Ezekiel 8

Ibada Ya Sanamu Hekaluni

Katika siku ya tano ya mwezi wa sita mwaka wa sita, baada ya kupelekwa uhamishoni nilipokuwa nimeketi katika nyumba yangu na wazee wa Yuda walikuwa wameketi mbele yangu, mkono wa BWANA Mwenyezi ulikuja juu yangu. Nikatazama, nikaona umbo mfano wa mwanadamu. Kutokana na kile kilichoonekana kuwa kiuno chake kuelekea chini alifanana na moto. Kuanzia kwenye kiuno kuelekea juu sura yake kama chuma king'aavyo kikiwa ndani ya moto. Akanyoosha kitu kilichoonekana kama mkono, akaniinua kwa kushika nywele za kichwa changu. Roho akaniinua juu kati ya nchi na mbingu nikiwa katika maono ya Mungu akanichukua mpaka Yerusalemu, kwenye ingilio la lango la upande wa kaskazini ya ukumbi wa ndani, mahali iliposimama ile sanamu ichocheayo wivu. Hapo mbele yangu palikuwa na utukufu wa Mungu wa Israeli, kama utukufu ule niliouona katika maono kule ua wa ndani.

Kisha akaniambia, “Mwanadamu, tazama kuelekea kaskazini.” Hivyo nikatazama na kwenye ingilio upande wa kaskazini wa lango la madhabahu, nikaona sanamu hii ya wivu.

Ndipo akaniambia, “Mwanadamu, je, unaona yale wanayofanya, haya mambo ya machukizo kabisa nyumba ya Israeli wanayotenda hapa, ambayo yatanifanya niende mbali na mahali pangu patakatifu? Lakini utaona vitu ambavyo vinachukiza zaidi hata kuliko hivi.”

Kisha akanileta mpaka ingilio la ukumbi. Nikatazama, nami nikaona tundu ukutani. Akaniambia, “Mwanadamu, sasa toboa kwenye ukuta huu.” Ndipo nikatoboa ule ukuta, nikaona hapo pana mlango.

Naye akaniambia, “Ingia ndani, ukaone maovu na machukizo wanayofanya humu.” 10 Hivyo nikaingia ndani na kutazama, nikaona kuta zote zimechorwa kila aina ya vitu vitambaavyo na ya wanyama wachukizao wa kila aina na sanamu zote za nyumba ya Israeli. 11 Mbele yao walisimama wazee sabini wa nyumba ya Israeli, naye Yaazania mwana wa Shafani alikuwa amesimama miongoni mwao. Kila mmoja alikuwa na chetezo mkononi na moshi wa harufu nzuri ya uvumba ulikuwa unapanda juu.

12 Akaniambia, “Mwanadamu, umeona wanayoyafanya wazee wa nyumba ya Israeli gizani, kila mmoja kwenye sehemu yake mwenyewe ya kufanyia ibada za sanamu yake? Wao husema, ‘BWANA hatuoni, BWANA ameiacha nchi.’ ” 13 Akasema tena, “Bado utaona machukizo wanayofanya ambayo ni makubwa kuliko haya.”

14 Ndipo akanileta mpaka ingilio la lango la kaskazini la nyumba ya BWANA, nami nikaona wanawake wameketi hapo, wakimwombolezea Tamuzi. 15 Akaniambia, “Unaliona hili, mwanadamu? Utaona vitu ambavyo ni machukizo kuliko hili.”

16 Ndipo akanileta mpaka kwenye ukumbi wa ndani wa nyumba ya BWANA, nako huko katika ingilio la Hekalu, kati ya baraza na madhabahu, walikuwapo wanaume wapatao ishirini na watano. Wakiwa wamelipa kisogo Hekalu la BWANA na kuelekeza nyuso zao upande wa mashariki, wakilisujudia jua huko mashariki.

17 Akaniambia, “Je, umeona hili mwanadamu? Je, ni jambo dogo sana kwa nyumba ya Yuda kufanya machukizo wanayoyafanya hapa? Je, ni lazima pia waijaze nchi dhuluma na kuendelea siku zote kunikasirisha? Watazame wanavyonibania pua kana kwamba ninanuka! 18 Kwa hiyo nitashughulika nao kwa hasira, sitawaonea huruma wala kuwaachilia. Wajapopiga makelele masikioni mwangu, sitawasikiliza.”

Copyright information for Neno