Ezekiel 6

Unabii Dhidi Ya Milima Ya Israeli

1Neno la BWANA likanijia kusema, 2“Mwanadamu, elekeza uso wako kukabili milima ya Israeli, utabiri dhidi yake 3na useme: ‘Ee milima ya Israeli, sikia neno la BWANA Mwenyezi. Hili ndilo BWANA Mwenyezi aliambiayo milima na vilima, magenge na mabonde: Ninakaribia kuleta upanga dhidi yenu, nami nitapaharibu mahali penu pote pa juu pa kuabudia miungu. 4Madhabahu zenu zitabomolewa na madhabahu zenu za kufukizia uvumba zitavunjwavunjwa, nami nitawachinja watu wenu mbele ya sanamu zenu. 5Nitazilaza maiti za Waisraeli mbele ya sanamu zao, nami nitatawanya mifupa yenu kuzunguka madhabahu zenu. 6Po pote mnapoishi, miji hiyo itafanywa ukiwa na mahali pa juu pa kuabudia miungu patabomolewa, ili madhabahu zenu zifanywe ukiwa na kuharibiwa, sanamu zenu zitavunjwavunjwa na kuharibiwa, madhabahu zenu za kufukizia uvumba zitabomolewa na kila mlichokifanya kitakatiliwa mbali. 7Watu wenu watachinjwa katikati yenu, nanyi mtatambua Mimi ndimi BWANA.

8“ ‘Lakini nitawabakiza hai baadhi yenu, kwa kuwa baadhi yenu watanusurika kuuawa watakapokuwa wametawanyika katika nchi na mataifa. 9Ndipo katika mataifa ambamo watakuwa wamechukuliwa mateka, wale ambao watanusurika watanikumbuka, jinsi ambavyo nimehuzunishwa na mioyo yao ya uzinzi, ambayo imegeukia mbali nami na macho yao ambayo yametamani sanamu zao. Watajichukia wenyewe kwa ajili ya uovu walioutenda na kwa ajili ya desturi zao za kuchukiza. 10Nao watajua kuwa Mimi ndimi BWANA, sikuwaonya bure kuwa nitaleta maafa hayo yote juu yao.

11“ ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Piga makofi, kanyaga chini kwa mguu na upige kelele, “Ole!” kwa sababu ya maovu yote na machukizo yote yanayofanywa na nyumba ya Israeli, kwa kuwa wataanguka kwa upanga, njaa na tauni. 12Yeye aliye mbali sana atakufa kwa tauni, naye aliye karibu atauawa kwa upanga, naye yule atakayenusurika na kubaki atakufa kwa njaa. Hivyo ndivyo nitakavyotimiza ghadhabu yangu dhidi yao. 13Nao watajua kwamba Mimi ndimi BWANA, wakati maiti za watu wao zitakapokuwa zimelala katikati ya sanamu zao kuzunguka madhabahu zao, juu ya kila kilima kilichoinuka na juu ya vilele vyote vya milima, chini ya kila mti uliotanda na kila mwaloni wenye majani, yaani, sehemu walizofukizia uvumba kwa sanamu zao zote. 14Nami nitanyosha mkono wangu dhidi yao na kuifanya nchi yao ukiwa, kuanzia jangwani hadi Dibla, kila mahali po pote wanapoishi. Ndipo watakapojua ya kwamba Mimi ndimi BWANA.’ ”

Copyright information for Neno