Exodus 10

Pigo La Nane: Nzige

1Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao, kwa kuwa nimeufanya moyo wake kuwa mgumu na mioyo ya maafisa wake ili kwamba nipate kutenda ishara hizi zangu za ajabu miongoni mwao 2ili upate kuwaeleza watoto wako na wajukuu wako jinsi nilivyowatendea Wamisri kwa ukali na jinsi nilivyofanya ishara zangu miongoni mwao, nanyi mpate kujua kuwa Mimi ndimi BWANA.”

3Kwa hiyo Mose na Aroni wakaenda kwa Farao na kumwambia, “Hili ndilo BWANA, Mungu wa Waebrania, asemalo: ‘Utaendelea hata lini kukataa kunyenyekea mbele yangu? Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu. 4Kama ukikataa kuwaachia waende, kesho nitaleta nzige katika nchi yako. 5Nao watafunika uso wa ardhi hata usionekana. Watatafuna mabaki machache yaliyobakizwa baada ya ile mvua ya mawe, yaani pamoja na kila mti unaoota katika mashamba yenu. 6Nzige hao watajaza nyumba zako, za maafisa wako wote na za Wamisri wote. Jambo ambalo baba zenu wala babu zenu hawajapata kuona tangu siku ile walipoanza kuishi katika nchi hii mpaka leo hii.’ ” Ndipo Mose akageuka na kumwacha Farao.

7Maafisa wa Farao wakamwambia, “Mpaka lini huyu mtu atakuwa tanzi kwetu? Waachie hao watu waende zao, ili wapate kumwabudu BWANA Mungu wao. Je, bado hutambui kuwa Misri imeangamia?”

8Ndipo Mose na Aroni wakaletwa kwa Farao. Farao akawaambia, “Nendeni, mkamwabudu BWANA Mungu wenu. Lakini ni nani hasa watakaokwenda?”

9Mose akajibu, “Tutakwenda na vijana wetu na wazee, pamoja na wana wetu na binti zetu, pia pamoja na kondoo zetu, ng'ombe, mbuzi, farasi na punda kwa sababu tutaadhimisha sikukuu kwa BWANA.”

10Farao akasema, “BWANA awe pamoja nanyi, kama nikiwaruhusu mwondoke pamoja na wanawake wenu na watoto wenu! Ni wazi kwamba mna makusudi mabaya. 11La hasha! Wanaume peke yao na waende, wakamwabudu BWANA, kwa kuwa hilo ndilo mmekuwa mkiomba.” Kwa hiyo Mose na Aroni wakaondolewa mbele ya Farao.

12Basi BWANA akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako juu ya Misri ili kundi la nzige liweze kuingia juu ya nchi na kutafuna kila kitu kiotacho katika mashamba na kila kitu kilichosazwa na ile mvua ya mawe.”

13Kwa hiyo Mose akanyosha fimbo yake juu ya Misri, BWANA akauleta upepo wa mashariki ukavuma katika nchi yote mchana wote na usiku kucha, kufikia asubuhi upepo ukawa umeleta nzige. 14Wakaivamia Misri yote na kukaa kila eneo la nchi kwa wingi. Kamwe hapajapata kuwepo pigo la nzige kama hilo, wala halitakuwepo tena. 15Wakafunika ardhi yote mpaka ardhi ikawa nyeusi. Wakatafuna kile chote kilichokuwa kimebakizwa na ile mvua ya mawe, kila kitu kiotacho mashambani pamoja na matunda kwenye miti. Hakuna kitu cho chote cha kijani kilichosalia katika miti au mmea katika nchi yote ya Misri.

16Farao akawaita Mose na Aroni kwa haraka na kuwaambia, “Nimetenda dhambi dhidi ya BWANA Mungu wenu na dhidi yenu pia. 17Sasa unisamehe dhambi yangu mara moja tena na umwombe BWANA Mungu wako aondoe pigo hili baya kwangu.”

18Kisha Mose akaondoka kwa Farao akamwomba BWANA. 19Naye BWANA akaugeuza upepo ukavuma kutoka magharibi, wenye nguvu nyingi, ambao uliwaondoa wale nzige na kuwapeleka kwenye Bahari ya Shamu. Hakuna nzige hata mmoja aliyebaki po pote katika nchi ya Misri. 20Lakini BWANA akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, wala hakuwaachia Waisraeli waondoke.

Pigo La Tisa: Giza

21Kisha BWANA akamwambia Mose, “Nyosha mkono wako kuelekea angani ili giza litande katika nchi ya Misri, giza ambalo watu wanaweza kulipapasa na kulihisi.” 22Kwa hiyo Mose akaunyosha mkono wake kuelekea angani, na giza nene likafunika pote katika nchi ya Misri kwa muda wa siku tatu. 23Hakuna mtu ye yote aliyeweza kumwona mwenzake, wala kuondoka mahali alipokuwa kwa muda wa siku tatu. Lakini Waisraeli wote walikuwa na mwanga katika maeneo yao waliyokuwa wanaishi.

24Ndipo Farao akamwita Mose na kusema, “Nendeni, mkamwabudu BWANA. Hata wanawake na watoto wenu mwaweza kwenda nao pia, lakini kondoo, mbuzi na ng'ombe wenu waacheni.”

25Lakini Mose akasema, “Huna budi kuturuhusu tuwe na dhabihu na sadaka za kuteketezwa za kutoa mbele za BWANA Mungu wetu. 26Sisi ni lazima tuondoke na mifugo yetu pia, wala hakuna ukwato utakaoachwa nyuma. Inatupasa kutumia baadhi ya hiyo mifugo katika kumwabudu BWANA Mungu wetu, kwa kuwa mpaka tutakapofika huko hatutakuwa tumefahamu ni nini tutakachotumia katika kumwabudu BWANA.”

27Lakini BWANA akaufanya moyo wa Farao kuwa mgumu, hakuwa radhi kuwaachia waondoke. 28Farao akamwambia Mose, “Ondoka mbele yangu! Hakikisha kuwa hutakuja mbele yangu tena! Siku ile utakapouona uso wangu utakufa.”

29Mose akamjibu, “Iwe kama ulivyosema! Kamwe sitauona uso wako tena.”

Copyright information for Neno