Ezekiel 25

Unabii Dhidi Ya Amoni

1Neno la BWANA likanijia kusema: 2“Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Waamoni utabiri dhidi yao. 3Waambie, ‘Sikieni neno la BWANA Mwenyezi. Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Kwa sababu ulisema, “Aha!” Juu ya mahali pangu patakatifu palipotiwa unajisi na juu ya nchi ya Israeli ilipoangamizwa na juu ya watu wa Yuda walipokwenda uhamishoni, 4kwa hiyo nitawatia mikononi mwa watu wa mashariki mkawe mali yao. Watapiga kambi zao katikati yenu na kufanya makazi miongoni mwenu, watakula matunda yenu na kunywa maziwa yenu. 5Nitaufanya mji wa Raba kuwa malisho ya ngamia na Amoni kuwa mahali pa kondoo pa kupumzikia. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA. 6Kwa kuwa hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Kwa kuwa umepiga makofi yako na kufanya kishindo kwa miguu, mkifurahia kwa mioyo yenu miovu juu ya yale mabaya yaliyoipata nchi ya Israeli, 7hivyo nitaunyosha mkono wangu dhidi yako na kukutoa kuwa nyara kwa mataifa. Nitakukatilia mbali kutoka kwenye mataifa na kukung'oa katika nchi. Nitakuangamiza, nawe utajua ya kuwa Mimi ndimi BWANA.’ ”

Unabii Dhidi Ya Moabu

8“Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: ‘Kwa sababu Moabu na Seiri wamesema, “Tazama, nyumba ya Yuda imekuwa kama mataifa mengine yote,” 9kwa hiyo nitaiondoa ile miji iliyo kando ya Moabu, kuanzia miji iliyoko mipakani, yaani: Beth-Yeshimothi, Baal-Meoni na Kiriathaimu, iliyo utukufu wa nchi hiyo. 10Nitaitia Moabu pamoja na Waamoni mikononi mwa watu wa Mashariki kuwa milki yao, ili kwamba Waamoni wasikumbukwe miongoni mwa mataifa, 11nami nitatoa adhabu kwa Moabu. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA.’ ”

Unabii Dhidi Ya Edomu

12“Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: ‘Kwa sababu Edomu ulilipiza kisasi juu ya nyumba ya Yuda na kukosa sana kwa kufanya hivyo, 13kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Nitaunyosha mkono wangu dhidi ya Edomu na kuua watu wake na wanyama wao. Nitaufanya ukiwa, kuanzia Temani hadi Dedani wataanguka kwa upanga. 14Nitalipiza Edomu kisasi kwa mkono wa watu wangu Israeli, nao watawatendea Edomu sawasawa na hasira yangu na ghadhabu yangu, nao watakijua kisasi changu, asema BWANA Mwenyezi.’ ”

Unabii Dhidi Ya Ufilisti

15“Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: ‘Kwa sababu Wafilisti wamewalipiza kisasi kwa uovu wa mioyo yao na kwa uadui wa siku nyingi wakataka kuangamiza Yuda, 16kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Mimi ninakaribia kuunyosha mkono wangu dhidi ya Wafilisti, nami nitawakatilia mbali Wakerethi na kuwaangamiza wale waliosalia katika pwani. 17Nitalipiza kisasi kikubwa juu yao na kuwaadhibu katika ghadhabu yangu. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA, nitakapolipiza kisasi juu yao.’ ”

Copyright information for Neno