Ezekiel 36

Unabii Kwa Milima Ya Israeli

“Mwanadamu, itabirie milima ya Israeli na useme, ‘Ee milima ya Israeli, sikieni neno la BWANA. Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Kwa sababu adui wanasema juu yako, “Aha! Mahali palipoinuka pa zamani pamekuwa milki yetu.” ’ Kwa hiyo tabiri na useme, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Kwa sababu wamewafanya ukiwa na kuwagandamiza kila upande ili mpate kuwa milki ya mataifa mengine na kuwa kitu cha kusimangwa na kudhihakiwa miongoni mwa watu, kwa hiyo, Ee milima ya Israeli, sikieni neno la BWANA Mwenyezi: Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo kwa milima na vilima, kwa makorongo na mabonde, kwa mahame yaliyo ukiwa, miji iliyoachwa ambayo imetekwa nyara na kudharauliwa na mataifa mengine yanayowazunguka, hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Katika wivu wangu uwakao nimenena dhidi ya mataifa mengine na dhidi ya Edomu yote, kwa maana kwa furaha na hila katika mioyo yao waliifanya nchi yangu kuwa milki yao ili wapate kuteka nyara sehemu yake ya malisho.’ Kwa hiyo tabiri kuhusu nchi ya Israeli na uiambie milima na vilima, makorongo na vijito na mabonde: ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ninanena katika wivu wa ghadhabu yangu kwa sababu mmedharauliwa na mataifa. Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ninaapa kwa mkono wangu ulioinuliwa kwamba mataifa wanaowazunguka nao pia watadharauliwa.

“ ‘Lakini ninyi, Ee milima ya Israeli, mtatoa matawi na matunda kwa ajili ya watu wangu Israeli, kwa sababu hivi karibuni watakuja nyumbani. Mimi ninawajibika nanyi na nitawaangalia kwa upendeleo, mtalimwa na kupandwa mbegu, 10 nami nitaizidisha idadi ya watu kwenu, naam, nyumba yote ya Israeli. Miji itakaliwa na watu na magofu yatajengwa upya. 11 Nitaongeza idadi ya watu na wanyama juu yenu, nao watazaana sana na kuwa wengi mno. Nitawakalisha watu ndani yenu kama ilivyokuwa wakati uliopita, nami nitawafanya mfanikiwe kuliko hapo kwanza. Ndipo mtakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA. 12 Nitawafanya watu, watu wangu Israeli, kutembea juu yenu. Watawamiliki ninyi, nanyi mtakuwa urithi wao, kamwe hamtawaondolea tena watoto wao.

13 “ ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Kwa sababu watu wanakuambia, “Unawala watu na kuliondolea taifa lako watoto wake,” 14 kwa hiyo hutakula tena watu wala kulifanya tena taifa lako lisiwe na watoto, asema BWANA Mwenyezi. 15 Sitakufanya tena usikie dhihaka za mataifa, wala kudharauliwa na kabila za watu, wala kulifanya taifa lako lianguke, asema BWANA Mwenyezi.’ ”

16 Neno la Mungu likanijia tena, kusema: 17 “Mwanadamu, nyumba ya Israeli walipokuwa wakiishi katika nchi yao wenyewe, waliinajisi kwa mwenendo wao na matendo yao. Mwenendo wao mbele zangu ulikuwa kama mwanamke aliye katika hedhi. 18 Hivyo nilimwaga ghadhabu yangu juu yao kwa sababu walikuwa wamemwaga damu katika nchi na kwa sababu walikuwa wameitia nchi unajisi kwa sanamu zao. 19 Nikawatawanya miongoni mwa mataifa, nao wakaenda huko na huko katika nchi mbalimbali, nikawahukumu sawasawa na mwenendo wao na matendo yao. 20 Tena po pote walipokwenda miongoni mwa mataifa walilitia unajisi Jina langu takatifu, kwa kuwa watu walisema kuhusu wao, ‘Hawa ndio watu wa BWANA, lakini imewapasa kuondoka katika nchi yake.’ 21 Lakini niliwahurumia kwa ajili ya Jina langu takatifu, ambalo nyumba ya Israeli imelitia unajisi miongoni mwa mataifa huko walikokwenda.

22 “Kwa hiyo iambie nyumba ya Israeli, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Si kwa ajili yako, Ee nyumba ya Israeli, kwamba ninafanya mambo haya, bali ni kwa ajili ya Jina langu takatifu, ambalo mmelitia unajisi miongoni mwa mataifa mliyoyaendea. 23 Nitauonyesha utakatifu wa Jina langu kuu, ambalo limetiwa unajisi miongoni mwa mataifa, jina ambalo limetiwa unajisi miongoni mwao. Ndipo mataifa watakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA, asema BWANA Mwenyezi, nitakapojionyesha mwenyewe kuwa mtakatifu kwa kuwapitia ninyi mbele ya macho yao.

24 “ ‘Kwa kuwa nitawaondoa ninyi toka katika mataifa, nitawakusanya kutoka katika nchi zote na kuwarudisha kwenye nchi yenu wenyewe. 25 Nitawanyunyizia maji safi, nanyi mtakuwa safi, nitawatakasa kutoka katika uchafu wenu wote na kutoka katika sanamu zenu zote. 26 Nitawapa moyo mpya na kuweka roho mpya ndani yenu, nitaondoa ndani yenu moyo wenu wa jiwe na kuwapa moyo wa nyama. 27 Nami nitaweka Roho yangu ndani yenu na kuwafanya ninyi mfuate amri zangu na kuwafanya kuwa waangalifu kuzishika sheria zangu. 28 Mtaishi katika nchi niliyowapa baba zenu, ninyi mtakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wenu. 29 Nitawaokoa ninyi kutoka katika unajisi wenu wote. Nitaiita nafaka na kuiongeza iwe nyingi sana nami sitaleta njaa juu yenu. 30 Nitaongeza matunda ya miti na mazao ya mashamba, ili kwamba msipate tena aibu miongoni mwa mataifa kwa ajili ya njaa. 31 Ndipo mtakapozikumbuka njia zenu za uovu na matendo yenu maovu, nanyi mtajichukia wenyewe kwa ajili ya dhambi zote na matendo yenu ya kuchukiza. 32 Ninataka ninyi mjue kwamba sifanyi hili kwa ajili yenu, asema BWANA Mwenyezi. Oneni aibu na mkatahayari kwa ajili ya mwenendo wenu, Ee nyumba ya Israeli!

33 “ ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Siku ile nitakapowasafisha kutoka katika dhambi zenu zote, nitarudisha watu waishi katika miji yenu na magofu yatajengwa upya. 34 Nchi iliyokuwa ukiwa italimwa badala ya kukaa ukiwa machoni mwa wale wote wanaopita ndani yake. 35 Watasema, “Hii nchi iliyokuwa imeachwa ukiwa sasa imekuwa kama bustani ya Edeni, miji ile iliyokuwa magofu, ukiwa na kuangamizwa, sasa imejengewa ngome na kukaliwa na watu.” 36 Ndipo mataifa yanayowazunguka yaliyobakia watakapojua kuwa Mimi BWANA nimejenga tena kile kilichoharibiwa na nimepanda tena kile kilichokuwa ukiwa. Mimi BWANA nimenena, nami nitalifanya.’

37 “Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Mara nyingine tena nitasikia maombi ya nyumba ya Israeli na kuwatendea jambo hili: Nitawafanya watu wake kuwa wengi kama kondoo, 38 kuwa wengi kama kundi la kondoo kwa ajili ya dhabihu huko Yerusalemu wakati wa sikukuu zao za wakati ulioamriwa. Hivyo ndivyo miji iliyokuwa magofu itajazwa na makundi ya watu. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA.”

Copyright information for Neno