Ephesians 4

Umoja Katika Mwili Wa Kristo

Basi, mimi niliye mfungwa wa Bwana, nawasihi mwenende kama inavyostahili wito wenu mlioitiwa. Iweni wanyenyekevu kabisa na wapole, mkiwa wavumilivu, mkichukuliana kwa upendo. Jitahidini kudumisha umoja wa Roho katika kifungo cha amani. Kuna mwili mmoja na Roho mmoja, kama vile mlivyoitwa katika tumaini moja. Tena kuna Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja, Mungu mmoja ambaye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote, katika yote na ndani ya yote.

Lakini kila mmoja wetu amepewa neema kwa kadiri ya kipimo cha kipawa cha Kristo. Kwa hiyo husema: “Alipopaa juu zaidi,
4.8 Juu zaidi hapa ina maana mbingu za mbingu

aliteka mateka
akawapa wanadamu vipawa.”


(Asemapo “alipaa juu,” maana yake nini isipokuwa ni kusema pia kwamba Kristo alishuka pande za chini sana za dunia?
4.9 Pande za chini sana za dunia hapa maana yake Sheol kwa Kiebrania, yaani Kuzimu
10 Yeye aliyeshuka ndiye aliyepaa juu zaidi kupita mbingu zote, ili apate kuujaza ulimwengu wote.) 11 Yeye ndiye aliyeweka wengine kuwa mitume, wengine kuwa manabii, wengine kuwa wainjilisti, wengine kuwa wachungaji na walimu, 12 kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu kwa ajili ya kazi za huduma, ili kwamba mwili wa Kristo upate kujengwa 13 mpaka sote tutakapoufikia umoja katika imani na katika kumjua sana Mwana wa Mungu na kuwa watu wazima kwa kufikia kimo cha ukamilifu wa Kristo.

14 Ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu. 15 Badala yake, tukiambiana kweli kwa upendo, katika mambo yote tukue, hata tumfikie yeye aliye kichwa, yaani, Kristo. 16 Kutoka kwake, mwili wote ukiwa umeungamanishwa na kushikamanishwa pamoja kwa msaada wa kila kiungo, hukua na kujijenga wenyewe katika upendo, wakati kila kiungo kinafanya kazi yake.

Maisha Ya Zamani Na Maisha Mapya

17 Hivyo nawaambia hivi, nami nasisitiza katika Bwana kwamba, msiishi tena kama watu Mataifa waishivyo, katika ubatili wa mawazo yao. 18 Watu hao akili zao zimetiwa giza na wametengwa mbali na uzima wa Mungu kwa sababu ya ujinga wao kutokana na ugumu wa mioyo yao. 19 Wakiisha kufa ganzi, wamejitia katika mambo ya ufisadi na kupendelea kila aina ya uchafu, wakiendelea kutamani zaidi.

20 Lakini ninyi, hivyo sivyo mlivyomjifunza Kristo. 21 Kama hivyo ndivyo ilivyo, ninyi mmemsikia, tena mmefundishwa naye, vile kweli ilivyo katika Yesu. 22 Mlifundishwa kuuvua mwenendo wenu wa zamani, utu wenu wa kale, ulioharibiwa na tamaa zake za udanganyifu, 23 ili mfanywe upya roho na nia zenu, 24 mkajivike utu mpya, ulioumbwa sawasawa na mfano wa Mungu katika haki yote na utakatifu.

Kanuni Za Maisha Mapya

25 Kwa hiyo kila mmoja wenu avue uongo na kuambiana kweli mtu na jirani yake, kwa maana sisi sote tu viungo vya mwili mmoja. 26 Mkikasirika, msitende dhambi, wala jua lisichwe mkiwa bado mmekasirika, 27 wala msimpe ibilisi nafasi. 28 Yeye ambaye amekuwa akiiba, asiibe tena, lakini lazima ajishughulishe, afanye kitu kifaacho kwa mikono yake mwenyewe, ili awe na kitu cha kuwagawia wahitaji.

29 Maneno mabaya yasitoke vinywani mwenu, bali yale yafaayo kwa ajili ya kuwajenga wengine kulingana na mahitaji yao, ili yawafae wale wasikiao. 30 Wala msimhuzunishe Roho Mtakatifu wa Mungu, ambaye kwa huyo mlitiwa muhuri kwa ajili ya siku ya ukombozi. 31 Ondoeni kabisa uchungu, ghadhabu, hasira, makelele na masingizio pamoja na kila aina ya uovu. 32 Iweni wafadhili na wenye kuhurumiana ninyi kwa ninyi, mkisameheana, kama vile naye Mungu katika Kristo alivyowasamehe ninyi.

Copyright information for Neno