Ezekiel 39

Majeshi Ya Gogu Yataangamizwa

1“Mwanadamu, tabiri dhidi ya Gogu useme: ‘Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ee Gogu mimi ni kinyume nawe, mtawala mkuu wa Roshi, Mesheki na Tubali. 2Nitakugeuza kuelekea ulikotoka na kukuburuta. Nitakuleta kutoka kaskazini ya mbali na kukupeleka wewe dhidi ya milima ya Israeli. 3Kisha nitaupiga upindi wako kutoka mkono wako wa kushoto na kuifanya mishale ianguke kutoka mkono wako wa kuume. 4Utaanguka kwenye milima ya Israeli, wewe pamoja na vikosi vyako vyote na yale mataifa yaliyo pamoja nawe. Nitakutoa uwe chakula cha ndege wa aina zote walao nyama na cha wanyama wa mwituni. 5Utaanguka katika uwanja, kwa kuwa nimenena, asema BWANA Mwenyezi. 6Nitatuma moto juu ya Magogu na kwa wale wanaoishi kwa salama huko pwani, nao watajua kwamba Mimi ndimi BWANA.

7“ ‘Nitalifanya Jina langu takatifu lijulikane miongoni mwa watu wangu Israeli. Sitaliacha tena Jina langu takatifu litiwe unajisi, nayo mataifa watajua kuwa Mimi BWANA ndimi niliye Mtakatifu wa Israeli. 8Hili jambo linakuja! Hakika litatokea, asema BWANA Mwenyezi. Hii ndiyo siku ile niliyosema habari zake.

9“ ‘Ndipo wale wanaoishi katika miji ya Israeli watakapotoka na kutumia hizo silaha kuwashia moto na kuziteketeza, yaani, kigao na ngao, pinde na mishale, rungu za vita na mikuki. Kwa miaka saba watavitumia kama kuni. 10Hawatahitaji kukusanya kuni kutoka mashambani wala kukata kuni kutoka kwenye misitu, kwa sababu watatumia silaha kuwa kuni. Nao watawateka mateka wale waliowateka na kuchukua nyara mali za wale waliochukua mali zao nyara, asema BWANA Mwenyezi.

11“ ‘Siku ile nitampa Gogu mahali pa kuzikia katika Israeli, katika bonde la wale wasafirio upande wa mashariki kuelekea baharini. Jambo hili litazuia njia ya wasafiri kwa sababu Gogu na makundi yake yote ya wajeuri watazikwa huko. Kwa hiyo litaitwa Bonde la Hamon-Gogu
39.11 Hamon-Gogu maana yake Makundi ya wajeuri wa Gogu
.

12“ ‘Kwa miezi saba nyumba ya Israeli itakuwa ikiwazika ili kuisafisha nchi. 13Watu wote wa nchi watawazika, nayo siku nitakayotukuzwa itakuwa siku ya kumbukumbu kwa ajili yao, asema BWANA Mwenyezi.

14“ ‘Watu wataajiriwa mara kwa mara kuisafisha nchi. Baadhi yao watapita nchini kote na zaidi yao hao wengine, watawazika wale waliosalia juu ya uso wa nchi. Mwisho wa hiyo miezi saba wataanza upekuzi wao. 15Wakati wanapopita nchini kote na mmoja wao akaona mfupa wa mwanadamu, ataweka alama kando yake mpaka wachimba kaburi wawe wameuzika katika Bonde la Hamon-Gogu. 16(Pia mji uitwao Hamona
39.16 Hamona maana yake Kundi (la wajeuri)
utakuwa humo.) Hivyo ndivyo watakavyoisafisha nchi.’

17“Mwanadamu, hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ita kila aina ya ndege na wanyama wote wa mwituni, waambie: ‘Kusanyikeni mje pamoja kutoka pande zote kwa ajili ya dhabihu ninayowaandalia, dhabihu kuu katika milima ya Israeli. Huko mtakula nyama na kunywa damu. 18Mtakula nyama za watu mashujaa na kunywa damu za wakuu wa dunia kana kwamba ni za kondoo waume na kondoo wake, mbuzi na mafahali, wote walionona kutoka Bashani. 19Katika dhabihu ninayoandaa kwa ajili yenu, mtakula mafuta mpaka mkinai na kunywa damu mpaka mlewe. 20Kwenye meza yangu watajishibisha kwa farasi na wapanda farasi, watu mashujaa na maaskari wa kila aina,’ asema BWANA Mwenyezi.

21“Nitauonyesha utukufu wangu miongoni mwa mataifa, nayo mataifa yote wataiona adhabu nitakayotoa na mkono wangu nitakaouweka juu yao. 22Kuanzia siku ile na kuendelea nyumba ya Israeli itajua kuwa Mimi ndimi BWANA, Mungu wao. 23Na mataifa watajua kuwa nyumba ya Israeli walikwenda utumwani kwa ajili ya dhambi yao, kwa sababu hawakuwa waaminifu kwangu. Hivyo niliwaficha uso wangu na kuwatia mikononi mwa adui zao, nao wote wakaanguka kwa upanga. 24Niliwatendea sawasawa na uchafu wao na makosa yao, nami nikawaficha uso wangu.

25“Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Sasa nitamrudisha Yakobo kutoka utumwani, nami nitawahurumia watu wote wa Israeli, nami nitakuwa na wivu kwa ajili ya Jina langu takatifu. 26Wataisahau aibu yao na jinsi walivyoonyesha kutokuwa waaminifu kwangu wakati walipoishi kwa salama katika nchi yao, bila kuwa na mtu ye yote wa kuwatia hofu. 27Nitakapokuwa nimewarudisha kutoka katika mataifa na kuwakusanya kutoka katika nchi za adui zao, mimi nitajionyesha kuwa mtakatifu kwa kupitia kwao machoni mwa mataifa mengi. 28Ndipo watakapojua kwamba Mimi ndimi BWANA, Mungu wao, ingawa niliwapeleka uhamishoni miongoni mwa mataifa, nitawakusanya tena katika nchi yao wenyewe, bila kumwacha ye yote nyuma. 29Sitawaficha tena uso wangu, kwa maana nitamimina Roho wangu juu ya nyumba ya Israeli, asema BWANA Mwenyezi.”

Copyright information for Neno