Ecclesiastes 6

1Nimeona ubaya mwingine chini ya jua, nao unalemea sana wanadamu: 2Mungu humpa mwanadamu utajiri, mali na heshima, hivyo hakukosa cho chote moyo wake unachokitamani. Lakini Mungu hamwezeshi kuvifurahia, badala yake mgeni ndiye anayevifurahia. Hili ni ubatili, ni ubaya unaosikitisha.

3Mtu anaweza kuwa na watoto mia moja naye akaishi miaka mingi, lakini haidhuru kuwa ataishi muda mrefu kiasi gani, kama hawezi kufurahia mafanikio yake na kwamba hapati mazishi ya heshima, ninasema afadhali mtoto aliyezaliwa akiwa amekufa kuliko yeye. 4Kuzaliwa kwake hakuna maana, huondokea gizani na gizani jina lake hufunikwa. 5Ingawa hakuwahi kuliona jua wala kujua kitu cho chote, yeye ana pumziko zaidi kuliko mtu huyo, 6Hata kama huyo mtu ataishi miaka elfu mara mbili na zaidi, lakini akashindwa kufurahia mafanikio yake, je, wote hawaendi sehemu moja? 7

Juhudi zote za binadamu ni kwa ajili ya kinywa chake,
hata hivyo hamu yake kamwe haitoshelezwi.
8Mtu mwenye hekima ana faida gani
zaidi ya mpumbavu?
Mtu maskini anapata faida gani
kwa kujua jinsi ya kujistahi
mbele ya watu wengine?
9Ni bora kile ambacho jicho linakiona
kuliko hamu isiyotoshelezwa.
Hili nalo ni ubatili,
ni kukimbiza upepo.
10Lo lote lililopo limekwisha kupewa jina,
naye mwanadamu alivyo ameshajulikana;
hakuna mtu awezaye kushindana
na mwenye nguvu kuliko yeye.
11Maneno yanavyokuwa mengi,
ndivyo yanavyokosa maana,
Je, hilo linamfaidia vipi ye yote?12Kwa maana ni nani anayejua lililo jema kwa ajili ya maisha ya mwanadamu, katika siku chache na za ubatili anazopita kama kivuli? Ni nani awezaye kumwambia yatakayotokea chini ya jua baada ya yeye kuondoka?

Copyright information for Neno