Ephesians 6

Mafundisho Kuhusu Watoto Na Wazazi

1Ninyi watoto, watiini wazazi wenu katika Bwana, kwa kuwa hili ni jema. 2“Waheshimu baba yako na mama yako,” hii ndio amri ya kwanza yenye ahadi, 3“upate baraka na uishi siku nyingi duniani.”

4Ninyi akina baba, msiwachokoze watoto wenu, bali waleeni kwa nidhamu na mafundisho ya Bwana.

Mafundisho Kuhusu Watumwa Na Mabwana

5Ninyi watumwa, watiini hao walio mabwana zenu hapa duniani kwa heshima na kwa kutetemeka na kwa moyo mmoja, kama vile mnavyomtii Kristo. 6Watiini, si tu wakati wakiwaona ili mpate upendeleo wao, bali mtumike kama watumwa wa Kristo, mkifanya mapenzi ya Mungu kwa moyo. 7Tumikeni kwa moyo wote, kama vile mnamtumikia Bwana na si wanadamu. 8Mkijua kwamba Bwana atampa kila mtu thawabu kwa lo lote jema alilotenda, kama yeye ni mtumwa au ni mtu huru.

9Nanyi mabwana, watendeeni watumwa wenu kwa jinsi iyo hiyo. Msiwatishe, kwa kuwa mnajua ya kwamba yeye aliye Bwana wenu na Bwana wao yuko mbinguni, naye hana upendeleo.

Silaha Za Mungu

10Hatimaye, mzidi kuwa hodari katika Bwana na katika uweza wa nguvu zake. 11Vaeni silaha zote za Mungu ili kwamba mweze kuzipinga hila za Shetani. 12Kwa maana kushindana kwetu si juu ya nyama na damu, bali dhidi ya falme, mamlaka, dhidi ya wakuu wa giza na majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho. 13Kwa hiyo vaeni silaha zote za Mungu ili mweze kushindana siku ya uovu itakapokuja nanyi mkiisha kufanya yote, simameni imara. 14Kwa hiyo simameni imara mkiwa mmejifunga kweli kiunoni na kuvaa dirii ya haki kifuani, 15nayo miguu yenu ifungiwe utayari tuupatao kwa Injili ya amani. 16Zaidi ya haya yote, twaeni ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye moto ya yule mwovu. 17Vaeni chapeo ya wokovu na mchukue upanga wa Roho, ambao ni Neno la Mungu. 18Mkiomba kwa Roho siku zote katika sala zote na maombi, mkikesha kila wakati mkiwaombea watakatifu wote.

19Niombeeni na mimi pia, ili kila nifunguapo kinywa changu, nipewe maneno ya kusema, niweze kutangaza siri ya Injili kwa ujasiri, 20ambayo mimi ni balozi wake katika vifungo. Ombeni ili nipate kuhubiri kwa ujasiri kama inipasavyo.

Salamu Za Mwisho

21Tikiko, aliye ndugu mpendwa na mtumishi mwaminifu katika Bwana, atawaambia kila kitu, ili pia mpate kujua hali yangu na kile ninachofanya sasa. 22Ninamtuma kwenu kwa ajili ya kusudi hili hasa, ili mpate kujua hali zetu, na awatie moyo.

23Amani iwe kwa ndugu, na pendo pamoja na imani kutoka kwa Mungu Baba na Bwana Yesu Kristo. 24Neema iwe na wote wampendao Bwana wetu Yesu Kristo kwa upendo wa dhati. Amen.

Copyright information for Neno