Ecclesiastes 11

Mkate Juu Ya Maji

1Tupa mkate wako juu ya maji,
kwa maana baada ya siku nyingi
utaupata tena.
2Wape sehemu watu saba, naam hata wanane,
kwa maana hujui ni baa gani
litakalokuwa juu ya nchi.
3Kama mawingu yamejaa maji,
hunyesha mvua juu ya nchi.
Kama mti ukianguka kuelekea kusini
au kuelekea kaskazini,
mahali ulipoangukia,
hapo ndipo utakapolala.
4Ye yote atazamaye upepo hatapanda,
ye yote aangaliaye mawingu hatavuna.
5Kama vile usivyofahamu njia ya upepo,
au jinsi mwili uumbwavyo
ndani ya tumbo la mama,
vivyo hivyo huwezi kufahamu kazi ya Mungu,
Muumba wa vitu vyote.
6Panda mbegu yako asubuhi,
nako jioni usiruhusu mikono yako ilegee,
kwa maana hujui ni ipi itakayofanikiwa,
kwamba ni hii au ni ile,
au kwamba zote zitafanikiwa sawasawa.

Mkumbuke Muumba Wako Ukiwa Bado Kijana

7Nuru ni tamu,
tena inafurahisha macho kuona jua.
8Hata kama mtu ataishi miaka mingi kiasi gani,
na aifurahie yote.
Lakini na akumbuke siku za giza,
kwa maana zitakuwa nyingi.
Kila kitu kitakachokuja ni ubatili.
9Furahi ewe kijana, wakati ungali kijana,
moyo wako na ukupe furaha
katika siku za ujana wako.
Fuata njia za moyo wako
na cho chote macho yako yaonayo,
lakini ujue kwamba kwa ajili ya haya yote
Mungu atakuleta hukumuni.
10Kwa hiyo basi, ondoa wasiwasi moyoni mwako
na utupilie mbali masumbufu ya mwili wako,
kwa kuwa ujana na nguvu ni ubatili.
Copyright information for Neno