Exodus 2

Kuzaliwa Kwa Mose

1Basi mtu mmoja wa nyumba ya Lawi akaoa mwanamke Mlawi, 2naye mwanamke huyo akapata mimba, akazaa mtoto wa kiume. Alipoona mtoto huyo ni mzuri, akamficha kwa miezi mitatu. 3Lakini alipoona hawezi kumficha zaidi, akamtengenezea kisafina cha matete, akakipaka lami. Kisha akamweka huyo mtoto ndani yake, akakificha katikati ya matete kando ya ukingo wa Mto Nile. 4Dada wa huyo mtoto akasimama mbali ili kuona kitakachompata mtoto.

5Ndipo binti Farao akatelemka mtoni Nile kuoga, nao wahudumu wake wakawa wanatembea ukingoni mwa mto. Binti mfalme akaona kisafina katikati ya manyasi, akamtuma mmoja wa mtumwa wake wa kike kukichukua. 6Alifungua kisafina akaona mtoto ndani yake. Mtoto alikuwa akilia, akamhurumia. Akasema, “Huyu ni mmoja wa watoto wa Kiebrania.”

7Ndipo dada wa huyo mtoto akamwuliza binti Farao, “Je, niende nikakutafutie mmoja wa wanawake wa Kiebrania akulelee huyu mtoto?”

8Binti Farao akamjibu, “Ndiyo, nenda.” Yule msichana akaenda akamleta mama wa mtoto. 9Binti Farao akamwambia, “Mchukue huyu mtoto unisaidie kumlea, nami nitakulipa.” Basi yule mwanamke akamchukua mtoto na kumlea. 10Mtoto alipokua, akampeleka kwa binti Farao, naye akawa mwanawe. Akamwita jina lake Mose, akisema, “Nilimtoa kwenye maji.”

Mose Akimbilia Midiani

11Siku moja, baada ya Mose kukua, akaondoka kwenda walikokuwa watu wake, na akachunguza jinsi walivyokuwa wakifanya kazi ngumu. Akamwona Mmisri akimpiga Mwebrania, mmojawapo wa watu wake. 12Mose akatazama huku na huko asione mtu ye yote, akamwua yule Mmisri, akamficha mchangani. 13Kesho yake akatoka, akaona Waebrania wawili wakipigana. Akamwuliza yule aliyekosa, “Mbona unampiga Mwebrania mwenzako?”

14Yule mtu akamjibu, “Ni nani aliyekuweka wewe kuwa mtawala na mwamuzi juu yetu? Je, unataka kuniua kama ulivyomwua yule Mmisri?” Ndipo Mose akaogopa na kuwaza, “Jambo lile nililofanya lazima limefahamika.”

15Farao aliposikia jambo hili, alijaribu kumwua Mose, lakini Mose akamkimbia Farao na kwenda kuishi katika nchi ya Midiani, akaketi kando ya kisima. 16Kuhani wa Midiani alikuwa na binti saba, nao wakaja kisimani ili kuchota maji na kujaza hori kwa ajili ya kunyweshea mifugo ya baba yao. 17Baadhi ya wachungaji wakaja wakawafukuza hao wasichana. Ndipo Mose akainuka, akawasaidia na kunywesha mifugo yao.

18Hao wasichana waliporudi nyumbani kwa Reueli baba yao, akawauliza, “Imekuwaje leo mmerudi mapema hivyo?”

19Wakamjibu, “Mmisri mmoja alituokoa kutoka mikononi mwa wachungaji. Pia mtu huyo alituchotea maji na kunywesha mifugo.”

20Akawauliza binti zake, “Yuko wapi? Mbona mmemwacha? Mkaribisheni ale chakula.”

21Mose akakubali kukaa kwa huyo mtu, ambaye alimpa Mose binti yake aliyeitwa Sipora amwoe. 22Sipora alizaa mtoto wa kiume, naye Mose akamwita Gershoni, akisema, “Nimekuwa mgeni katika nchi ya kigeni.”

23Baada ya muda mrefu, mfalme wa Misri akafa. Waisraeli wakalia kwa huzuni katika utumwa wao, walilia na kilio chao cha kutaka msaada kwa ajili ya utumwa kikamfikia Mungu. 24Mungu akasikia kilio chao cha huzuni, akakumbuka Agano alilofanya na Abrahamu pamoja na Isaki na Yakobo. 25Kwa hiyo Mungu akawaangalia Waisraeli na kuwahurumia.

Copyright information for Neno