Ezekiel 15

Yerusalemu Mzabibu Usiofaa

1Neno la BWANA likanijia kusema: 2“Mwanadamu, je, ni vipi mti wa mzabibu unaweza kuwa bora zaidi kuliko tawi la mti mwingine wo wote ndani ya msitu? 3Je, mti wake kamwe huchukuliwa na kutengeneza cho chote cha manufaa? Je, watu hutengeneza vigingi vya kuning'inizia vitu kutokana na huo mti wake? 4Nao baada ya kutiwa motoni kama nishati na moto ukateketeza ncha zote mbili na kuunguza sehemu ya kati, je, unafaa kwa lo lote? 5Kama haukufaa kitu cho chote ulipokuwa mzima, je, si zaidi sana sasa ambapo hauwezekani kufanyishwa cho chote cha kufaa baada ya moto kuuchoma na kuuunguza?

6“Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Kama nilivyoutoa mti wa mzabibu miongoni mwa miti ya msituni kuwa nishati kwa ajili ya moto, hivyo ndivyo nitakavyowatendea watu waishio Yerusalemu. 7Nitaukaza uso wangu dhidi yao. Ingawa watakuwa wameokoka kwenye moto, bado moto utawateketeza. Nami nitakapoukaza uso wangu dhidi yao, ninyi mtajua kwamba Mimi ndimi BWANA. 8Nitaifanya nchi kuwa ukiwa kwa sababu wamekuwa si waaminifu, asema BWANA Mwenyezi.”

Copyright information for Neno