Ezekiel 10

Utukufu Unaondoka Hekaluni

1Nikatazama, nikaona juu ya ile nafasi iliyokuwa juu ya vichwa vya wale makerubi kulikuwa na kitu kilichofanana na kiti cha enzi cha yakuti samawati. 2BWANA akamwambia mtu yule aliyekuwa amevaa nguo ya kitani, “Ingia katikati ya yale Magurudumu yaliyo chini ya makerubi. Ukaijaze mikono yako makaa ya mawe ya moto kutoka katikati ya makerubi na uyatawanye juu ya mji.” Nilipokuwa nikiangalia, akaingia ndani.

3Basi wale makerubi walikuwa wamesimama upande wa kusini wa Hekalu wakati yule mtu alipoingia ndani, wingu likaujaza ule ukumbi wa ndani. 4Kisha utukufu wa BWANA ukainuka kutoka juu ya wale makerubi ukaenda kwenye kizingiti cha Hekalu. Wingu likajaza Hekalu, nao ukumbi ukajawa na mng'ao wa utukufu wa BWANA. 5Sauti ya mabawa ya wale makerubi ingeweza kusikika mpaka kwenye ukumbi wa nje, kama sauti ya Mungu Mwenyezi
10:5 Mungu Mwenyezi hapa ina maana ya El-Shaddai kwa Kiebrania
wakati anapoongea.

6BWANA alipomwamuru yule mtu aliyevaa nguo za kitani akisema, “Chukua moto toka katikati ya magurudumu, kutoka katikati ya makerubi,” yule mtu aliingia ndani akasimama pembeni mwa gurudumu. 7Ndipo mmoja wa wale makerubi akanyoosha mkono wake kwenye moto uliokuwa katikati yao. Akachukua baadhi ya moto na kuutia mikononi mwa yule mtu aliyevaa mavazi ya kitani, naye akaupokea akatoka nje. 8(Chini ya mabawa ya makerubi paliweza kuonekana kitu kilichofanana na mikono ya mwanadamu.)

9Nikatazama, nikaona magurudumu manne pembeni mwa makerubi, moja pembeni mwa kila kerubi. Magurudumu hayo yalimetameta kama jiwe la zabarajadi. 10Kule kuonekana kwake, yote manne yalifanana kila gurudumu lilikuwa kama linazunguka ndani ya lingine. 11Yalipozunguka, yalikwenda kokote katika pande nne walikoelekea wale makerubi. Magurudumu hayakugeuka wakati makerubi yalipokwenda. Makerubi walikwenda upande wo wote kichwa kilikoelekea pasipo kugeuka walipokuwa wakienda. 12Miili yao yote, pamoja na migongo yao, mikono na mabawa yao yote yalikuwa yamejaa macho kabisa kama yalivyokuwa yale magurudumu yao manne. 13Nikasikia magurudumu yakiitwa, “Magurudumu ya kisulisuli.” 14Kila mmoja wa wale makerubi alikuwa na nyuso nne: Uso mmoja ulikuwa kama vile wa kerubi, uso wa pili ulikuwa wa mwanadamu, uso wa tatu ulikuwa wa simba na uso wa nne ulikuwa wa tai.

15Kisha makerubi wakapaa juu. Hawa ndio wale viumbe walio hai niliowaona kando ya Mto Kebari. 16Wakati makerubi walipokwenda, magurudumu yaliyoko kando yao yalikwenda na wakati makerubi walipotanda mabawa yao wapate kupaa juu kutoka katika ardhi, magurudumu yale hayakuondoka pembeni mwao. 17Makerubi yaliposimama kimya, nayo pia yalitulia kimya, nao makerubi yalipoinuka juu, magurudumu nayo yaliinuka juu pamoja nao, kwa sababu roho ya vile viumbe hai ilikuwa ndani yake.

18Kisha utukufu wa Mungu ukaondoka pale kwenye kizingiti cha Hekalu na kusimama juu ya wale makerubi. 19Nilipokuwa nikitazama, makerubi yakatanda mabawa yao na kuinuka kutoka ardhini, nao walipokuwa wakienda yale magurudumu yakaenda pamoja nao. Wakasimama kwenye ingilio la lango la mashariki la nyumba ya BWANA, nao utukufu wa Mungu wa Israeli ukawa juu yao.

20Hawa walikuwa ndio viumbe hai niliokuwa nimewaona chini ya Mungu wa Israeli kando ya Mto Kebari, nami nikatambua ya kuwa hao walikuwa makerubi. 21Kila mmoja alikuwa na nyuso nne, mabawa manne, chini ya mabawa yao kulikuwa na kile kilichoonekana kama mikono ya mwanadamu. 22Nyuso zao zilifanana kama zile nilizokuwa nimeziona kando ya Mto Kebari. Kila mmoja alikwenda mbele moja kwa moja.

Copyright information for Neno