Exodus 31

Bezaleli Na Oholiabu

Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Tazama, nimemchagua Bezaleli mwana wa Uri, mwana wa Huri, wa kabila la Yuda, nami nimemjaza Roho wa Mungu, pamoja na ustadi, uwezo na maarifa katika aina zote za ufundi, ili kubuni kazi za ustadi katika ufundi wa dhahabu, fedha na shaba, kuchonga vito vya kutia mahali, kufanya kazi kwa mbao na kujishughulisha na aina zote za ufundi. Tena nimemweka Oholiabu mwana wa Ahisamaki, wa kabila la Dani, ili kumsaidia. Pia mafundi wote nimewapa ustadi wa kufanya kila kitu nilichokuamuru wewe: Hema la Kukutania, Sanduku la Ushuhuda pamoja na kiti cha rehema juu yake, pia na vifaa vyote vya kwenye hema, meza na vifaa vyake, kinara cha taa cha dhahabu safi na vifaa vyake vyote, madhabahu ya kufukizia uvumba, madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa na vyombo vyake vyote, sinia na kinara chake, 10 pamoja na mavazi matakatifu yaliyofumwa ya kuhani Aroni, na mavazi kwa ajili ya wanawe wakati wanahudumu katika kazi ya ukuhani, 11 pia mafuta ya upako na uvumba wenye harufu nzuri kwa ajili ya Mahali Patakatifu. Watavitengeneza sawasawa kama vile nilivyokuagiza wewe.”

Sabato

12 Kisha BWANA akamwambia Mose, 13 “Waambie Waisraeli, ‘Ninyi ni lazima mzishike Sabato zangu. Hii itakuwa ni ishara kati yangu na ninyi kwa ajili ya vizazi vijavyo, ili mpate kujua kwamba Mimi Ndimi BWANA, niwafanyaye ninyi watakatifu.

14 “ ‘Mtaishika Sabato, kwa sababu ni takatifu kwenu. Ye yote atakayeinajisi lazima auawe, ye yote atakayefanya kazi siku hiyo lazima akafie mbali na watu wake. 15 Kwa siku sita, mtafanya kazi, lakini siku ya saba ni Sabato ya kupumzika, takatifu kwa BWANA. Ye yote afanyaye kazi yo yote siku ya Sabato ni lazima auawe. 16 Waisraeli wataishika Sabato, kuiadhimisha kwa vizazi vijavyo kuwa Agano la milele. 17 Itakuwa ishara kati yangu na Waisraeli milele, kwa kuwa kwa muda wa siku sita BWANA aliumba mbingu na dunia, na siku ya saba akaacha kufanya kazi, akapumzika.’ ”

18 BWANA alipomaliza kusema na Mose juu ya Mlima Sinai, Mungu akampa vile vibao viwili vya Ushuhuda, vibao vya mawe vilivyoandikwa kwa kidole cha Mungu.

Copyright information for Neno