Ezra 5

Barua Ya Tatenai Kwa Dario

1Ndipo nabii Hagai na nabii Zekaria mzao wa Ido, wakawatolea unabii Wayahudi waliokuwa Yuda na Yerusalemu kwa jina la Mungu wa Israeli, aliyekuwa pamoja nao. 2Ndipo Zerubabeli mwana wa Shealtieli na Yeshua mwana wa Yosadaki wakaanza kujenga tena nyumba ya Mungu huko Yerusalemu. Nao manabii wa Mungu walikuwa pamoja nao, wakiwasaidia.

3Wakati ule Tatenai mtawala wa ng'ambo ya mto Eufrati na Shethar-Bozenai na wenzao waliwaendea, wakawauliza, “Ni nani aliyewapa ruhusa ya kujenga tena Hekalu hili na kurudishia upya kama lilivyokuwa?” 4Pia waliwauliza, “Je, majina ya watu wanaofanya ujenzi huu ni nani?” 5Lakini jicho la Mungu wao lilikuwa likiwaangalia wazee wa Wayahudi, nao hawakuzuiliwa kujenga mpaka taarifa ikaandikwa kwa Dario na majibu yake kupokelewa.

6Hii ni nakala ya barua ile Tatenai, mtawala wa ng'ambo ya mto Eufrati na Shethar-Bozenai na wenzao maafisa wa ng'ambo ya mto Eufrati waliyompelekea Mfalme Dario. 7Taarifa waliyompelekea ilisomeka kama ifuatavyo:Kwa Mfalme Dario:Salamu kwa moyo mkunjufu.8Inampasa Mfalme ajue kwamba tulikwenda katika eneo la Yuda, kwenye Hekalu la Mungu mkuu. Watu wanalijenga kwa mawe makubwa na kuweka mbao kwenye kuta. Kazi inafanyika kwa bidii na inaendelea kwa haraka chini ya uongozi wao.

9Tuliwauliza viongozi, “Ni nani aliyewapa ruhusa kujenga upya Hekalu hili na kurejesha hali ya jengo kama lilivyokuwa?” 10Pia tuliwauliza majina yao, ili tukuandikie kukujulisha majina ya viongozi wao.11Hili ndilo jibu walilotupa:“Sisi ni watumishi wa Mungu wa mbingu na nchi, nasi tunalijenga upya Hekalu ambalo lilijengwa miaka mingi iliyopita, lile ambalo mfalme mkuu wa Israeli alilijenga na kulikamilisha.
12Lakini kwa sababu baba zetu walimkasirisha Mungu wa mbinguni, basi aliwatia mkononi mwa Nebukadneza, Mkaldayo, mfalme wa Babeli, ambaye aliliharibu Hekalu hili na kuwaondoa watu na kuwapeleka uhamishoni huko Babeli.

13“Pamoja na hayo, katika mwaka wa kwanza wa kutawala Koreshi mfalme wa Babeli, Mfalme Koreshi alitoa amri ya kujengwa upya nyumba hii ya Mungu. 14Yeye hata aliviondoa vyombo vya dhahabu na fedha vya nyumba ya Mungu, kutoka Hekalu la Babeli ambavyo Nebukadneza alikuwa amevichukua kutoka ndani ya Hekalu huko Yerusalemu na kuvileta katika Hekalu la Babeli.

“Vyombo hivyo Mfalme Koreshi alimkabidhi mtu aliyeitwa Sheshbaza, ambaye Koreshi alikuwa amemteua awe mtawala,
15naye akamwambia, ‘Chukua vyombo hivi uende ukaviweke ndani ya Hekalu huko Yerusalemu. Nawe uijenge upya nyumba ya Mungu mahali pake.’ 16Hivyo huyu Sheshbaza alikuja na kuweka misingi ya nyumba ya Mungu iliyoko Yerusalemu. Tangu siku hiyo hadi sasa imekuwa ikiendelea kujengwa lakini bado haijamalizika.”17Sasa kama ikimpendeza mfalme, uchunguzi na ufanyike katika kumbukumbu ya maandishi ya kifalme mjini Babeli kuona kama kweli Mfalme Koreshi alitoa amri ya kujenga upya nyumba ya Mungu katika Yerusalemu. Kisha tunaomba mfalme na atutumie uamuzi wake kuhusu jambo hili.

Copyright information for Neno