Galatians 6

Chukulianeni Mizigo

Ndugu zangu, ikiwa mtu ameghafilika akatenda dhambi, basi ninyi mlio wa rohoni, mrejezeni upya mtu huyo kwa roho ya upole. Lakini jihadharini, ili ninyi wenyewe msije mkajaribiwa. Chukulianeni mizigo ninyi kwa ninyi, nanyi kwa njia hii mtatimiza sheria ya Kristo. Kama mtu ye yote akijiona kuwa yeye ni bora na kumbe sivyo, basi mtu huyo anajidanganya mwenyewe. Lakini kila mtu na aipime kazi yake mwenyewe, ndipo aweze kujisifu, bila kujilinganisha na mtu mwingine. Kwa maana, kila mtu atauchukuwa mzigo wake mwenyewe. Basi, yeye afundishwaye katika neno na amshirikishe mwalimu wake mema yote.

Msidanganyike, Mungu hadhihakiwi. Kwa kuwa kile apandacho mtu ndicho atakachovuna. Apandaye kwa mwili, katika mwili wake, atavuna uharibifu, lakini yeye apandaye katika Roho, katika Roho atavuna uzima wa milele. Hivyo, tusichoke katika kutenda mema, kwa kuwa tutavuna kwa wakati wake tusipokata tamaa. 10 Kwa hiyo, kadiri tupatavyo nafasi na tuwatendee watu wote mema, hasa wale wa jamaa ya waaminio.

Si Kutahiriwa Bali Kuwa Kiumbe Kipya

11 Angalieni ni herufi gani kubwa nitumiazo ninapowaandikia kwa mkono wangu mwenyewe!

12 Wale wanaotaka kuonekana wazuri kwa mambo ya mwili wanaotaka wawalazimishe kutahiriwa, sababu pekee ya kufanya hivyo ni kuepuka kuteswa kwa ajili ya msalaba wa Kristo. 13 Hata wale waliotahiriwa wenyewe hawaitii sheria, lakini wanataka ninyi mtahiriwe ili wapate kujivuna kwa habari ya miili yenu. 14 Mungu apishie mbali nisije nikajivunia kitu cho chote isipokuwa msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo, ambaye kwa yeye ulimwengu umesulibiwa kwangu, nami nimesulibiwa kwa ulimwengu. 15 Kwa maana katika Kristo Yesu kutahiriwa au kutokutahiriwa si kitu, bali kule kuwa kiumbe kipya ni kila kitu! 16 Amani na rehema viwe na wote wanaofuata kanuni hii na juu ya Israeli wa Mungu.

17 Hatimaye, tangu sasa mtu ye yote asinitaabishe, kwa maana nachukua katika mwili wangu chapa zake Yesu.

18 Ndugu zangu, neema ya Bwana wetu Yesu Kristo ikae pamoja na roho zenu. Amen.

Copyright information for Neno