Ezekiel 1

Viumbe Hai Na Utukufu Wa BWANA

1Katika mwaka wa thelathini, mwezi wa nne, siku ya tano ya mwezi, wakati nilipokuwa miongoni mwa hao waliokuwa uhamishoni kando ya Mto Kebari, mbingu zilifunguka nami nikaona maono ya Mungu.

2Katika siku ya tano ya mwezi, ilikuwa mwaka wa tano wa kuhamishwa kwa Mfalme Yehayakini, 3neno la BWANA lilimjia Ezekieli kuhani, mwana wa Buzi, kando ya Mto Kebari, katika nchi ya Wakaldayo. Huko mkono wa BWANA ulikuwa juu yake.

4Nilitazama, nikaona dhoruba kubwa ikitoka kaskazini, wingu kubwa sana pamoja likiwa na umeme wa radi likiwa limezungukwa na mwanga mkali. Katikati ya huo moto kulikuwa kama rangi ya manjano ya chuma kinapokuwa ndani ya moto. 5Katika ule moto kulikuwa na kitu kinachofanana na viumbe vinne vyenye uhai. Katika kuonekana kwake vilikuwa na umbo mfano wa mwanadamu, 6lakini kila kimoja kilikuwa na nyuso nne na mabawa manne. 7Miguu yao ilikuwa imenyooka, nyayo za miguu yao zilikuwa kama kwato za miguu ya ndama, nazo zilimetameta kama shaba iliyosuguliwa. 8Chini ya mabawa yao katika pande zao nne walikuwa na mikono ya mwanadamu. Wote wanne walikuwa na nyuso na mabawa, 9nayo mabawa yao yaligusana. Kila mmoja alikwenda kuelekea mbele moja kwa moja, hawakugeuka walipokuwa wanatembea.

10Kuonekana kwa nyuso zao kulikuwa hivi: Kila mmoja wa wale wanne alikuwa na uso wa mwanadamu na kwa upande wa kulia kila mmoja alikuwa na uso wa simba, upande wa kushoto alikuwa na uso wa ng'ombe pia kila mmoja alikuwa na uso wa tai. 11Hivyo ndivyo zilivyokuwa nyuso zao. Mabawa yao yalikunjuliwa kuelekea juu, kila mmoja alikuwa na mabawa mawili ambayo kila moja liligusa bawa la mwenzake kila upande na mabawa mengine mawili yakifunika mwili wake. 12Kila mmoja alikwenda kuelekea mbele moja kwa moja. Po pote roho alipotaka kwenda, ndipo walipokwenda pasipo kugeuka. 13Kuonekana kwa vile viumbe hai katikati kulikuwa kama makaa ya mawe yanayowaka au kama mienge. Moto ule ulikuwa ukienda mbele na nyuma katikati ya vile viumbe, ulikuwa na mwangaza mkali na katikati ya ule moto kulitoka kimulimuli kama umeme wa radi. 14Vile viumbe vilipiga mbio kwenda na kurudi, kama vimulimuli vya umeme wa radi.

15Nilipokuwa nikitazama vile viumbe hai, niliona gurudumu moja juu ya ardhi kando ya kila kiumbe kikiwa na nyuso zake nne. 16Hivi ndivyo ilivyokuwa kuonekana kwa hayo magurudumu na muundo wake: yaling'aa kama zabarajadi, nayo yote manne yalifanana. Kila gurudumu lilikuwa na gurudumu jingine ndani yake. 17Yalipokwenda yalielekea upande wo wote wa pande nne walipoelekea wale viumbe, magurudumu hayakuzunguka wakati viumbe vile vilipokwenda. 18Kingo zake zilikuwa ndefu kwenda juu na za kutisha, nazo zote nne zilijawa na macho pande zote.

19Vile viumbe hai vilipokwenda, magurudumu yaliyokuwa kando yao yalisogea na wakati hivyo viumbe hai vilipoinuka kutoka ardhini magurudumu nayo yaliinuka. 20Mahali po pote roho alipokwenda wale viumbe nao walikwenda, nayo magurudumu yaliinuka pamoja navyo, kwa sababu roho ya vile viumbe hai alikuwa ndani ya hayo magurudumu. 21Wakati viumbe vile viliposogea, nayo magurudumu yalisogea, viumbe viliposimama kimya, nayo pia yalisimama kimya, viumbe vilipoinuka juu ya nchi magurudumu yaliinuliwa pamoja navyo kwa kuwa roho ya hivyo viumbe hai alikuwa ndani ya hayo magurudumu.

22Juu ya vichwa vya hao viumbe hai palikuwa na kitu mfano wa eneo lililokuwa wazi, lililokuwa angavu kabisa na lenye kutisha. 23Chini ya hiyo nafasi mabawa yao yalitanda moja kuelekea jingine, kila mmoja alikuwa na mabawa mengine mawili yaliyofunika mwili wake. 24Viumbe wale waliposogea nilisikia sauti ya mabawa yao, kama ngurumo ya maji yaendayo kasi, kama sauti ya Mwenyezi
1.24 Mwenyezi hapa ina maana ya Shaddai kwa Kiebrania
, kama makelele ya jeshi. Waliposimama kimya walishusha mabawa yao.

25Ndipo ikaja sauti toka juu ya ile nafasi ya wazi iliyokuwa juu ya vichwa vyao, wakati waliposimama mabawa yao yakiwa yameshushwa. 26Juu ya ile nafasi ya wazi iliyokuwa juu ya vichwa vyao kulikuwa na kitu mfano wa kiti cha enzi kuonekana kwake chenye rangi ya yakuti samawi, na juu ya kile kiti cha enzi kulikuwa na umbo mfano wa mwanadamu. 27Nikaona kwamba kutokana na kile nilichoona kama kiuno chake kuelekea juu alionekana kama chuma inayowaka kana kwamba imejaa moto na kuanzia kiuno kwenda chini alionekana kama moto na mwanga mkali ulimzunguka. 28Kama vile kuonekana kwa upinde wa mvua mawinguni siku ya mvua, ndivyo ulivyokuwa ule mng'ao uliomzunguka.

Hivi ndivyo ilivyokuwa kuonekana kwa utukufu wa BWANA. Nilipouona, nikaanguka kifudifudi, nikasikia sauti ya mtu anaongea.

Copyright information for Neno