Ezekiel 11

Hukumu Juu Ya Viongozi Wa Israeli

1Ndipo Roho akaniinua na kunileta mpaka kwenye lango la nyumba ya BWANA linalotazama upande wa mashariki. Pale kwenye ingilio la lango kulikuwepo wanaume ishirini na watano, nami nikaona miongoni mwao Yaazania mwana wa Azuri na Pelatia mwana wa Benaya, viongozi wa watu. 2BWANA akaniambia, “Mwanadamu, hawa ndio wafanyao hila na kutoa mashauri potovu katika mji huu. 3Wao husema, ‘Je, hivi karibuni hautakuwa wakati wa kujenga nyumba? Mji huu ni chungu cha kupikia, nasi ndio nyama.’ 4Kwa hiyo toa unabii dhidi yao, tabiri, Ewe mwanadamu.”

5Kisha Roho wa BWANA akaja juu yangu, naye akaniambia niseme: “Hili ndilo BWANA asemalo: Hili ndilo ninyi mnalosema, Ee nyumba ya Israeli, lakini ninajua mnalowaza mioyoni mwenu. 6Mmewaua watu wengi katika mji huu na kujaza barabara zake maiti.

7“Kwa hiyo hili ndilo asemalo BWANA Mwenyezi: maiti ulizozitupa huko ni nyama na mji huu ni chungu, lakini nitawaondoa mtoke huko. 8Mnaogopa upanga, nao upanga huo ndio nitakaouleta juu yenu, asema BWANA Mwenyezi. 9Nitawaondoa mtoke katika mji na kuwatia mikononi mwa wageni nami nitawaadhibu. 10Mtaanguka kwa upanga, nami nitatimiza hukumu dhidi yenu katika mipaka ya Israeli. Ndipo mtajua kuwa Mimi ndimi BWANA. 11Mji huu hautakuwa chungu kwa ajili yenu, wala hamtakuwa nyama ndani yake. Nitatoa hukumu dhidi yenu katika mipaka ya Israeli. 12Nanyi mtajua ya kuwa Mimi ndimi BWANA, kwa kuwa hamkufuata amri zangu wala kuzishika sheria zangu, bali mmefuata mwenendo wa mataifa yanayowazunguka.”

13Basi nilipokuwa ninatoa unabii, Pelatia mwana wa Benaya akafa. Ndipo nikaanguka kifudifudi, nikalia kwa sauti kuu nikasema, “Ee BWANA Mwenyezi! Je utaangamiza kabisa mabaki ya Israeli?”

14Neno la BWANA likanijia kusema: 15“Mwanadamu, ndugu zako, ndugu zako ambao ni wa uhusiano wa damu na nyumba yote ya Israeli, ndio wale ambao watu wa Yerusalemu wamesema, ‘Wako mbali na BWANA; nchi hii tulipewa sisi kuwa milki yetu.’

Ahadi Ya Kurudi Kwa Israeli

16“Kwa hiyo sema, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ingawa niliwapeleka mbali miongoni mwa mataifa na kuwatawanya katika nchi mbali-mbali, lakini kwa kitambo kidogo mimi nimekuwa mahali patakatifu kwao katika nchi walizokwenda.’

17“Kwa hiyo sema: ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Nitawakusanyeni kutoka katika mataifa na kuwarudisha kutoka katika nchi ambazo mmetawanywa, nami nitawarudishia nchi ya Israeli.’

18“Watairudia nchi na kuondoa vinyago vyote vya upotovu na sanamu zote za machukizo. 19Nitawapa moyo mmoja na kuweka roho mpya ndani yao, nitaondoa kutoka ndani yao moyo wa jiwe na kuwapa moyo wa nyama. 20Kisha watafuata amri zangu na kuwa waangalifu kutii sheria zangu. Watakuwa watu wangu nami nitakuwa Mungu wao. 21Lakini kwa wale ambao mioyo yao imeambatana na vinyago vyao vya upotovu na sanamu zao za machukizo, nitaleta juu ya vichwa vyao yale waliyotenda asema BWANA Mwenyezi.”

22Ndipo wale makerubi, wenye magurudumu pembeni mwao, wakakunjua mabawa yao, nao utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwa juu yao. 23Basi utukufu wa BWANA ukapaa juu kutoka katika mji, ukatua juu ya mlima ulio upande wa mashariki ya mji. 24Roho akaniinua na kunileta mpaka kwa watu wa uhamisho huko Ukaldayo nikiwa katika yale maono niliyopewa na Roho wa Mungu.

Ndipo maono niliyokuwa nimeyaona yakanitoka,
25nami nikawaeleza wale watu wa uhamisho kila kitu BWANA alichokuwa amenionyesha.

Copyright information for Neno