Ezekiel 40

Eneo La Hekalu Jipya

1Katika mwaka wa ishirini na tano wa uhamisho wetu, mwanzoni mwa huo mwaka, siku ya kumi ya mwezi, katika mwaka wa kumi na nne baada ya kuanguka kwa mji, siku hiyo hiyo mkono wa BWANA ulikuwa juu yangu, naye akanipeleka huko. 2Nikiwa katika maono ya Mungu alinichukua mpaka nchi ya Israeli, naye akaniweka kwenye mlima mrefu sana, ambako upande wa kusini kulikuwepo baadhi ya majengo ambayo yalionekana kama mji. 3Akanipeleka huko, nami nikamwona mtu ambaye kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwa shaba. Alikuwa amesimama kwenye lango akiwa na kamba ya kitani na ufito wa kupimia mkononi mwake. 4Mtu huyo akaniambia, “Mwanadamu, angalia kwa macho yako na usikie kwa masikio yako nawe uzingatie kitu nitakachokuonyesha, kwa kuwa ndiyo sababu umeletwa hapa. Iambie nyumba ya Israeli kila kitu utakachoona.”

Lango La Mashariki Kuelekea Ukumbi Wa Nje

5Nikaona ukuta uliozunguka eneo lote la Hekalu. Ule ufito wa kupimia uliokuwa mkononi mwa yule mtu ulikuwa na urefu wa dhiraa ndefu sita
40.5 Dhiraa ndefu 6 ni sawa na mita 3.18
, yaani, dhiraa ndefu ni sawa na dhiraa na nyanda nne, akapima ule ukuta. Ukuta huo ulikuwa na unene wa dhiraa ndefu sita na kimo cha dhiraa ndefu sita.

6Kisha akaenda kwenye lango linaloelekea mashariki. Akapanda ngazi zake akapima kizingiti cha lango, nacho kilikuwa na kina cha huo ufito. 7Vyumba vya kupumzikia vya walinzi vilikuwa na urefu wa huo ufito mmoja na upana wa huo ufito, kuta zilizogawa vyumba hivyo vya mapumziko zilikuwa na unene wa dhiraa tano
40.7 Dhiraa 5 ni sawa na mita 2.25
. Nacho kizingiti cha lango lililokuwa karibu na ukumbi unaoelekea hekaluni ulikuwa na kina cha huo ufito.

8Kisha akapima baraza ya njia ya lango, 9ambayo ilikuwa na kina cha dhiraa nane
40.9 Dhiraa 8 ni sawa na mita 3.6
na miimo yake ilikuwa na unene wa dhiraa mbili
40.9 Dhiraa 2 ni sawa na sentimita 90
. Baraza ya lango ilielekea Hekalu.

10Ndani ya lango la mashariki kulikuwepo vyumba vitatu vya kupumzikia kila upande, vyote vitatu vilikuwa na vipimo vilivyo sawa, nazo nyuso za kuta zilizotenganisha kila upande zilikuwa na vipimo vilivyo sawa. 11Kisha akapima upana wa ingilio la lango, ilikuwa dhiraa kumi na urefu wake ulikuwa dhiraa kumi na tatu. 12Mbele ya kila chumba cha kupumzikia kulikuwepo ukuta uliokuwa na kimo cha dhiraa moja
40.12 Dhiraa 1 ni sawa na sentimita 45
kwenda juu, navyo hivyo vyumba vilikuwa dhiraa sita mraba.
13Kisha akapima njia ya lango kuanzia juu ya ukuta wa nyuma wa chumba kimoja cha kupumzikia hadi juu ya ukuta wa nyuma wa chumba upande wa pili kukawa na nafasi ya dhiraa ishirini na tano, kuanzia ukuta mmoja hadi mwingine. 14Akapima pia ukumbi, urefu wa dhiraa ishirini
40.14 Dhiraa 20 ni sawa na mita 9
na lango linalofuatia hiyo nguzo kila upande wa huo ukumbi.
15Umbali kuanzia ingilio la njia ya lango hadi mwisho kabisa wa baraza yake ulikuwa dhiraa hamsini
40.15 Dhiraa 50 ni sawa na mita 22.5
.
16Kulikuwa na vidirisha kwenye hivyo vyumba vya walinzi na nguzo za hivyo vyumba zilikuwa kwenye mzunguko wa hilo lango, vivyo hivyo kulikuwa na madirisha yaliyozunguka kuelekeana na ua na juu ya kila nguzo kulikuwa na mapambo ya miti ya mitende.

Ukumbi Wa Nje

17Kisha akanileta katika ukumbi wa nje. Huko nikaona vyumba vingine pamoja na njia iliyokuwa imejengwa kuzunguka ukumbi wote, kulikuwa na vyumba thelathini vimepangana kando ya hiyo njia. 18Njia hii iliyojengwa iliambaa na lango, ikiwa na urefu sawa na lango, hii ilikuwa ni njia ya chini. 19Kisha akapima umbali kutoka ndani ya lango la chini mpaka nje ya ukumbi wa ndani, nao ulikuwa dhiraa mia moja
40.19 Dhiraa 100 ni sawa na mita 45
upande wa mashariki na dhiraa mia moja upande wa kaskazini.

Lango La Kaskazini

20Kisha akapima urefu na upana wa lango linaloelekea kaskazini, kukabili ukumbi wa nje. 21Vyumba vyake vilikuwa vitatu kila upande, kuta zilizogawanya vyumba na baraza ilikuwa na vipimo sawa na zile kuta za lango la kwanza. Zilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wa dhiraa ishirini na tano
40.21 Dhiraa 25 ni sawa na mita 11.25
.
22Madirisha yake, baraza yake na nakshi yake ya miti ya mitende vilikuwa na vipimo sawasawa na vile vya lango linaloelekea mashariki. Kulikuwa na ngazi saba za kupandia huko, pamoja na baraza yake mkabala nazo. 23Kulikuwa na lango kwenye ukumbi wa ndani lililoelekea lile lango la kaskazini, kama vile ilivyokuwa ule upande wa mashariki. Akapima kutoka lango moja hadi lile lililo mkabala nalo, lilikuwa dhiraa mia moja.

Lango La Kusini

24Ndipo akaniongoza mpaka upande wa kusini, nami nikaona lango linaloelekea kusini. Akaipima miimo yake na baraza yake, navyo vilikuwa na vipimo sawa kama hivyo vingine. 25Lango na baraza yake vilikuwa na madirisha membamba pande zote, kama madirisha ya huko kwingine. Ilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wake dhiraa ishirini na tano. 26Kulikuwa na ngazi saba za kupandia huko, pamoja na baraza yake mkabala nazo, ilikuwa na nakshi ya miti ya mitende kwenye kuta zinazogawanya vyumba kila upande. 27Ukumbi wa ndani pia ulikuwa na lango linaloelekea kusini, naye akapima kutoka lango hili mpaka kwenye lango la nje upande wa kusini, ilikuwa dhiraa mia moja.

Malango Ya Kuelekea Ukumbi Wa Ndani

28Kisha akanileta mpaka ukumbi wa ndani kwa kupitia lango la kusini, naye akapima lango la kusini, ambalo lilikuwa na vipimo sawa na yale mengine. 29Vyumba vyake, kuta zilizogawanya vyumba na ukumbi wake zilikuwa na vipimo sawasawa na zile nyingine. Hilo lango na baraza yake vilikuwa na madirisha pande zote. Navyo vilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wa dhiraa ishirini na tano. 30(Baraza za malango zilizozunguka ukumbi wa ndani zilikuwa na upana wa dhiraa ishirini na tano na kina cha dhiraa tano.) 31Baraza yake ilielekeana na ukumbi wa nje, miimo yake ilinakshiwa miti ya mitende, kulikuwa na ngazi nane za kupandia huko.

32Kisha akanileta mpaka kwenye ukumbi wa ndani ulioko upande wa mashariki, naye akalipima lango hilo, lilikuwa na vipimo vilivyo sawasawa na yale mengine. 33Vyumba vyake, kuta zake na baraza yake vilikuwa na vipimo vilivyo sawa na vile vingine. Lile lango pamoja na baraza yake vilikuwa na madirisha pande zote. Urefu wake ulikuwa dhiraa hamsini na upana wake dhiraa ishirini na tano. 34Baraza yake ilielekea ukumbi wa nje, miimo yake ilinakshiwa miti ya mitende pande zote. Kulikuwa na ngazi nane za kupandia huko.

35Kisha akanileta mpaka kwenye lango la kaskazini na kulipima. Lilikuwa na vipimo sawa na yale mengine, 36kama vile ilivyokuwa kwa vyumba, kuta zake na baraza yake, tena kulikuwa na madirisha pande zote. Ilikuwa na urefu wa dhiraa hamsini na upana wake dhiraa ishirini na tano. 37Baraza yake ilielekeana na ukumbi wa nje, miimo yake ilinakshiwa miti ya mitende pande zote, kulikuwa na ngazi nane za kupandia huko.

Vyumba Vya Kutayarishia Dhabihu

38Kulikuwa na chumba na mlango karibu na baraza katika kila njia ya ndani ya lango ambamo sadaka za kuteketezwa zilioshwa. 39Kwenye baraza ya lile lango kulikuwepo meza mbili kila upande, ambako sadaka za kuteketezwa, sadaka za dhambi na sadaka za hatia zilichinjiwa. 40Karibu na ukuta wa nje wa baraza ya lile lango karibu na ngazi kwenye ingilio kuelekea kaskazini kulikuwa na meza mbili, nako upande mwingine wa ngazi kulikuwepo na meza mbili. 41Kwa hiyo kulikuwa na meza nne upande mmoja wa lango na nyingine nne upande mwingine, zote zilikuwa meza nane, ambapo dhabihu zilichinjiwa. 42Pia kulikuwa na meza nne za mawe yaliyochongwa kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, kila meza ilikuwa na urefu wa dhiraa moja na nusu
40.42 Dhiraa 1.5 ni sawa na sentimita 67.5
, upana wake dhiraa moja na nusu na kimo cha dhiraa moja. Juu ya meza hizo viliwekwa vyombo vya kuchinjia sadaka za kuteketezwa na dhabihu nyingine mbalimbali.
43Kulikuwa na kulabu, urefu wake nyanda nne
40.43 Nyanda 4 ni sawa na sentimita 8
, zilikuwa zimeshikizwa ukutani pande zote. Meza zilikuwa kwa ajili ya nyama za sadaka.

Vyumba Kwa Ajili Ya Makuhani

44Nje ya lango la ndani, kwenye ukumbi wa ndani, kulikuwa na vyumba viwili, kimoja upande wa lango la kaskazini nacho kilielekea kusini, kingine upande wa lango la kusini nacho kilielekea kaskazini. 45Akaniambia, “Chumba kinachoelekea upande wa kusini ni kwa ajili ya makuhani ambao wana usimamizi wa hekaluni, 46nacho chumba kinachoelekea upande wa kaskazini ni kwa ajili ya makuhani wenye usimamizi wa madhabahuni. Hawa ni wana wa Sadoki, ambao ndio Walawi pekee wanaoweza kumkaribia BWANA ili kuhudumu mbele zake.”

47Ndipo alipopima ukumbi: nao ulikuwa mraba wa dhiraa mia moja urefu na upana. Madhabahu ilikuwa mbele ya Hekalu.

Hekalu

48Akanileta mpaka kwenye baraza ya Hekalu naye akaipima miimo ya hiyo baraza, nayo ilikuwa na upana wa dhiraa tatu
40.48 Dhiraa 3 ni sawa na mita 1.35
kila upande. Upana wa ingilio ulikuwa dhiraa kumi na nne
40.48 Dhiraa 14 ni sawa na mita 6.3
na kuta zake zilikuwa na upana wa dhiraa tatu kila upande.
49Baraza ilikuwa na dhiraa ishirini kwenda juu na dhiraa kumi na mbili
40.49 Dhiraa 12 ni sawa na mita 5.4
kuanzia mbele hadi nyuma. Kulikuwa na ngazi kumi za kupandia huko, pia kulikuwa na nguzo kwa kila upande wa miimo.

Copyright information for Neno