Ezekiel 27

Maombolezo Kwa Ajili Ya Tiro

1Neno la BWANA likanijia kusema: 2“Mwanadamu, fanya maombolezo kwa ajili ya Tiro. 3Umwambie Tiro, ulioko kwenye lango la bahari, ufanyao biashara na mataifa mengi ya pwani, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “ ‘Ee Tiro, wewe umesema,
“Mimi ni mkamilifu katika uzuri.”
4Mipaka yako ilikuwa katika moyo wa bahari,
wajenzi wako walikamilisha uzuri wako.
5Walizifanya mbao zako zote
kwa misonobari itokayo Seniri
27:5 Yaani Hermoni
;
walichukua mierezi kutoka Lebanoni
kukutengenezea mlingoti.
6Walichukua mialoni toka Bashani
wakakutengenezea makasia yako;
kwa miti ya msanduku
kutoka pwani ya Kitimu
wakatengeneza sitaha yako
na kuipamba kwa pembe za ndovu.
7Kitani safi kilichotariziwa kutoka Misri kilikuwa tanga lako,
nacho kilikuwa bendera yako;
chandarua chako kilikuwa cha rangi ya buluu na ya zambarau
kutoka visiwa vya Elisha.
8Watu kutoka Sidoni na Arvadi walikuwa wapiga makasia yako;
watu wako wenye ustadi, Ee Tiro,
walikuwa ndio mabaharia wako.
9Wazee wa Gebali
27:9 Yaani Bubilo, mji wa zamani sana wa Ufoinike (kama kilomita 80 kaskazini mwa Beiruti)
pamoja na mafundi stadi
walikuwa mafundi wako melini.
Meli zote za baharini na mabaharia wao
walikuja kwako ili kubadilishana bidhaa zako.
10“ ‘Watu wa Uajemi, Ludi na Putu
walikuwa askari katika jeshi lako.
Walitundika ngao zao na chapeo zao kwenye kuta zako,
wakileta fahari yako.
11Watu wa Arvadi na wa Heleki
walikuwa juu ya kuta zako pande zote;
watu wa Gamadi
walikuwa kwenye minara yako.
Walitundika ngao zao kuzizunguka kuta zako;
wakaukamilisha uzuri wako.12“ ‘Tarshishi walifanya biashara nawe kwa sababu ya utajiri wako mkubwa wa bidhaa, walibadilisha fedha, chuma, bati na risasi kwa mali zako.

13“ ‘Uyunani, Tubali na Mesheki, walifanya biashara nawe, walibadilisha watumwa na vyombo vya shaba kwa bidhaa zako.

14“ ‘Watu wa Beth-Togarma walibadilisha farasi wa mizigo, farasi wa vita na nyumbu kwa mali zako.

15“ ‘Watu wa Dedani
27.15 Yaani Rhodesi
walifanya biashara nawe, watu wengi wa nchi za pwani walikuwa wachuuzi wako, walikulipa kwa pembe za ndovu na mpingo.

16“ ‘Watu wa Edomu
27:16 Au: Aramu
walifanya biashara nawe kwa ajili ya wingi wa kazi za mikono yako, walibadilishana kwa almasi, vitambaa vya rangi ya zambarau, vitambaa vilivyotariziwa, kitani safi, matumbawe na akiki nyekundu.

17“ ‘Yuda na Israeli walifanya biashara nawe, walibadilishana kwa ngano kutoka Minithi, mtama, asali, mafuta na marhamu ya kuponyeshea.

18“ ‘Dameski, kwa sababu ya wingi wa kazi za mikono yako na ukuu wa utajiri wa mali, walifanya biashara nawe wakibadilishana mvinyo kutoka Helboni na sufu kutoka Zahari.

19“ ‘Wadani na Wayunani kutoka Uzali, walikuletea mali za biashara, nao wakabadilishana nawe chuma kilichofuliwa, mdalasini na mchaichai.

20“ ‘Dedani alifanya biashara nawe kwa matandiko ya farasi.

21“ ‘Arabia na wakuu wote wa Kedari walikuwa wanunuzi wako waliobadilishana bidhaa zako na wana-kondoo, kondoo waume na mbuzi.

22“ ‘Wafanya biashara wa Sheba na wa Rama walifanya biashara nawe, walibadilishana bidhaa zako na aina zote za vikolezi, vito vya thamani na dhahabu.

23“ ‘Harani, Kane na Edeni na wafanyabiashara wa Sheba, Ashuru na Kilmadi walifanya biashara nawe. 24Kwenye soko lako, walifanya biashara nawe kwa mavazi mazuri, vitambaa vya buluu, nguo za kutariziwa na mazulia ya rangi mbalimbali yenye kamba zilizosokotwa na kuwekwa mafundo imara. 25“ ‘Merikebu za Tarshishi ndizo
zinazokusafirishia bidhaa zako.
Umejazwa shehena kubwa
katika moyo wa bahari.
26Wapiga makasia wako wanakupeleka
mpaka kwenye maji makavu.
Lakini upepo wa mashariki umekuvunja vipande vipande
katika moyo wa bahari.
27Utajiri wako, bidhaa zako na mali zako,
mabaharia wako, manahodha wako,
mafundi wako wa meli,
wafanyabiashara wako na askari wako wote,
na kila mmoja aliyeko melini
atazama kwenye moyo wa bahari
siku ile ya kuvunjika kwa meli yako.
28Nchi za pwani zitatetemeka
wakati mabaharia wako watakapopiga kelele.
29Wote wapigao makasia
wataacha meli zao,
mabaharia wote na wanamaji wote
watasimama pwani.
30Watapaza sauti zao
na kulia sana kwa ajili yako;
watajitupia mavumbi juu ya vichwa vyao
na kujivingirisha kwenye majivu.
31Watanyoa nywele zao kwa ajili yako,
nao watavaa nguo za magunia.
Watakulilia kwa uchungu wa moyo
na kwa maombolezo makuu.
32Watakapokuwa wanalia na kuomboleza juu yako,
watafanya maombolezo kukuhusu wakisema:
“Ni nani aliyepata kuangamizwa kama Tiro,
katika moyo wa bahari?”
33Wakati bidhaa zako zilipotoka baharini,
ulitosheleza mataifa mengi;
kwa wingi wa utajiri wako na bidhaa zako
ulitajirisha wafalme wa dunia.
34Sasa umevunjwavunjwa na bahari,
katika vilindi vya maji,
bidhaa zako na kundi lako lote
vimezama pamoja nawe.
35Wote waishio katika nchi za pwani
wanakustaajabia;
wafalme wao wanatetemeka kwa hofu kuu,
nazo nyuso zao zimekunjamana kwa woga.
36Wafanya biashara miongoni mwa mataifa wanakucheka;
umefikia mwisho wa kutisha
nawe hutakuwepo tena.’ ”


Copyright information for Neno