Ezekiel 3

1Naye akaniambia, “Mwanadamu, kula kile kilichoko mbele yako, kula huu ukurasa wa kitabu, kisha uende ukaseme na nyumba ya Israeli.” 2Ndipo nikafungua kinywa changu, naye akanilisha ule ukurasa wa kitabu.

3Ndipo akaniambia, “Mwanadamu, kula ukurasa huu wa kitabu ninaokupa ujaze tumbo lako.” Kwa hiyo nikaula, ulikuwa mtamu kama asali kinywani mwangu.

4Kisha akaniambia, “Mwanadamu, sasa nenda katika nyumba ya Israeli ukaseme nao maneno yangu. 5Hukutumwa kwa taifa lenye maneno ya kutatiza na lugha ngumu, bali kwa nyumba ya Israeli. 6Sikukutuma kwa mataifa mengi yenye maneno ya kutatiza na lugha ngumu ambao maneno yao hutayaelewa. Hakika ningekutuma kwa watu hao, wangekusikiliza. 7Lakini nyumba ya Israeli haitakusikiliza kwa kuwa hawako radhi kunisikiliza mimi, kwa kuwa nyumba yote ya Israeli ni wenye vipaji vya nyuso vigumu na mioyo ya ukaidi. 8Tazama nimefanya uso wako mgumu dhidi ya nyuso zao na kipaji cha uso wako kigumu dhidi ya vipaji vya nyuso zao. 9Kama vile almasi ilivyo ngumu kuliko gumegume, ndivyo nilivyokifanya kipaji cha uso wako. Usiwaogope wala usiwahofu, wajapokuwa ni nyumba ya kuasi.”

10Naye akaniambia, “Mwanadamu, sikiliza kwa makini na uyatie moyoni mwako maneno yote nitakayosema nawe. 11Kisha nenda kwa watu wa taifa lako walio uhamishoni, ukaseme nao. Waambie, ‘Hivi ndivyo BWANA Mwenyezi asemavyo,’ kwamba watasikiliza au hawatasikiliza.”

12Ndipo Roho akaniinua, nikasikia sauti kubwa nyuma yangu ya ngurumo. (Utukufu wa BWANA na utukuzwe katika mahali pa makao yake!) 13Ilikuwa ni sauti ya mabawa ya wale viumbe hai yakisuguana moja kwa jingine, sauti kama ya ngurumo. 14Ndipo Roho aliponiinua na kunipeleka mbali. Nikaenda nikiwa na uchungu na hasira moyoni mwangu, nao mkono wa BWANA ukiwa juu yangu. 15Nikafika kwa wale watu waliokuwa uhamishoni huko Tel-Abibu karibu na Mto Kebari. Nikakaa miongoni mwao kwa muda wa siku saba, nikiwa nimejawa na mshangao.

Onyo Kwa Israeli

16Mwishoni mwa hizo siku saba neno la BWANA likanijia kusema: 17“Mwanadamu, nimekufanya uwe mlinzi wa nyumba ya Israeli, kwa hiyo sikia neno nisemalo, ukawape onyo litokalo kwangu. 18Nimwambiapo mtu mwovu, ‘Hakika utakufa,’ na wewe usipomwonya mtu huyo au kumshauri aache njia zake mbaya ili kuokoa maisha yake, huyo mtu mwovu atakufa katika dhambi yake na damu yake nitaidai mkononi mwako. 19Lakini ukimwonya mtu mwovu naye akakataa kuacha uovu wake na njia zake mbaya, atakufa katika dhambi yake, lakini wewe utakuwa umejiokoa nafsi yako.

20“Tena, mtu mwenye haki akiacha haki yake na kutenda maovu, nami nikaweka kikwazo mbele yake mtu huyo atakufa. Kwa kuwa hukumwonya, atakufa katika dhambi yake. Mambo ya haki aliyotenda, hayatakumbukwa, damu yake nitaidai mkononi mwako. 21Lakini ukimwonya mwenye haki asitende dhambi na akaacha kutenda dhambi, hakika ataishi kwa sababu alipokea maonyo na utakuwa umejiokoa nafsi yako.”

22Mkono wa BWANA ulikuwa juu yangu huko, naye akaniambia, “Simama uende mpaka sehemu tambarare, nami nitasema nawe huko.” 23Kwa hiyo niliinuka nikaenda mpaka mahali pa tambarare. Utukufu wa BWANA ulikuwa umesimama huko, kama utukufu ule niliouona kando ya Mto Kebari, nami nikaanguka kifudifudi.

24Ndipo Roho akaja ndani yangu akanisimamisha kwa miguu yangu. Akasema nami akaniambia: “Nenda ukajifungie ndani ya nyumba yako. 25Nawe, Ee mwanadamu, watakufunga kwa kamba, watakufunga ili usiweze kutoka na kuwaendea watu. 26Nitaufanya ulimi wako ushikamane kwenye kaa la kinywa chako, ili uwe kimya usiweze kuwakemea, wajapokuwa ni nyumba ya kuasi. 27Lakini nitakaposema nawe, nitafungua kinywa chako nawe utawaambia, ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo.’ Ye yote atakayesikiliza na asikilize, na ye yote atakayekataa na akatae; kwa kuwa wao ni nyumba ya kuasi.

Copyright information for Neno