Ezekiel 9

Waabudu Sanamu Wauawa

Kisha nikamsikia akiita kwa sauti kubwa akisema, “Walete wasimamizi wa mji hapa, kila mmoja akiwa na silaha mkononi mwake.” Nami nikaona watu sita wakija toka upande wa lango la juu, linalotazama kaskazini kila mmoja na silaha za kuangamiza mkononi mwake. Pamoja nao alikuwepo mtu aliyekuwa amevaa mavazi ya kitani safi, naye alikuwa na vifaa vya mwandishi akiwa amevishikilia upande mmoja. Wakaingia ndani ya Hekalu wakasimama pembeni mwa madhabahu ya shaba.

Basi utukufu wa Mungu wa Israeli ukaondoka hapo juu ya makerubi, ulikokuwa umekaa, ukaenda kwenye kizingiti cha Hekalu. Ndipo BWANA akamwita yule mtu aliyevaa kitani safi aliyekuwa na vifaa vya mwandishi akiwa amevishikilia upande wake mmoja, akamwambia, “Pita katika mji wote wa Yerusalemu ukaweke alama juu ya vipaji vya nyuso za wale watu wanaohuzunika na kuomboleza kwa sababu ya machukizo yote yanayotendeka katika mji huu.”

Nikiwa ninasikia, akawaambia wale wengine, “Mfuateni anapopita katika mji wote mkiua, pasipo huruma wala masikitiko. Waueni wazee, vijana wa kiume na wa kike, wanawake na watoto, lakini msimguse mtu ye yote mwenye alama. Anzieni katika mahali pangu patakatifu.” Kwa hiyo wakaanza na wale wazee waliokuwa mbele ya Hekalu.

Ndipo akawaambia, “Linajisini Hekalu na mkazijaze kumbi zake maiti za wale waliouawa. Nendeni!” Kwa hiyo wakaenda wakaanza kuua watu mjini kote. Wakati walipokuwa wanaua watu, mimi nilikuwa nimeachwa peke yangu, nikaanguka kifudifudi, nikapiga kelele nikisema, “Ee BWANA Mwenyezi! Je, utaangamiza mabaki yote ya Israeli, katika kumwagwa huku kwa ghadhabu yako juu ya Yerusalemu?”

BWANA akanijibu, “Dhambi ya nyumba ya Israeli na Yuda imekuwa kubwa mno kupita kiasi, nchi imejaa umwagaji damu na mjini kumejaa udhalimu. Kwani wamesema, ‘BWANA ameiacha nchi, BWANA hauoni.’ 10 Kwa hiyo sitawahurumia wala kuwaachilia lakini nitaleta juu ya vichwa vyao, yale waliyoyatenda.”

11 Ndipo mtu yule aliyekuwa amevaa nguo ya kitani safi na vifaa vya mwandishi akiwa amevishikilia upande wake mmoja, akarudi na kutoa taarifa akisema, “Nimefanya kama ulivyoniagiza.”

Copyright information for Neno