Ezekiel 23

Dada Wawili Makahaba

Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, walikuwepo wanawake wawili, binti wa mama mmoja. Wakawa makahaba huko Misri, wakajitia kwenye ukahaba tangu ujana wao. Katika nchi ile vifua vyao vya ubikira vikakumbatiwa huko na wakapoteza ubikira wao. Mkubwa aliitwa Ohola na mdogo wake Oholiba. Walikuwa wangu nao wakazaa wavulana na msichana. Ohola ni Samaria, Oholiba ni Yerusalemu.

“Ohola akajitia kwenye ukahaba alipokuwa bado ni wangu, akatamani sana wapenzi wake, mashujaa Waashuru, waliovaa nguo za buluu, watawala na majemadari, wote walikuwa wanaume vijana wa kuvutia, wapandao farasi. Akafanya ukahaba na wasomi wote wa Kiashuru na kujinajisi kwa sanamu zote za kila mwanaume aliyemtamani. Hakuacha ukahaba wake aliouanza huko Misri, wakati ambapo tangu ujana wake wanaume walilala naye, wakikumbatia kifua cha ubikira wake na kumwaga tamaa zao juu yake.

“Kwa hiyo nilimtia mikononi mwa wapenzi wake, Waashuru, kwa kuwa ndio aliowatamani. 10 Wakamvua nguo zake wakamwacha uchi, wakawachukuwa wanawe na binti zake, naye wakamwua kwa upanga. Akawa kitu cha kudharauliwa miongoni mwa wanawake na adhabu ikatolewa dhidi yake.

11 “Oholiba dada yake aliliona jambo hili, lakini kwa tamaa zake na ukahaba wake, akaharibu tabia zake kuliko Ohola dada yake. 12 Yeye naye aliwatamani Waashuru, watawala na majemadari, mashujaa waliovalia sare, wapandao farasi, wanaume vijana wote waliovutia. 13 Nikaona kuwa yeye pia alijinajisi, wote wawili wakaelekea njia moja.

14 “Lakini yeye akazidisha ukahaba wake. Akaona wanaume waliochorwa ukutani, picha za Wakaldayo waliovalia nguo nyekundu, 15 wakiwa na mikanda viunoni mwao na vilemba vichwani mwao, wote walifanana na maafisa wa Kikaldayo wapandao magari ya vita, wenyeji wa Ukaldayo. 16 Mara tu alipowaona, aliwatamani akatuma wajumbe kwao huko Ukaldayo. 17 Ndipo hao Wakaldayo wakaja kwake, kwenye kitanda cha mapenzi, nao katika tamaa zao wakamtia unajisi. Baada ya kutiwa unajisi akawaacha kwa kuwachukia. 18 Alipofanya ukahaba wake waziwazi na kuonyesha hadharani uchi wake, nilimwacha kwa kuchukia, kama vile nilivyokuwa nimemwacha dada yake. 19 Lakini akazidisha zaidi ukahaba wake alipozikumbuka siku zake za ujana, alipokuwa kahaba huko Misri. 20 Huko aliwatamani wapenzi wake, ambao viungo vyao vya uzazi ni kama vya punda na kile kiwatokacho ni kama kiwatokacho farasi. 21 Hivyo ulitamani uasherati wa ujana wako wakati ulipokuwa Misri kifua chako kilipokumbatiwa na walipokutomasa kwa sababu ya matiti yako machanga.

22 “Kwa hiyo, Oholiba, hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Nitawachochea wapenzi wako wawe kinyume na wewe, wale uliowaacha kwa kuchukia, nitawaleta dhidi yako kutoka kila upande, 23 yaani Wababeli na Wakaldayo wote, watu toka Pekodi, Shoa, Koa, wakiwa pamoja na Waashuri wote, vijana wazuri, watawala wote majemadari na maafisa wa magari ya vita na watu wa vyeo vya juu, wote wakiwa wamepanda farasi. 24 Watakuja dhidi yako wakiwa na silaha, magari ya vita, magari ya kukokota pamoja na umati mkubwa wa watu, watakuzingira pande zote kwa ngao na vigao na kofia za chuma. Nitakutia mikononi mwao ili wakuadhibu nao watakuadhibu sawasawa na sheria zao. 25 Nitaelekeza wivu wa hasira yangu dhidi yako nao watakushughulikia kwa hasira kali. Watakatilia mbali pua yako na masikio yako, na wale watakaosalia miongoni mwako watauawa kwa upanga. Watachukua wana wako na binti zako na wale watakaosalia miongoni mwenu watateketezwa kwa moto. 26 Watakuvua pia nguo zako na kuchukua mapambo yako yaliyotengenezwa kwa vito na dhahabu. 27 Hivyo ndivyo nitakavyokomesha uasherati wako na ukahaba wako uliouanza huko Misri. Hutatazama vitu hivi kwa kuvitamani tena wala kukumbuka Misri tena.

28 “Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ninakaribia kukutia mikononi mwa wale unaowachukia, kwa wale uliojitenga nao kwa kuwachukia. 29 Watakushughulikia kwa chuki na kukunyang'anya kila kitu ulichokifanyia kazi. Watakuacha uchi na mtupu na aibu ya ukahaba wako itafunuliwa. Uasherati wako na uzinzi wako 30 umekuletea haya yote, kwa sababu ulitamani mataifa na kujinajisi kwa sanamu zao. 31 Umeiendea njia ya dada yako, hivyo nitakitia kikombe chake mkononi mwako.

32 “Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “Utakinywea kikombe cha dada yako,
kikombe kikubwa na chenye kina kirefu;
nitaletea juu yako dharau na dhihaka,
kwa kuwa kimejaa sana.
33 Utalewa ulevi na kujawa huzuni,
kikombe cha maangamizo na ukiwa,
kikombe cha dada yako Samaria.
34 Utakinywa chote na kukimaliza;
utakivunja vipande vipande
na kuyararua matiti yako.


Nimenena haya, asema BWANA Mwenyezi.

35 “Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Kwa kuwa tangu uliponisahau mimi na kunitupa nyuma yako, lazima ubebe matokeo ya uasherati wako na ukahaba wako.”

36 BWANA akaniambia, “Mwanadamu, Je, utawahukumu Ohola na Oholiba? Basi wakabili kwa ajili ya matendo yao ya machukizo, 37 kwa kuwa wamefanya uzinzi na damu imo mikononi mwao. Wamefanya uzinzi na sanamu zao, hata wamewatoa watoto wao walionizalia kuwa kafara, kuwa chakula kwao. 38 Pia wamenifanyia hili: wakati huo huo wamenajisi patakatifu pangu na kuzitangua Sabato zangu. 39 Siku ile ile walitoa watoto wao kuwa kafara kwa sanamu zao, waliingia patakatifu pangu na kupatia unajisi. Hilo ndilo walilolifanya katika nyumba yangu.

40 “Walituma hata wajumbe kuwaita watu kutoka mbali, nao walipowasili ulioga kwa ajili yao, ukapaka macho yako rangi na ukavaa mapambo yako yaliyotengenezwa kwa vito vya dhahabu. 41 Ukaketi kwenye kiti cha anasa, kukiwa na meza iliyoandaliwa mbele yake ambayo juu yake ulikuwa umeweka uvumba na mafuta ambayo yalikuwa yangu.

42 “Kelele za umati wa watu wasiojali zilikuwa zimemzunguka, wakaleta watu wengi waliokuwa wakifanya makelele na walevi kutoka nyikani, ambao walitia bangili kwenye mikono ya yule mwanamke na dada yake na pia taji nzuri za kupendeza kwenye vichwa vyao. 43 Ndipo nikasema kuhusu yule aliyechakazwa na uzinzi, ‘Basi wamtumie kama kahaba, kwa kuwa ndivyo alivyo.’ 44 Nao wakazini naye. Kama vile watu wazinivyo na kahaba, ndiyo hivyo walivyozini na hao wanawake waasherati, Ohola na Oholiba. 45 Lakini watu wenye haki, watawahukumia adhabu wanawake wafanyao uzinzi na kumwaga damu, kwa kuwa ni wazinzi na damu iko mikononi mwao.

46 “Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo, Leteni watu wengi wenye makelele dhidi yao na uwaache wapate hofu na watekwe nyara. 47 Hao watu wengi watawapiga kwa mawe na kuwaua kwa panga zao, watawaua wana wao na binti zao na kuzichoma nyumba zao.

48 “Hivyo nitaukomesha uasherati katika nchi, ili wanawake wote wapate onyo nao wasije wakafanya uasherati kama ninyi mlivyofanya. 49 Utapata adhabu kwa ajili ya uasherati wako na kuchukua matokeo ya dhambi zako za uasherati. Ndipo utakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA Mwenyezi.”

Copyright information for Neno