhani atapokea lile kapu mikononi mwako na kuliweka chini mbele ya madhabahu ya BWANA Mungu wako. Kisha utatangaza mbele za BWANA Mungu wako: “Baba yangu alikuwa Mwarami aliyekuwa anatangatanga, akaenda Misri pamoja na watu wachache akaishi huko akawa taifa kubwa, lenye nguvu na watu wengi. Lakini Wamisri walituonea na kututaabisha, wakitufanyisha kazi ngumu. Kisha tulimlilia BWANA, Mungu wa baba zetu, naye BWANA akasikia sauti yetu na akaona huzuni yetu, taabu yetu na mateso yetu. Kwa hiyo BWANA akatutoa nchi ya Misri kwa mkono wenye nguvu na ulionyooshwa, pamoja na utisho mkuu, ishara za miujiza na maajabu. Akatuleta mahali hapa akatupa nchi hii, nchi inayotiririka maziwa na asali; 10 nami sasa ninaleta malimbuko ya ardhi ambayo wewe, Ee BWANA, umenipa.” Weka kapu mbele za BWANA Mungu wako na usujudu mbele zake. 11 Kisha wewe pamoja na Walawi na wageni wote walioko miongoni mwenu mtafurahi katika vitu vyote vizuri ambavyo BWANA Mungu wenu amewapa pamoja na wa nyumbani mwenu.

12 Wakati utakapokuwa umeshatoa zaka zote za mazao yako katika mwaka wa tatu, ambao ni mwaka wa zaka, utampa Mlawi, mgeni, yatima na mjane, ili waweze kula katika miji yenu na kushiba. 13 Kisha umwambie BWANA Mungu wako: “Nimeondoa katika nyumba yangu ile sehemu iliyowekwa wakfu na nimempa Mlawi, mgeni, yatima na mjane, kulingana na yote uliyoamuru. Sijazihalifu amri zako wala kusahau hata mojawapo. 14 Sijala sehemu iliyowekwa wakfu wakati nilipokuwa nikiomboleza, wala sijaondoa mojawapo wakati nilipokuwa najisi, wala sijatoa sehemu yake yo yote kwa wafu. Nimemtii BWANA Mungu wangu; nimefanya kila kitu ulichoniamuru. 15 Angalia chini kutoka mbinguni, maskani yako matakatifu, uwabariki watu wako Israeli pamoja na nchi uliyotupa kama ulivyoahidi kwa kiapo kwa baba zetu, nchi inayotiririka maziwa na asali.”

Fuata Maagizo Ya BWANA

16 BWANA Mungu wako anakuagiza leo kufuata amri hizi na sheria; zishike kwa bidii kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote. 17 Umetangaza leo kwamba BWANA ndiye Mungu wako na kwamba utafuata njia zake, kwamba utayashika maagizo yake, amri zake na sheria zake nawe utamtii. 18 Naye BWANA ametangaza leo kwamba ninyi ni taifa lake, hazina yake ya thamani kama alivyoahidi, ili kwamba mpate kuyashika maagizo yake yote. 19 Ametangaza kwamba atawaweka juu kuliko mataifa mengine aliyoyafanya katika sifa, kuwa fahari na heshima, na kwamba mtakuwa taifa takatifu kwa BWANA Mungu wenu, kama alivyoahidi.

Copyright information for Neno