Ecclesiastes 1

Kila Kitu Ni Ubatili Mtupu

1Maneno ya Mhubiri, mwana wa Daudi, mfalme huko Yerusalemu: 2“Ubatili mtupu! Ubatili mtupu!”
Mhubiri anasema.
“Ubatili mtupu!
Kila kitu ni ubatili.”
3Mwanadamu anafaidi nini kutokana na kazi yake yote
anayotaabikia chini ya jua?
4Vizazi huja na vizazi hupita,
lakini dunia inadumu milele.
5Jua huchomoza na jua huzama,
nalo huarakisha kurudi maawioni.
6Upepo huvuma kuelekea kusini
na kugeukia kaskazini,
hurudia mzunguko huo huo,
daima ukirudia njia yake.
7Mito yote hutiririka baharini,
hata hivyo bahari kamwe haijai.
Mahali mito inapotoka,
huko hurudi tena.
8Vitu vyote vinachosha,
zaidi kuliko mtu anavyoweza kusema.
Jicho kamwe halitosheki kutazama,
wala sikio halishibi kusikia.
9Kile kilichokuwapo kitakuwapo tena,
kile kilichofanyika kitafanyika tena,
hakuna kilicho kipya chini ya jua.
10Kuna kitu cho chote ambacho mtu anaweza kusema,
“Tazama! Kitu hiki ni kipya”?
Kilikuwapo tangu zamani za kale,
kilikuwapo kabla ya wakati wetu.
11Hakuna kumbukumbu ya watu wa zamani,
hata na wale ambao hawajaja bado
hawatakumbukwa
na wale watakaofuata baadaye.


Hekima Ni Ubatili

12Mimi, Mhubiri, nilikuwa mfalme katika Yerusalemu. 13Nilitumia muda wangu wote kujifunza na kuvumbua kwa hekima yote yanayofanyika chini ya mbingu. Jinsi gani Mungu ameweka mzigo mzito juu ya wanadamu! 14Nimeshaona mambo yote yanayotendeka chini ya jua, hayo yote ni ubatili, hii ni kukimbiza upepo. 15

Kilichopindika hakiwezekani kunyoshwa,
kile ambacho hakipo haiwezekani kukihesabu.


16Niliwaza mwenyewe, “Tazama, nimekua na kuongezeka katika hekima kuliko ye yote aliyewahi kutawala Yerusalemu kabla yangu. Nimekuwa na uzoefu mkubwa wa hekima na maarifa.” 17Ndipo nilipojitahidi kufahamu kutofautisha hekima, wazimu na upumbavu, lakini nikatambua hata hili nalo ni kukimbiza upepo. 18Kwa kuwa hekima nyingi huleta huzuni kubwa;
maarifa yanapoongezeka, masikitiko yanaongezeka.


Copyright information for Neno