Ezekiel 29

Unabii Dhidi Ya Misri

1Katika mwaka wa kumi, mwezi wa kumi, siku ya kumi na mbili, neno la BWANA likanijia kusema: 2“Mwanadamu, elekeza uso wako juu ya Farao mfalme wa Misri na utabiri dhidi yake na dhidi ya Misri yote. 3Nena, nawe useme: ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: “ ‘Mimi ni kinyume nawe, Farao, mfalme wa Misri,
joka kubwa ulalaye katikati ya vijito vyako.
Unasema, “Mto Nile ni wangu mwenyewe;
niliufanya kwa ajili yangu mwenyewe.”
4Lakini nitatia ndoana katika mataya yako
nami nitawafanya samaki wa vijito vyako
washikamane na magamba yako.
Nitakutoa katikati ya vijito vyako,
pamoja na samaki wote
walioshikamana na magamba yako.
5Nitakutupa jangwani,
wewe pamoja na samaki wote wa vijito vyako.
Utaanguka uwanjani,
nawe hutakusanywa au kuchukuliwa.
Nitakutoa uwe chakula
kwa wanyama wa nchi
na ndege wa angani.6Ndipo wale wote waishio Misri watakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA.

“ ‘Umekuwa fimbo ya tete kwa nyumba ya Israeli.
7Walipokushika kwa mikono yao, ulivunjika na kuchana mabega yao, walipokuegemea, ulivunjika na migongo yao ikateguka.

8“ ‘Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Nitaleta upanga juu yako na kuua watu wako na wanyama wao. 9Misri itakuwa ukiwa na isiyolimwa wala kukaliwa na watu. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA.

“ ‘Kwa sababu ulisema, “Mto Nile ni wangu; mimi niliufanya,”
10kwa hiyo mimi ni kinyume nawe na kinyume na vijito vyako, nami nitaifanya nchi ya Misri kuwa magofu na ukiwa isiyolimwa wala kukaliwa na watu kuanzia Migdoli hadi Aswani, hata kufikia mpakani wa Ethiopia. 11Hakuna unyayo wa mtu au mnyama utakaopita ndani yake, wala hakuna ye yote atakayeishi humo kwa muda wa miaka arobaini. 12Nitaifanya nchi ya Misri ukiwa, miongoni mwa nchi zilizo ukiwa, nayo miji yake itabaki ukiwa miaka arobaini miongoni mwa miji iliyo magofu. Nami nitawatawanya Wamisri miongoni mwa mataifa na kuwafukuza huko na huko katika nchi nyingine.

13“ ‘Lakini hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Mwishoni mwa hiyo miaka arobaini, nitawakusanya Wamisri kutoka katika mataifa walikotawanywa. 14Nitawarudisha kutoka kwenye kutekwa kwao na kuwaweka katika Pathrosi
29:14 Pathrosi ni Misri ya Juu
, nchi ya baba zao. Huko watakuwa na ufalme usiokuwa na nguvu.
15Utakuwa ufalme dhaifu kuliko zote na kamwe Misri haitajikweza tena juu ya mataifa mengine. Nitaufanya ufalme wake dhaifu sana kiasi kwamba kamwe hautatawala tena juu ya mataifa mengine. 16Misri haitakuwa tena tumaini la watu wa Israeli bali itakuwa kumbukumbu ya dhambi yao kwa kuigeukia kuomba msaada. Ndipo watakapojua kuwa Mimi ndimi BWANA Mwenyezi.’ ”

17Katika mwaka wa ishirini na saba, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza, neno la BWANA likanijia, kusema: 18“Mwanadamu, Nebukadneza mfalme wa Babeli aliongoza jeshi lake kufanya kazi ngumu dhidi ya Tiro; kila kichwa kilipata upaa na kila bega likachunika. Lakini yeye na jeshi lake hawakupata malipo yo yote kutokana na muda wote alioongoza hiyo vita dhidi ya Tiro. 19Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Nitaitia Misri mikononi mwa Nebukadneza mfalme wa Babeli, naye atachukua utajiri wa Misri. Atateka mateka na kuchukua nyara mali za Misri kama ujira kwa ajili ya jeshi lake. 20Nimempa mfalme wa Babeli nchi ya Misri kuwa ujira kwa juhudi zake kwa sababu yeye na jeshi lake walifanya kwa ajili yangu, asema BWANA Mwenyezi.

21“Katika siku hiyo nitaifanya nyumba ya Israeli iwe na nguvu nami nitakifungua kinywa chako miongoni mwao. Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi BWANA.”

Copyright information for Neno