Exodus 8

Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Nenda kwa Farao ukamwambie, ‘Hili ndilo asemalo BWANA: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu. Kama ukikataa kuwaruhusu kuondoka, basi nitaipiga nchi yako yote kwa kuwaletea vyura. Mto Nile utafurika vyura. Watakuja kwenye jumba lako la kifalme na katika chumba chako cha kulala na kitandani mwako, katika nyumba za maafisa wako na kwa watu wako, vyura hao wataingia katika meko yenu na kwenye vyombo vya kukandia unga. Vyura watapanda juu yako, juu ya watu wako na maafisa wako wote.’ ”

Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Mwambie Aroni, ‘Nyosha mkono wako ukiwa na ile fimbo yako juu ya vijito, mifereji na madimbwi, fanya vyura waje juu ya nchi ya Misri.’ ”

Ndipo Aroni akaunyosha mkono wake juu ya maji ya Misri, nao vyura wakatokea na kuifunika nchi. Lakini waganga wakafanya vivyo hivyo kwa siri ya uganga wao, nao pia wakafanya vyura kuja juu ya nchi ya Misri.

Ndipo Farao akamwita Mose na Aroni na kusema, “Mwombeni BWANA awaondoe vyura kutoka kwangu na kwa watu wangu, nami nitawaachia watu wenu waende kumtolea BWANA dhabihu.”

Mose akamwambia Farao, “Ninakupa heshima ya kuamua ni wakati gani wa kukuombea wewe, maafisa wako na watu wako ili kwamba vyura watoke kwenu na kwenye nyumba zenu. Isipokuwa wale walio katika Mto Nile.”

10 Farao akasema, “Kesho.”

Mose akamjibu, “Itakuwa kama unavyosema, ili upate kujua kwamba hakuna ye yote kama BWANA Mungu wetu.
11 Vyura wataondoka kwako na katika nyumba zako, kwa maafisa wako na kwa watu wako, ila watabakia katika Mto Nile tu.”

12 Baada ya Mose na Aroni kuondoka kwa Farao, Mose akamlilia BWANA kuhusu vyura aliokuwa amewaleta kwa Farao. 13 Naye BWANA akafanya lile Mose alilomwomba. Vyura wafia ndani ya nyumba, viwanjani na mashambani. 14 Wakayakusanya malundo, nchi nzima ikanuka. 15 Lakini Farao alipoona pametokea nafuu, akaushupaza moyo wake na hakuwasikiliza Mose na Aroni, kama vile BWANA alivyokuwa amesema.

Pigo La Tatu: Viroboto

16 Ndipo BWANA akamwambia Mose, “Mwambie Aroni, ‘Nyosha fimbo yako uyapige mavumbi ya ardhi,’ nayo nchi yote ya Misri mavumbi yatakuwa viroboto.” 17 Wakafanya hivyo, Aroni aliponyosha mkono wake wenye fimbo na kuyapiga mavumbi ya nchi, viroboto wakawajia watu na wanyama. Mavumbi yote katika nchi ya Misri yakawa viroboto. 18 Lakini waganga walipojaribu kutengeneza viroboto kwa siri ya uganga wao, hawakuweza. Nao viroboto walikuwa juu ya watu na wanyama.

19 Waganga wale wakamwambia Farao, “Hiki ni kidole cha Mungu.” Lakini moyo wa Farao ukawa mgumu naye hakuwasikiliza, kama vile BWANA alivyosema.

Pigo La Nne: Mainzi

20 Kisha BWANA akamwambia Mose, “Amka mapema asubuhi na usimame mbele ya Farao wakati anapokwenda mtoni nawe umwambie, ‘Hili ndilo BWANA asemalo: Waachie watu wangu waende, ili wapate kuniabudu. 21 Kama hutawaachia watu wangu waondoke nitakupelekea makundi ya mainzi juu yako, kwa maafisa wako, kwa watu wako na kwenye nyumba zenu. Nyumba za Wamisri zitajazwa mainzi, hata na ardhi yote ya Misri.

22 “ ‘Lakini siku ile nitafanya kitu tofauti katika nchi ya Gosheni, ambapo watu wangu wanaishi, hapatakuwepo na makundi ya mainzi, ili mpate kujua kwamba Mimi, BWANA, niko katika nchi hii. 23 Nitaweka tofauti kati ya watu wangu na watu wenu. Ishara hii ya ajabu itatokea kesho.’ ”

24 Naye BWANA akafanya hivyo. Makundi makubwa ya mainzi yalimiminika katika jumba la kifalme la Farao na katika nyumba za maafisa wake, pia nchi yote ya Misri ikaharibiwa na mainzi.

25 Ndipo Farao akamwita Mose na Aroni na kuwaambia, “Nendeni mkamtolee Mungu wenu dhabihu katika nchi hii.”

26 Lakini Mose akamwambia, “Hilo halitakuwa sawa. Dhabihu tutakazomtolea BWANA Mungu wetu zitakuwa chukizo kwa Wamisri. Kama tukitoa dhabihu ambazo ni chukizo mbele yao, je, hawatatupiga mawe? 27 Ni lazima twende mwendo wa siku tatu mpaka tufike jangwani ili tumtolee BWANA Mungu wetu dhabihu, kama alivyotuagiza.”

28 Farao akamwambia, “Nitawaruhusu mwende kumtolea BWANA Mungu wenu dhabihu huko jangwani, lakini hamna ruhusa kwenda mbali sana. Sasa mniombee.”

29 Mose akajibu, “Mara tu nitakapoondoka, nitamwomba BWANA na kesho mainzi yataondoka kwa Farao, kwa maafisa wake na kwa watu wake. Hakikisha tu kwamba Farao hatatenda kwa udanganyifu tena kwa kutokuwaachia watu waende kumtolea BWANA dhabihu.”

30 Ndipo Mose akamwacha Farao na kumwomba BWANA, 31 naye BWANA akafanya lile Mose alilomwomba. Mainzi yakaondoka kwa Farao, kwa maafisa wake na kwa watu wake, wala hakuna hata inzi aliyebakia. 32 Lakini wakati huu pia Farao akaushupaza moyo wake, wala hakuwaruhusu Waisraeli waondoke.

Copyright information for Neno