Deuteronomy 30

Mafanikio Baada Ya Kumgeukia BWANA

1Wakati baraka hizi zote pamoja na laana nilizoziweka mbele yako zitakapokujia, nawe ukazitafakari moyoni popote BWANA Mungu wako atakapokutawanya miongoni mwa mataifa, 2hapo wewe na watoto wako mtakapomrudia BWANA Mungu wako, na kumtii kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote kulingana na kila kitu ninachokuamuru leo, 3ndipo BWANA Mungu wako atakapokurudisha kutoka utumwani na kukuhurumia, naye atakukusanya tena kutoka katika mataifa yote kule alikokutawanya wewe. 4Hata kama umefukuziwa katika nchi ya mbali kiasi gani chini ya mbingu, kutoka huko BWANA Mungu wako atakukusanya na kukurudisha. 5Atakurudisha katika nchi iliyokuwa mali ya baba zako, nawe utaimiliki. Atakufanya ufanikiwe sana na kukuzidisha kwa idadi kuliko baba zako. 6BWANA Mungu wako ataitairi mioyo yenu na mioyo ya wazao wenu ili mweze kumpenda kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote ukaishi. 7BWANA Mungu wako ataweka laana hizi zote juu ya adui zako ambao wanakuchukia na kukutesa. 8Utamtii tena BWANA na kuzishika amri zake zote ninazokupa leo. 9Ndipo BWANA Mungu wako atakapokufanikisha sana katika kazi zote za mikono yako na katika uzao wa tumbo lako, wadogo wa mifugo yako na mazao ya nchi yako. BWANA atakufurahia tena na kukufanikisha, kama alivyowafurahia baba zako, 10kama ukimtii BWANA Mungu wako, na kuzishika amri zake na maagizo yake ambayo yameandikwa katika Kitabu hiki cha Sheria, na kumgeukia BWANA Mungu wako kwa moyo wako wote na kwa roho yako yote.

Uzima Na Mauti

11Ninachokuagiza leo sio kigumu sana kwako au usichokiweza. 12Hakiko juu mbinguni, ili uulize, “Ni nani atakayepanda kwenda mbinguni kukileta na kututangazia ili tuweze kutii?” 13Wala hakiko ng'ambo ya bahari, ili uulize, “Ni nani atakayevuka bahari kwenda kukichukua na kututangazia ili tupate kutii?” 14La hasha! Lile neno liko karibu sana nawe; liko kinywani mwako na ndani ya moyo wako ili uweze kulitii.

15Tazama, naweka mbele yako leo uzima na mafanikio, mauti na maangamizo. 16Ninakuamuru leo kwamba umpende BWANA Mungu wako, utembee katika njia zake, na kutunza maagizo yake, amri na sheria zake; ndipo utakapoishi na kuongezeka, naye BWANA Mungu wako atakubariki katika nchi unayoiingia kuimiliki.

17Lakini kama moyo wako ukigeukia mbali ukawa huna utii, kama umevutwa kuisujudia miungu mingine na kuiabudu, 18nakutangazia leo hii kwamba hakika utaangamizwa. Hutaishi maisha marefu katika nchi unayovuka Yordani kuiingia na kuimiliki.

19Leo ninaziita mbingu na nchi kama mashahidi dhidi yako kwamba nimeweka mbele yako uzima na mauti, baraka na laana. Basi sasa chagueni uzima, ili wewe na watoto wako mpate kuishi, 20na ili upate kumpenda BWANA Mungu wako, uisikilize sauti yake na kuambatana naye. Kwa kuwa BWANA ndiye uzima wako, na atakupa wingi wa siku ili upate kuishi katika nchi aliyoapa kuwapa baba zako Abrahamu, Isaki na Yakobo.

Copyright information for Neno