Ezekiel 5

Upanga Dhidi Ya Yerusalemu

1“Mwanadamu, sasa chukua upanga mkali na uutumie kama wembe wa kinyozi ili kunyolea nywele za kichwa chako na ndevu zako. Kisha uchukue mizani ya kupimia ukazigawanye nywele hizo. 2Wakati siku zako za kuzingirwa zitakapokwisha, choma theluthi moja ya hizo nywele zako kwa moto ndani ya mji. Chukua theluthi nyingine ya hizo nywele uzipige kwa upanga kuuzunguka mji wote na theluthi nyingine ya mwisho utaitawanya kwa upepo. Kwa kuwa nitawafuatia kwa upanga uliofutwa. 3Lakini chukua nywele chache uzifungie ndani ya pindo la vazi lako. 4Tena chukua nywele nyingine chache uzitupe motoni uziteketeze. Moto utaenea kutoka humo na kufika katika nyumba yote ya Israeli.

5“Hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Huu ndio Yerusalemu ambao nimeuweka katikati ya mataifa ukiwa umezungukwa na nchi pande zote. 6Lakini katika uovu wake umeasi sheria na amri zangu kuliko mataifa na nchi zinazouzunguka. Umeasi sheria zangu wala haukufuata amri zangu.

7“Kwa hiyo hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo: Ninyi mmekuwa wakaidi kuliko mataifa yanayowazunguka na hamkufuata amri zangu wala kuzishika sheria zangu. Wala hamkuweza hata kuzifuata kawaida za mataifa yanayowazunguka.

8“Kwa hiyo, hili ndilo BWANA Mwenyezi asemalo, Mimi mwenyewe, niko kinyume nanyi Yerusalemu, nitawapiga kwa adhabu yangu mbele ya mataifa. 9Kwa ajili ya sanamu zenu zote za machukizo, nitawafanyia kile ambacho kamwe sijawafanyia kabla wala kamwe sitawafanyia tena. 10Kwa hiyo katikati yenu baba watakula watoto wao na watoto watakula baba zao. Nitawapiga kwa adhabu, nami nitawatawanya watu wenu walionusurika pande zote za dunia. 11Kwa hiyo hakika kama niishivyo, asema BWANA Mwenyezi, kwa kuwa mmenajisi mahali pangu patakatifu kwa sanamu zenu mbaya sana na desturi zenu za machukizo, mimi mwenyewe nitaondoa fadhili zangu kwenu. 12Theluthi ya watu wako watakufa kwa tauni au kwa njaa humu ndani yako, theluthi nyingine itaanguka kwa upanga nje ya kuta zako, nayo theluthi nyingine nitaitawanya kwenye pande nne kuwafuatia kwa upanga uliofutwa.

13“Ndipo hasira yangu itakapokoma na ghadhabu yangu dhidi yao itatulia, nami nitakuwa nimelipiza kisasi. Baada ya kuimaliza ghadhabu yangu juu yao, watajua kuwa mimi BWANA nimenena katika wivu wangu.

14“Nitakuangamiza na kukufanya kitu cha kudharauliwa miongoni mwa mataifa yanayokuzunguka, machoni pa watu wote wapitao karibu nawe. 15Utakuwa kitu cha kudharauliwa na cha aibu, cha dhihaka, ovyo na kitu cha kutisha kwa mataifa yanayokuzunguka, nitakapokupiga kwa adhabu yangu katika hasira na ghadhabu yangu kwa kukukemea kwa ukali. Mimi BWANA nimesema. 16Nitakapokupiga kwa mishale yangu ya kufisha na yenye kuharibu ya njaa, nitaipiga ili kukuangamiza. Nitaleta njaa zaidi na zaidi juu yako na kukomesha upatikanaji kwako wa chakula. 17Nitapeleka njaa na wanyama wa mwituni dhidi yenu, navyo vitawaacha bila watoto. Tauni na umwagaji wa damu utapita katikati yenu, nami nitaleta upanga juu yenu. Mimi BWANA nimenena haya.”

Copyright information for Neno