Ezekiel 35

Unabii Dhidi Ya Edomu

Neno la BWANA likanijia kusema: “Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya mlima Seiri, utabiri dhidi yake na useme: ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Mimi ni kinyume nawe, Ee mlima Seiri, nami nitanyosha mkono wangu dhidi yako na kukufanya ukiwa na usiyekaliwa na watu wala kulimika. Nitaifanya miji yako kuwa magofu nawe utakuwa ukiwa. Ndipo utakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA.

“ ‘Kwa sababu ulificha moyoni uadui wa siku nyingi nawe ukawatoa Waisraeli wauawe kwa upanga wakati wa maafa yao, wakati adhabu yake ilipofikia kilele chake, kwa hiyo hakika kama niishivyo, asema BWANA Mwenyezi, nitakutia katika umwagaji damu nao utakufuatia. Kwa kuwa hakuchukia kumwaga damu, kumwaga damu kutakufuatia. Nitaufanya Mlima Seiri ukiwa na usiokaliwa na watu wala kulimika na kuukatilia mbali na wote wanaokuja na wanaokwenda. Nitaijaza milima yenu kwa watu wake waliouawa, wale waliouawa kwa upanga wataanguka juu ya vilima vyako na katika mabonde yako na katika makorongo yako yote. Nitakufanya ukiwa milele, watu hawataishi katika miji yako. Ndipo utakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA.

10 “ ‘Kwa sababu umesema, “Mataifa haya mawili na nchi hizi zitakuwa zetu nasi tutazimiliki,” ingawa hata mimi BWANA nilikuwa huko, 11 kwa hiyo hakika kama niishivyo, asema BWANA Mwenyezi, nitakutenda kwa kadiri ya hasira na wivu uliouonyesha katika chuki yako juu yao nami nitafanya nijulikane miongoni mwao wakati nitakapokuhukumu. 12 Ndipo utakapojua kuwa Mimi BWANA nimesikia mambo yote ya dharau uliyosema dhidi ya milima ya Israeli. Ulisema, “Wamefanyika ukiwa na kutiwa mikononi mwetu tuwararue.” 13 Ulijigamba dhidi yangu na kusema maneno dhidi yangu bila kujizuia, nami nikayasikia. 14 Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Wakati dunia yote inashangilia nitakufanya ukiwa. 15 Kwa sababu ulishangilia wakati urithi wa nyumba ya Israeli ulipofanyika ukiwa, hivyo ndivyo nitakavyokutendea. Utakuwa ukiwa, Ee mlima Seiri, wewe na Edomu yote. Kisha ndipo watajua kuwa Mimi ndimi BWANA.’ ”

Copyright information for Neno