Ezekiel 34

Wachungaji Na Kondoo

Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, tabiri juu ya wachungaji wa Israeli, tabiri na uwaambie: ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ole wa wachungaji wa Israeli ambao hujitunza wenyewe tu! Je, haiwapasi wachungaji kutunza kundi la kondoo? Mnakula mafuta ya wanyama, mnavaa mavazi ya sufu na kuchinja kondoo walionona, lakini hamlitunzi kundi. Hamkuwatia nguvu walio dhaifu wala hamkuwaganga wenye maradhi wala kuwafunga waliojeruhiwa. Hamkuwarudisha waliotangatanga wala kuwatafuta wale waliopotea. Badala yake mmewatawala kwa ukali na kwa ukatili. Hivyo walitawanyika kwa sababu hapakuwepo mchungaji, nao walipotawanyika, wakawa chakula cha wanyama wa mwitu wote. Kondoo wangu walitawanyika, wakatangatanga kwenye milima yote na kwenye kila kilima kirefu. Kondoo wangu walitawanyika juu ya uso wa dunia yote bila kuwa na ye yote wa kuwaulizia wala wa kuwatafuta.

“ ‘Kwa hiyo, ninyi wachungaji, lisikieni neno la BWANA: Kwa hakika kama niishivyo, asema BWANA Mwenyezi, kwa sababu kondoo zangu wamekosa mchungaji na hivyo wametekwa nyara na kuwa chakula cha wanyama wote wa mwituni na kwa sababu wachungaji wangu, hawakuwatafuta kondoo zangu, bali wachungaji wamejitunza wenyewe, nao hawakuwalisha kondoo zangu, kwa hiyo enyi wachungaji, sikieni neno la BWANA: 10 Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Mimi ni kinyume na wachungaji nami nitawadai kondoo zangu mikononi mwao. Nitawafukuza kutoka kwenye kuchunga kundi langu, ili wachungaji wasiendelee kujitunza wenyewe. Nitaokoa kondoo zangu kutoka kwenye vinywa vyao, nao kondoo hawatakuwa tena chakula chao.

11 “ ‘Kwa kuwa hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Mimi mwenyewe nitawaulizia kondoo zangu na kuwatafuta. 12 Kama vile mchungaji atafutavyo kundi lake lililotawanyika wakati akiwa pamoja nalo, hivyo ndivyo nitakavyowatafuta kondoo wangu. Nitawaokoa kutoka mahali pote walipokuwa wametawanyikia katika siku ya mawingu na giza nene. 13 Nitawatoa katika mataifa na kuwakusanya kutoka nchi mbalimbali, nami nitawaleta katika nchi yao wenyewe. Nitawalisha kwenye milima ya Israeli, katika mabonde na mahali pote panapokalika katika nchi. 14 Nitawachunga kwenye malisho mazuri na miinuko ya mlima wa Israeli patakuwa mahali pao pa malisho. Huko watajipumzisha kwa amani katika nchi ya malisho mazuri, nao watajilisha huko katika malisho tele katika milima ya Israeli. 15 Mimi mwenyewe nitawachunga kondoo zangu na kuwafanya wapumzike, asema BWANA Mwenyezi. 16 Nitawaulizia kondoo waliopotea na kuwaleta walio tangatanga. Nitawafunga waliojeruhiwa na kuwatia nguvu waliodhaifu lakini wale waliojikinai na wenye nguvu nitawaangamiza. Nitalichunga kundi kwa haki.

17 “ ‘Kwa habari yenu, enyi kundi langu, hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Nitahukumu kati ya kondoo na kondoo, kati ya kondoo waume na mbuzi. 18 Je, haiwatoshi ninyi kujilisha kwenye malisho mazuri? Je, ni lazima ninyi kuyakanyaga pia malisho yenu yaliyobaki kwa miguu yenu? Je, haiwatoshi ninyi kunywa maji safi? Je, ni lazima kuyachafua maji mengine kwa miguu yenu? 19 Je, ni lazima kundi langu wajilishe kwa yale mliyoyakanyaga na kunywa maji mliyoyachafua kwa miguu yenu?

20 “ ‘Kwa hiyo, hili ndilo BWANA Mwenyezi awaambialo: Tazama, mimi mwenyewe nitahukumu kati ya kondoo wanono na waliokonda. 21 Kwa sababu mmewapiga kikumbo na kuwapiga kwa pembe zenu kondoo wote walio dhaifu mpaka wakawafukuza, 22 nitaliokoa kundi langu na hawatatekwa nyara tena. Nitahukumu kati ya kondoo na kondoo. 23 Nitaweka juu yao mchungaji mmoja, mtumishi wangu Daudi, naye atawachunga, atawachunga na kuwa mchungaji wao. 24 Mimi BWANA nitakuwa Mungu wao, naye mtumishi wangu Daudi atakuwa mkuu miongoni mwao. Mimi BWANA nimenena.

25 “ ‘Nitafanya nao Agano la amani na kuwaondoa wanyama wa mwitu kutoka katika nchi yao ili kondoo wangu waweze kupumzika nyikani na msituni kwa salama. 26 Nitawabariki wao pamoja na maeneo yanayozunguka kilima changu. Nitawanyeshea mvua kwa majira yake, kutakuwepo mvua za baraka. 27 Miti ya shambani itatoa matunda yake na ardhi itatoa mazao yake, watu watakaa salama katika nchi yao. Watajua kuwa Mimi ndimi BWANA, nitakapovunja vifungo vya nira zao na kuwaokoa kutoka katika mikono ya wale waliowafanya watumwa. 28 Hawatatekwa tena nyara na mataifa, wala wanyama pori hawatawala tena. Wataishi kwa salama, wala hakuna ye yote atakayewatia hofu. 29 Nitawapa nchi yenye sifa kutokana na mazao yake, hawatapatwa na njaa katika nchi tena wala hawatadharauliwa na mataifa. 30 Ndipo watakapojua kuwa Mimi, BWANA, Mungu wao, niko pamoja nao na ya kuwa wao, nyumba ya Israeli, ni watu wangu, asema BWANA Mwenyezi. 31 Ninyi ni kondoo wangu, kondoo wa malisho yangu, ninyi ni watu wangu, nami ni Mungu wenu, asema BWANA Mwenyezi.’ ”

Copyright information for Neno